Wawili wafariki dunia ajali ya gari na baiskeli Kiteto

Kiteto. Jeshi la Polisi wilayani Kiteto, mkoani Manyara linamshikilia dereva wa gari aina ya Mistubishi, Haruna Salumu (35) mkazi wa Kibaya kwa tuhuma za kusababisha vifo vya watu wawili waliokuwa kwenye baiskeli moja kwa kuwagonga kwa gari.

Taarifa hizo zinasema marehemu walikuwa wanaingia barabara kuu, waligongwa na gari hiyo iliyokuwa ikitokea makao makuu ya Wilaya ya Kiteto, Kibaya, kuelekea kata ya Sunya.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Manyara, ACP George Katabazi akizungumza na Mwananchi Digital leo,  jumapili Novemba 12.2023 amewataja marehemu hao kuwa ni dereva baiskeli, Matonya Lemtya (59) na abiria wake David Mayai (15) wote wakazi wa Logoit wilayani Kiteto

“Chanzo cha ajali ni, Matonya Lemtya (59) mwendesha baiskeli, huyu aliyekuwa  amepakia abiria aliingia barabara kuu ghafla bila tahadhari wakitokea kwenye chochoro na kugongwa na gari hilo,” amesema ACP Katabazi

Amesema tukio hilo limetokea Novemba 10 saa 12 jioni eneo la kitongoji cha Kona Kijiji cha Kijungu na kwamba miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi wa kidaktari na kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi

Kamanda Katabazi amesema dereva wa gari hilo Haruna salimu, amejisalimisha kituo kidogo cha Polisi Kijungu kwa ajili ya mahojiano zaidi huku vielelezo gari na baiskeli vikiwa katika kituo hicho cha Kijungu.

Katika hatua hiyo Kamanda Katabazi ametoa wito kwa madereva kuchukua tahadhari wanapokuwa barabarani na kuendesha vyombo vya moto akidai ajali nyingi zinasababishwa na uzembe ambao unaepukika

“Unapoendesha chombo cha moto barabarani lazima uchukue tahadhari…barabara sio wewe unayotumia pekee yako, ni vyema kuwa makini ili usilete madhara zaidi kama ilivyotokea kwa ajali hii ya watu wawili kupoteza maisha kwa wakati mmoja”amesema ACP Katabazi.