Watoto wafa maji kwenye shimo la choo

New Content Item (1)

Waombolezaji wakiwa msibani.

Muktasari:

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro miili tayari imeshatolewa kwenye shimo hilo na wananchi

Morogoro. Watoto wawili waliokuwa wakiishi Mtaa wa Mkwajuni Manispaa ya Morogoro wamefariki dunia baada ya kuzama kwenye shimo la choo Aprili 23, 2024 lililochimbwa na jirani yao mwaka mmoja uliopita.

Watoto hao, Glory Geitan (12) na Neema Emmanuel (11) walikuwa wakiishi na bibi yao, Anastazia Mpilipili.

Akizungumzia siku ya tukio, Anastazia ameeleza  kuwa,  aliwaacha nyumbani na kuwataka wamsaidie kazi za nyumbani.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro limethibitisha kutokea kwa vifo hivyo.

Taarifa za kuwataka kwenda kufanya uokoaji ziliwafikia Aprili 23, 2024 saa 4:38 usiku, walipofika walikuta wananchi wameshawatoa.

“Jana saa 4:38 usiku tulipata wito wa uokoaji katika tukio la watoto wawili kuzama kwenye dimbwi la maji ambalo limesababishwa na uchimbaji wa shimo la choo maeneo ya Mindu, kwa hiyo tulitoka haraka kuelekea eneo la tukio tukakuta ile miili tayari imeshatolewa kwenye yale maji na wananchi.

“Tulichokifanya sisi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni kuchukua miili ya wale watoto tukawapeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, baada ya kufika madaktari wakatuthibitishia kuwa wameshafariki, kwa hivyo wakaenda kuhifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti,” amesema Sajenti Benjamin Bandula, kwa niaba ya Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Morogoro.

Amesema shimo hilo halikuwa na ulinzi wowote na majirani wanasema limekaa muda mrefu bila kufunikwa na mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha lifurike maji, jambo limesababisha madhara hayo kutokea.

“Jeshi la Zimamoto linawashauri wananchi wote wa Morogoro wanaoendelea na ujenzi, wajitahidi kuweka vizuizi au kufunika kabisa mashimo ya vyoo ili watoto na mifugo wasipate madhara kama haya,” amesema Sajenti Bandula.

Akisimulia mkasa huo, bibi wa watoto hao, Anastazia amesema siku hiyo alishinda na mjukuu wake Neema aliyekuwa anaumwa shingo, ilipofika saa 11 jioni, Glory naye alirudi kutoka shuleni, akawaacha na kwenda kufuata simu yake alikokuwa anachaji.

“Niliporudi saa 12 jioni nikakuta mlango umefungwa, nikaanza kuita kwa majina yao wakawa hawaitiki, nikarudi, mizigo niliyokuwa nayo nikaitunza jikoni, nikadhani wako kwa jirani, jua likazidi kuzama na nikawa siwaoni ikabidi nianze kupita kwa majirani nauliza,wakaniambia hawapo, nikazunguka kote nikawakosa, hata zile familia ambazo tumezoeana nikafika lakini sikuwapata.

“Nikakumbuka kwamba wakati naondoka wajukuu zangu niliwaacha na mtoto wa jirani, ikabidi niende nikamuulize kama amewaona, akaniambia yeye amewaacha wanapanga kwenda kuogelea kwenye shimo ambalo liko jirani na nyumbani,” amesimulia mwanamke huyo.

Amesema mawazo yake yote yakawa kwenye shimo hilo na baada ya kufika akakuta nguo za Neema zikiwa pembeni ya shimo, alipoangalia kwenye shimo akaona ndala za Glory zinaelea kwenye maji, akaangua kilio na kuomba msaada wa majirani.

Mama wa watoto hao, Veronica Kindanda huwa hakai na watoto wake hao aliowazaa na wanaume tofauti, bali anaishi kwa mume wake, na taarifa za vifo hivyo alizipata kupitia kwa majirani waliompigia simu.

“Kiukweli imeniuma sana kwa maana watoto wangu wameenda pamoja na hapa sina mtoto mwingine yeyote,” amesema mama huyo huku akilia kwa uchungu baada ya kuondokewa watoto wote wawili kwa mpigo.

Jirani yake bibi Anastazia, Maftaha Shaban amesema kuna haja ya Serikali ya mtaa huo kufukia mashimo yote ambayo yako wazi ili kunusuru watoto na vifo kama hicho.

“Hili tukio limetuhuzunisha, hawa watoto wamefariki pamoja na kuacha simanzi kubwa, kwa mtazamo wangu, Serikali ya mtaa inapaswa kuweka mkakati wa kuhakikisha mashimo yote ya choo ambayo yamechimbwa kwenye mtaa wetu na hayana vizuizi kwa watoto yafukiwe ili tuokoe maisha ya hawa watoto,” amesema.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Juma Ahmed Bilali amesema baada ya kupata taarifa za watoto hao kuzama kwenye shimo la choo walijaribu kuwaokoa watoto hao lakini haikuwezekana

“Kwa kuwa kuna mvua zinaendelea kunyesha, mpango wetu kwa sasa tutaanzisha msako wa kuhakikisha wale wenye mashimo hatarishi kama haya yanawekewa vizuizi ili kuepusha vifo kama hivi na wale watakaoshindwa tutayafukia mashimo hayo, hatuwezi kuvumilia kuona watoto wanakufa kisa uzembe wa baadhi ya watu,” amesema Ahmed.