Watoto wafariki kwa kuzama bwawani wazazi wakiwa msibani

Muktasari:
Watoto wawili wa familia moja katika Kitongoji cha Nkongolo Kijiji cha Kabila Kata ya Mondo Wilayani Kishapu, wamefariki dunia baada ya kuzama kwenye bwawa la maji lililopo jirani na makazi yao.
Shinyanga. Watoto wawili wa familia moja katika Kitongoji cha Nkongolo Kijiji cha Kabila Kata ya Mondo Wilayani Kishapu, wamefariki dunia baada ya kuzama kwenye bwawa la maji lililopo jirani na makazi yao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mondo, William Jijimya amesema watoto hao waliachwa na wazazi wao nyumbani kisha kwenda msibani kwenye kijiji cha Kabila.
Amewataja watoto waliofariki ni Meckline Dioniz (6) na Mbalu Dioniz (3) ambapo amesema wazazi wao waliporudi usiku hawakuwakuta nyumbani na kuanza kuwatafuta, ilipofika saa 4 usiku wakaupata mwili wa mtoto mmoja ukielea juu ya maji na baadaye wakaupata mwili wa mtoto mwingine.
Amesema juhudi za kuwatafuta watoto hao zimefanywa na wazazi kwa kushirikiana na wananchi wa kitongoji hicho baada ya kukusanyika usiku huo na kuanza kutafuta kisha kufanikiwa kuwapata wote wawili .
“Tukio hili limetusikitisha limetokea wakati wazazi wakiwa wameenda msibani na baada ya kurudi wamekumbana na mkasa huo wamepoteza watoto wote wawili hili nifundisho kwetu sisi wazazi watoto hawakuwa na mtu mzima wa kuwasimamia”amesema Jijimya
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola wamefika eneo la tukio ambapo miili ya watoto hao imefanyiwa uchunguzi na taratibu zingine kuendendelea.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa watoto hao waliachwa nyumbani bila uangalizi na ndipo wakakumbwa na umauti.