Wateule wa Rais katendeni kwa viwango

Muktasari:

  • Tukiwa tunahitimisha siku 21 za maombolezo ya hayati John Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuijenga Serikali itakayowatumikia wananchi.

Tukiwa tunahitimisha siku 21 za maombolezo ya hayati John Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuijenga Serikali itakayowatumikia wananchi.

Rais Samia alianza kwa kuijaza nafasi aliyoiacha na Bunge likamthibitisha Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais, halafu akambadili Dk Bashiru Ally kwa kumteua Hussein Kattanga kuwa katibu mkuu kiongozi.

Hakumgusa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa bali aliwahamisha baadhi ya mawaziri na kuwaongeza wachache. Juzi amefanya mabadiliko kadhaa kwa makatibu wakuu na manaibu wao. Aliwaongeza baadhi ya wakuu wa mashirika ya umma na taasisi nyeti.

Mabadiliko machache yaliyofanywa yanamaanisha mategemeo makubwa aliyonayo Rais Samia kwa wasaidizi wake. Anafahamu udhaifu uliokuwapo hivyo anataka damu mpya itakayobadili mambo.

Wateule waliopelekwa kwenye wizara, taasisi au mashirika ya umma, wahakikishe wanatenda tofauti na watangulizi wao. Wawe wabunifu wa kusimamia mapato na matumizi. Waimarishe uwajibikaji na huduma bora kwa wananchi.

Hapa kuna wapya na waliobadilishiwa ofisi. Kwa wapya wachache walioteuliwa wameaminiwa ndio maana wamepandishwa cheo. Wakumbuke kuna wenzao wengi wamewaacha nyuma wakiwa na sifa zinazotosha kukaa kwenye nafasi hizo, na kuteuliwa kwao sio upendeleo bali kwa kuwa wana sifa za ziada.

Kuonyesha kuwa haikuwa bahati mbaya kuteuliwa kwao, ni lazima waonyeshe utofauti kwa kuongeza ufanisi wa wizara au taasisi waliyokabidhiwa. Uongozi ni dhamana wakati wote, hivyo wawajibike kwa kukidhi matarajio ya mteule na wananchi wanaowahudumia.

Wapo waliohamishwa. Hii nayo ni fursa kwamba wanaweza kuongeza ufanisi wa hizo ofisi mpya kama walivyofanya walikotoka. Rais angeweza kuwaacha lakini amewaona bado wana umuhimu wa kumsaidia. Wakatende yanayopaswa. Hakuna kingine kinachotarajiwa zaidi ya wao kukaza buti.

Rais anajaza nafasi muhimu zitakazomsaidia kufanikisha malengo ya kuwa na Tanzania yenye uchumi imara. Wakati ujenzi wa miundombinu itakayosaidia kukuza uchumi ikiendelea kujengwa nchini, usimamizi makini unahitaji kuipata thamani ya fedha na kuikamilisha kwa wakati.

Kuiweka Tanzania yenye uchumi wa kati sehemu salama, Taifa linapaswa kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia nane kwa mwaka mpaka mwaka 2026. Kufanikisha hili, tunahitaji watendaji makini wenye uwezo wa kutatua kero kwa haraka.

Wateule wote wanapaswa kukumbuka kwamba bado maadui watatu waliobainishwa na Mwalimu Julius Nyerere tunaendelea kupambana nao. Hao ni ujinga, maradhi na umasikini. Takwimu zinaonyesha kuna zaidi ya Watanzania milioni 14 wanaoishi kwenye ufukara. Hawana uhakika na mlo wa kila siku, makazi wala mavazi.

Tanzania inapambana na magonjwa ambayo kwingineko duniani yamedhibitiwa. Wapo Watanzania wanaopoteza maisha kwa maradhi yanayosababishwa na uchafu. Ingawa sasa elimu ni bure, kuna wazazi hawawapeleki watoto wao shule au huwakatisha masomo hivyo kulifanya Taifa kuendelea kuwa na idadi ya watu wasiojua kusoma wala kuandika.

Wateule hawa wana majukumu makubwa kulivusha Taifa. Atakayelegalega asishangae akipumzishwa awapishe wenye kasi zaidi yake. Tunawaomba wasisite kumshauri Rais pia namna ya kunufaika na fursa za sayansi na teknolojia.