Wawili wafariki kwa kula chakula chenye sumu

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa

Muktasari:

  • Watu hao ni kati ya wanafamilia saba wa familia ya Jamila Rajabu (25) waliokula ugali na furu waliopikwa katika familia hiyo Jumamosi, Disemba 24 mwaka huu.

Mwanza. Jenipha Kishosha (27) na Godfrey Emmanuel (miezi sita) ambao ni wakazi wa Mtaa wa Chabakima Wilayani Ilemela mkoani Mwanza wamefariki kwa kula chakula chenye sumu.

  

Watu hao ni kati ya wanafamilia saba wa familia ya Jamila Rajabu (25) waliokula ugali na furu waliopikwa katika familia hiyo Jumamosi, Disemba 24, 2022.


Akizungumza leo Jumatano, Desemba 28, 2022 na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema wana familia hao baada ya kula chakula hicho walianza kutapika na kukimbizwa katika Kituo cha Afya Buzuruga ambapo wawili hao walifariki wakipatiwa huduma ya kwanza.


"Baada ya kula walianza kujisikia vibaya wakakimbizwa Kituo cha Afya kupatiwa matibabu, walipata maumivu makali ya tumbo na kutapika na kupoteza maisha wengine watano wamenusurika na wanaendelea na matibabu," amesema


Kamanda huyo amesema hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kwa kuhusika katika tukio hilo huku akisema Maofisa wa Jeshi hilo wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha sumu hiyo.


"Tumeanza kuchunguza unga na furu waliobaki kama mboga na ukoko kwenye sufuria kubaini ubag huo ulikuwa na kitu gani kilichowasababishia madhara na miili ya marehemu itachunguzwa kubaini sumu iliyokuwemo," amesema na kuongeza:


"Mpaka sasa hakuna mtu tunayemshikilia kuhusu tukio hilo lakini pamoja na kuchukua mabaki ya chakula hicho pia tumechukua matapishi ya marehemu ili kubaini aina ya sumu waliyokula, niwaomba wananchi kuwa makini na vyakula wanavyokula."