Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watoto 624,346 kupata chanjo ya polio Mkoa wa Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Juma Homera akizungumza na watendaji wa Serikali wakiwepo wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Kamati ya ulinzi na Usalama na Kamati ya Msingi ya Afya ngazi ya Jamii (PHC) leo Ijumaa Septemba 15, 2023. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Huku ikielezwa mkoa huo uko katika hatari ya watoto kuugua kufuatia kuibuka kwa kirusi kipya cha type 2 katika nchi jirani ya Malawi inayopakana na Mbeya.

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema kuwa watoto 614,346 walio na umri kati ya kuanzia 0 mpaka  miaka 8 watapatiwa matone ya chanjo ya polio huku akisisitisha maeneo ya mipakani kuwekewa utaratibu kwa wageni wanaoingia.

Homera amesema leo Ijumaa Septemba 15, 2023 wakati akizungumza Kamati ya Msingi ya Afya Ngazi ya Jamii (PHC) wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri zote na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ikiwa ni kuweka mikakati ya utoaji wa chanjo ili kukabiliana na ugojwa huo.

“Mkoa wa Mbeya uko katika hatari kubwa kwa watoto kupata ugonjwa wa polio kwani tayari kuna kirusi kimegundulika katika nchi  jirani ya Malawi sambamba na Mkoa wa Katavi. Ni wakati sasa wataalamu  kujipanga kikamilifu katika kuendesha zoezi hilo linalotarajia kuanza Septemba 21 mpaka 24 mwaka huu,” amesema.


Amesema kuwa mkoa umepokea dozi zaidi ya 700,000 ambazo zitatolewa katika vijiji 764 huku wataalamu 141,000 watasambazwa katika halmashauri zote lengo ni kutekeleza agizo la Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Hata Waziri Ummy akiwa kwenye ziara ya kikazi ametaja  Mkoa wa Mbeya kuwa miongoni mwa mikoa nchini uko  kwenye hatari ya watoto kupata ugonjwa wa polio  kutokana na kupakana na nchi jirani na mwingiliano wa watu na kuwataka  waganga wakuu, wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha zoezi hilo linawafikia watoto wote hata katika maeneo yasoyofikika,” amesema Homera.


Amesema chanjo ya mwaka huu imekuwa ya tofauti watoto watakaochanjwa ni kuanzia 0 mpaka miaka 8 ambapo miaka ya nyuma walikuwa wakipata walio chini ya miaka mitano.

“Nitumie tena fursa hii kumshukuru Rais Samia kwani anafanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani ya uchaguzi 2020 kwa kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama kwa kifikisha chanjo za magonjwa ya surua, Uviko 19, polio na mengineyo ambayo ni hatari kwa watoto,” amesema.

Upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa  Mkoa, Dk Elizabeth Nyema amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa zaidi ya Sh1.3 bilioni kwa ajili ya kuendesha zoezi chanjo ya polio kwa muda wa siku nne ikiwepo malipo kwa wataalamu, gharama za usafiri na mengineyo.

“Chanjo ya polio itafanywa katika halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, makanisani, misikitini, masokoni na maeneo ya shule za msingi lengo ni kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo kwani tayari kuna kesi moja ya mgonjwa imeripotiwa Mkoa wa Katavi,”amesema.

Amesema kuwa imebainika watoto waliozaliwa kati ya Mwaka 2013 ambao hawakupata chanjo wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo na kufuatia kuwepo kwa kirusi kilichoingia nchini Malawi ndiyo sababu ya zoezi hilo kufanywa kwa haraka ili kuokoa watoto kupata ulemavu na kupooza.


Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Zainab Nyamungumi amesema kuwa licha ya nchi za Zambia, Congo na Burundi kutoa chanjo lakini bado wanapaswa kuweka utaratibu kwa  watoto wanaosafiri kutoka nchi jirani kupatiwa chanjo maeneo mipakani.

“Utawekwa utaratibu maeneo ya mipakani kwani tayari kirusi cha polio kimeingia nchi Jirani ya Malawi ambayo inapakana na Mkoa wa Mbeya na kutokana na tabia ya kirusi hicho  kuhama hama ni lazima chanjo itolewe ili kuepuka kuleta madhara ya ulemavu na kupooza kwa watoto watakaobainika,”amesema.

Mkazi wa Jakalanda, Witness Joram amesema kikubwa elimu itolewe kwa wananchi hususan wa vijijini kujua umuhimu wa chanjo ili kuwaondoa na dhana ya chanjo inaleta ulemavu kwa watoto.