Watoto wawili waua kwa mapanga, wivu wa mapenzi wahusishwa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Caster Ngonyani akizungumzia tukio hilo. Picha na Mary Clemence

Katavi. Watoto wawili Maria Mtemvu (13) na Ester Enock (2); wakazi wa kitongoji cha Kabatini Kijiji cha Mpimbwe Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika, wameua kikatili kwa kukatwakatwa mapanga chanzo kikitajwa ni wivu wa kimapenzi.

Tukio hilo limeripotiwa kutokea Oktoba 3, 2023 saa 10:00 jioni kijijini hapo wakati mzazi wao Rose Kavuta (30), ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi Kabatini, akiwa anatekeleza majukumu yake shuleni hapo.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Caster Ngonyani, amesema marehemu Maria alikuwa mfanyakazi za ndani na Ester alikuwa mtoto wa mwalimu huyo.

Amesema Polisi wanawashikilia watu wanne wanaoshukiwa kuhusika na tukio hilo, ambapo uchunguzi wa awali umebaini kuwa mama wa watoto hao, alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mmoja wa watuhumiwa.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa baada ya mwalimu huyo kuachana na mtuhumiwa; alipata hasira na kuamua kutafuta wauaji, mmoja wao akiwa fundi aliyekuwa akichimba   kisima nyumbani hapo,”

Amewataja watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo kuwa ni pamoja na Dotto Machiya (37), Kija Maige (25), Moses Daud (52) na Yohana Leonard (35) wote wakazi wa Kijiji cha Mpimbwe.

“Tumewakamata wote, mmoja amekiri kufanya mauaji hayo amedai alitumwa na mpenzi wa mwalimu huyo kwenda kumuua asipomkuta aibe vitu vyote vya ndani,” amesema.

Aidha amesema baada ya kufika nyumbani hapo hakumkuta mwalimu kwani alikuwa kazini, hivyo akaamua kuingia ndani ili aibe kama alivyoelekezwa, lakini watoto walipiga kelele akawaua.

Amesema walipomhoji Mwalimu Rose, alikiri kuwa mmoja wa washukiwa wa mauaji hayo, alikuwa fundi wake wa kuchimba kisima lakini alishangaa usiku wa kuamkia siku ya tukio hilo, fundi huyo alikwenda nyumbani hapo bila sababu za msingi.

“Ilikuwa usiku saa nne alikuja akaingia ndani nikashtuka nikamuuliza umekuja kufanya nini akadai amekuja kutoa maji kwenye shimo la choo alilokuwa akichimba,”

“Nilishtuka sana nadhani alihisi nimemshtukia aliaga na kuniambia naenda nitarudi kesho, niliamka nikaenda shuleni baada ya kurudi nyumbani nikakuta unyama huo.

Hata hivyo Polisi wanaendelea kuwahoji watuhumiwa endapo upelelezi ukikamilika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amelaani vikali kitendo hicho akiahidi kuendelea kuwachukulia hatua watu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji.

“Nitoe rai kwa wananchi, hii tabia ni ya kinyama kabisa siyo utu waache kujichukulia sheria mkononi kwani watakaokiuka watawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Mrindoko