Watoto wawili wajeruhiwa kwa bomu Tabora

Muktasari:

  • Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema tukio hilo limetokea Jumatano asubuhi katika kijiji na kata ya Kabila ambapo walikuwa wakichunga ng’ombe ndani ya hifadhi ya Taifa ya Igombe na kuokota kitu ambacho walitaka kukifahamu kilikuwa nini.

Tabora. Watoto wa kijiji cha Kabila kilichopo katika manispaa ya Tabora wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao baada ya kulipukiwa na bomu walilolikata kwa kutumia panga wakitaka kufahamu kilikuwa ni kitu gani.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao amewataja waliojeruhiwa kuwa ni Kikombe Kishagembe (17) na Said Dulu (10) ambao ni wakazi wa kitongoji cha Igosha.

Amesema tukio hilo limetokea Jumatano asubuhi katika kijiji na kata ya Kabila ambapo walikuwa wakichunga ng’ombe ndani ya hifadhi ya Taifa ya Igombe na kuokota kitu ambacho walitaka kukifahamu kilikuwa nini.

Amesema vijana hao walichukua kitu hicho hadi nyumbani na kisha kutaka kufahamu kilikuwa na nini ndani yake, hivyo walichukua panga na kukata, ndipo mlipuko ukatokea na kuwajeruhi.

“Wamejeruhiwa sehemu kadhaa za miili yao ikiwemo kwenye mikono,miguuni na mapajani,” amesema.

Kamanda Abwao ameeleza kuwa uchunguzi wa awali umebainisha kuwa kitu hicho ni bomu aina ya Stick Hand Grunet na kwamba wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Amesema majeruhi wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora ya Kitete.