Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watoto milioni 10 kupata chanjo ya polio

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa na baadhi ya wazazi waliojitokeza kupata chanjo ya polio kwenye uzinduzi wa Kampeni ya utoaji wa chanjo kitaifa leo jijini Dodoma.

Muktasari:

Wizara ya Afya inatarajia kutoa chanjo kwa watoto zaidi ya milioni 10.5 ili kukabiliana na virusi vya polio nchini.

Dodoma/Mikoani. Wizara ya Afya inatarajia kutoa chanjo kwa watoto zaidi ya milioni 10.5 ili kukabiliana na virusi vya polio nchini.

Mkakati huo umekuja kutokana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza mlipuko wa ugonjwa huo Februari 2022 nchini Malawi.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya utoaji chanjo kitaifa jijini Dodoma leo Jumatano Mei 18, 2022 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema nchi ina jukumu la kuweka tahadhari kwakuwa nchi zilizotangazwa kuwepo kwa mlipuko huo ziko karibu ambapo hivi karibuni Msumbiji nayo imetangazwa kuwa na ugonjwa huo.

“Nchi ina mipaka yake lakini magonjwa hayana mipaka, sisi kama Serikali tuna wajibu wa kulinda watoto wetu kwakuwa nchi zilizotangazwa kuwepo na ugonjwa huo ni majirani zetu” amesema Waziri Ummy

Hata hivyo Waziri Ummy amewataka wasimamizi wa utoaji wa chanjo hiyo kuipa kipaumbele mikoa ya mipakani kwa kuongeza watendaji kazi na vifaa.

“Niagize tu katika utekelezaji wa zoezi hilo wasimamizi waone namna ya kuipa kipaumbele mikoa ya Mipakani kama vile Mtwara, Ruvuma kwa kuwaongezea watendaji kazi na vifaa vya kutosha”alisema

Amesema Serikali itawachukulia hatua wote watakaotumia ruzuku zilizotolewa kwa ajili ya zoezi hilo huku akiahidi kufanya tathmini ya hatari na ufuatiliaji wa ugonjwa huo mpaka katika ngazi ya mitaa.

Mikoa yaanza chanjo

Wakati Waziri Ummy akizindua utoaji chanjo kitaifa, baadhi ya mikoa nayo imefanya hivyo huku wananchi wakitakiwa kutoa ushirikiano na kupuuza upotoshaji juu ya chanjo hiyo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema wanatarajia kuchanja watoto 476,156 katika mitaa na vijiji 822.

Kwa upande wa mkoa wa Geita, mratibu wa chanjo mkoani humo, Wille Luhangija amewataka wananchi wa kuachana na uvumi na taarifa za upotoshaji za kuwa chanjo ya polio inayotolewa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni chanjo ya Uviko-19 huku mkoa huo ukitarajia kutoa chanjo kwa watoto zaidi ya 500,000.

"Niwatoe wasiwasi chanjo hii ni ya kawaida na nisalama kwa watoto tunatoa chanjo ya polio kwa watoto chanjo ya Uviko-19 tunaitoa kwa watu wazima na hii ya polio tunatoa kwa siku nne kwa watoto na tutakua na wataalam wanaopita nyumba kwa nyumba na tutaambatana na viongozi wa mitaa husika" amesema Luhangija.

 Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amewataka wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watalamu wa afya watakapopita kwenye maeneo yao ili waweze kukamilisha kampeni hiyo kwa urahisi.

Kunenge amesema kuwa mkoa huo unatarajiwa kutoa chanjo kwa zaidi ya watoto 200,000 wenye umri chini ya miaka mitano.

"Kampeni hii itafanyika nyumba kwa nyumba kwa siku tatu lakini baada ya muda huo watoto ambao watakuwa hawajapata huduma hiyo wataendelea kuhudumiwa kwenye vituo vya afya hivyo nitoe wito kwa wazazi kutoa ushirikiano katika hilo Ili kufikia lengo kusudiwa" amesema Kunenge

Kunenge ameyataja madhara ya ugonjwa wa polio kuwa ni pamoja na ulemavu wa ghafla wa viingo hivyo ambapo huathiri zaidi watoto wenye chini ya umri wa miaka 15.

Akizindua kampeni hiyo kwa Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa mkoa huo, Sophia Mjema amewasihi wazazi na walezi mkoani humo kuepuka maneno ya upotoshaji yanayosambazwa kuwa chanjo hiyo ina madhara.

Mjema amesema zaidi ya watoto 300,000 walio chini ya miaka mitano watapatiwa chanjo hiyo katika mkoa wa Shinyanga.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Waziri Kindamba amewaonya watu wanaotoa taarifa za upotoshaji juu ya chanjo hiyo na kusababisha taharuki na hofu kwa wananchi.

"Naomba nitoe rai kwa wananchi kuepuka taarifa zozote za upotoshaji kuhusiana na huduma zozote za chanjo kwani katika mambo haya mazuri tunayofanya na wabaya pia wamo" amesema Kindamba akizindua kampeni hiyo kimkoa

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wananchi wa mkoa huo kutopuuzia chanjo hiyo badala yake watumie fursa hiyo kuwapatia watoto wao chanjo hiyo.


Amesema kuwa Mkoa huo unatarajia kutoa matone ya chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wapatao 287,525.

Kagaigai ameyasema "Niwaombe sana wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanapatiwa chanjo, niwahakikishie kuwa chanjo hii ni salama na serikali imetumia gharama kubwa kupata chanjo hii," amesema Kagaigai.

Imeandikwa na Mainda Mhando (Dodoma), Rehema Matowo (Geita), Suzy Butondo (Shinyanga), Seif Jumanne (Njombe), Sanjito Msafiri (Pwani) na Janeth Joseph (Kilimanjaro)