Watoto watano wa familia moja wafariki wakidhaniwa kula chakula chenye sumu

Muktasari:

  • Watoto watano wa familia moja wamefariki dunia katika kijiji cha Nyakanazi Wilaya ya Biharamlo mkoani Kagera kwa kile kinachosadikika kula chakula chenye sumu.

Biharamlo. Watoto watano wa familia moja wamefariki dunia katika kijiji cha Nyakanazi Wilaya ya Biharamlo mkoani Kagera kwa kile kinachosadikika kula chakula chenye sumu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kusema kuwa vimetokea kwa nyakati tofauti baada ya wanafamilia 11 kula chakula cha usiku Novemba 13, 2023.

Chatanda amesema, wanafamilia hao baada ya kula chakula cha usiku walienda kupumzika  lakini asubuhi yake watoto watatu  Brayan Ezekiel (2),  Kahindi Samson (9) ambaye ni mwanafunzi wa awali shule ya msingi Muungano na Happines Razaro (12) mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Muungano walianza kujisikia vibaya wakakimbizwa kituo cha afya Nyakanazi wakati wanaendelea na matibabu Novemba 14, 2023 wakapoteza maisha.

Amesema kuwa, baada ya watoto hao kupoteza maisha wengine watatu walianza kujisikia vibaya nao walipelekwa katika hospitali ya rufaa ya wilaya ya Biharamlo wakati wakiendelea na matibabu Novemba 15, 2023 wawili walipoteza maisha na hivyo idadi ya waliofariki kuwa watano.

Wawili waliofariki ni Melisiana Razaro (11) na Melina Razaro (9) huku Josephina Juma (5) akiendelea na matibabu katika hospitali hiyo.

Aidha amesema wanafamilia wengine ambao walishiriki chakula hicho akiwemo mama aliyepika wako salama na uchunguzi wa awali umebaini kuwa chakula kilikuwa na sumu na uchunguzi unaendelea kubaini ilikuwa ni sumu ya namna gani.

Amesema miili ya watoto watatu bado imehifadhiwa katika kituo cha afya Nyakanazi huku miili miwili ikiwa imehifadhiwa katika hospital ya rufaa ya wilaya ya Biharamlo.

Chatanda amasema wamechukua sampuli kwa ajili ya kuzipeleka kwa mkemia mkuu wa serikali.

Diwani wa kata ya Rusahunga Amos Madebwa amesikitishwa na vifo hivyo na kusema kuwa, alipokwenda hospitali daktari alimwambia watoto walikuwa wanabanwa kifua pamoja na maumivu ya tumbo.