Watumishi wa umma zaidi ya 180,000 wapandishwa madaraja

Wednesday January 19 2022
watumishi pic

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi

By Mwandishi Wetu

Nkasi. Serikali imesema kuwa zaidi ya watumishi wa umma 180,000 wamepandishwa madaraja tangu Serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani.

 Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan aliapishwa Machi 19, 2021 baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amebainisha kuwa tangu Serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani zaidi ya watumishi wa umma 180,000 wamepandishwa madaraja huku Wilaya wa Nkasi ikinufaika na promosheni kwa watumishi wake 837 kupandishwa madaraja.

Ndejembi amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imejikita katika kuwaboreshea maisha watumishi wa umma huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu kazini.

"Rais Samia Suluhu Hassan ameweka kipaumbele kabisa katika kutatua changamoto zenu watumishi, Ndio maana katika kipindi kifupi alichoingia amefanya mambo makubwa kwa haraka ikiwemo upandishwaji wa madaraja, Haya ni mambo ambayo kwa muda mrefu mlikua hamjayapata”.

Amesema kuwa Ofisi ya Rais Utumishi itaendelea kutetea haki za watumishi wa umma akiahidi kuwa hakuna haki ya mtumishi yeyote itakayopotea na kuwataka kusikilizana kwenye utendaji.

Advertisement

“Watumishi hebu chapeni kazi kwa ubunifu, simamieni rasilimali fedha, simamieni rasilimali watu mnaowaongoza, ukiteuliwa kuwa Mkuu wa Idara tenga muda wa kuwasikiliza walio chini yako, wafuateni hadi katika ngazi ya kata msiishie kukaa maofisini tu, fanyeni kazi ya kumsaidia Rais wetu,"amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Pia ametoa wito kwa baadhi ya viongozi kuacha kuwafokea na kuwadhalilisha watumishi wa umma hadharani wanapokosea badala yake wafuate utaratibu wa kumuwajibisha mtumishi anapokosea kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye utumishi wa umma.

"Mtumishi wa umma anapokosea siyo busara kumfokea na kumdhalilisha hadharani, waiteni faragha muwaeleze wapi walipokosea, siyo vema kumfokea mtumishi mbele za watu tena wale anaowahudumia au kuwasimamia, tunataka watumishi wa umma waheshimiwe," amesema Ndejembi.

Advertisement