Watumishi wa umma kusahihishwa kwa kufuata mashauri ya nidhamu
Meneja Rasilimali Watu na Utawala (HR) wa mikoa ya Tanzania bara kutoka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) pamoja na maafisa utumishi wa Halmashsuri za Bunda na Tanga wakiwa kwenye mafunzo ya Uendeshaji wa Taratibu za Nidhamu yaliyoandaliwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida yanayoendelea mkoani Morogoro. Picha Lilian Lucas.
Muktasari:
- Serikali inatakiwa kuondokana na sintofahamu kwa kuingia kwenye gharama ya kulipa mtumishi anayeshitaki baada ya kuondolewa kazini.
Morogoro. Masuala ya nidhamu pamoja na kuwahusu watumishi wote waliopo kwenye utumishi wa umma bado wanatakiwa kusahihishwa kutokana na taratibu zilizoelezewa kwenye utumushi huo kwa kufuata mashauri ya nidhamu na si vinginevyo.
Mratibu wa Uendeshaji wa Taratibu za Nidhamu kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida, Assumpta Wambura amesema hayo Aprili 17, 2023 wakati mafunzo kwa Mameneja Rasilimali Watu na Utawala (HR) wa mikoa ya Tanzania bara kutoka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) pamoja na maafisa utumishi wa Halmashauri za Bunda na Tanga yanayoendelea mkoani Morogoro.
Wambura amesema Mashauri ya Nidhamu yamekuwa ni tatizo kwa watumishi si Tarura tu bali maeneo mengi ya umma hivyo watumishi wanatakiwa kufahamu mashauri ya nidhamu ukikosa wapi unatakiwa kuhukumiwa ama kufuata taratibu zipi za kufuata.
“Mtumishi wa umma anapaswa kujua kama atakuwa amepata uelewa wa mashauri ya nidhamu ni kwamba atakuwa yuko makini katika kujua kwamba nikikosea mahali hapa nitashitakiwa kwa kifungu namba furani,”amesema.
Mratibu huyo amesema maafisa utumishi wote Tanzania nzima wanapatiwa weledi ili waweze kupata uelewa wa uendeshaji wa masuala ya nidhamu kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na utumishi wa umma katika kumwadhibu mtumishi(au kumrekebisha) pale ambapo atakuwa ameenda kinyume na taratibu za utumishi huo wa umma.
Aidha amesema chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo hayo kwa viongozi ambao ni wakuu wa taasisi za umma, ziliwemo halmashauri na kwamba hii imekuwa ikisaidia na kuwaondoa hofu watumishi wa umma kwa kutoishi kwa wasiwasi na wanaweze kupata shida yoyote ambayo itakuwa imekwenda kinyume na taratibu za utumishi lakini ukapata stahiki ambayo inahusiana na lile shauri ambalo limefanywa.
“Taratibu za nidhamu ni ngumu, ili kuondokana na sintofahamu ambazo unakuta mtumishi amesimamishwa kazi kumbe taratibu hazikufuatwa baadae unakuta mtumishi anaidai serikali kiasi kikubwa cha fedha kwa kushindwa kufuata sheria na kanuni na kusababisha hasara kwa serikali,”amesema.
Mkurugenzi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma kampasi ya Singida Dk Hamisi Nalinga akimwakilisha mtendaji mkuu wa chuo hicho amesema mafunzo hayo ni miongoni mwa progaramu mbalimbali zinazoandaliwa na chuo Utumishi wa Umma Tanzania kwa ajili ya kuboresha utendaji katika utumishi na hiyo inalenga maeneo mahususi ambayo yanachangamoto katika utendaji wake.
Pia Nalinga amesema tayari Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala imeendelea kuuwisha sera na kanuani za utumishi wa umma ili kuendana na mazingira na mahitaji ya sasa katika ujenzi wa uchumi wa maendeleo ya taifa.
“Taarifa zilizopo toka tume ya utumishi wa umma eneo hilo limeonekena kuwa na changamoto kadhaa na kupunguza kuwepo kwa ufanishi wa ushughulikaji wa masuala ya nidhamu,”amesema.
Afisa Utumishi makamu makuu Tarura Selemani Luhunga amesema utumishi wa umma kumekuwa na changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo hivyo kwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo, mbinu, maarifa na akili mpya zenye uwezo wa kukabiliana masuala ya kinidhamu.
Wakaongeza kuwa mafunzo hayo ni faida kwa wakala huo kwani watakuwa na wataalamu wenye ujuzi na uelewa wa mambo ya nidhamu ambapo kupitia sheria mpya ya watumishi ya mwaka 2019 pamoja na kanuani zake za mwaka 2022 zimeleta marekebisho mbalimbali.
Luhunga akabainisha marekebisho yaliyofanyika ni pamoja na kuongezwa mambo mapya ikiwemo masuala ya uhujumu uchumi na mambo mengine yakiyoonekana kukidhi matakwa na mahitaji ya watumishi katika utumishi wa umma kwa wakati huu.