Watumishi waliofanya mzaha wa chanjo corona wasimamishwa kazi

Watumishi waliofanya mzaha wa chanjo corona wasimamishwa kazi

Muktasari:

  • Watumishi wawili wanaodaiwa kufanya mzaha wa maigizo ya kuwachoma sindano ya chanjo ya Covid-19 wamesimamishwa kazi kwa kukiuka maadili ya kazi.

Dar es Salaam, Watumishi wawili wanaodaiwa kufanya mzaha wa maigizo ya kuwachoma sindano ya chanjo ya Covid-19 wamesimamishwa kazi kwa kukiuka maadili ya kazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Ummy Mwalimu, leo Ijumaa, Agosti 6,2021 ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mkuu wa idara ya elimu msingi wa Halmashauri ya jiji la Arusha Omary Abdalahemedi Kwesiga kufuatia kufanya mzaha wa maigizo ya uchomaji sindano ya chanjo ya Covid-19.

Hata hivyo Waziri Ummy amemuagiza Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, kumchukulia hatua muuguzi wa Hospitali ya Mount Meru Arusha, Scholastica Kanje.

Ummy ametoa maagizo hayo leo Ijumaa, Agosti 6, 2021 siku moja baada ya video iliyosambaa mitandaoni inawaonyesha wawili hao wakifanya kitendo hicho.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini ofisi ya Rais Tamisemi, Nteghenjwa Hoseah imeeleza kuwa kitendo hicho ni kinyume cha taratibu na kanuni za utoaji wa huduma za chanjo na hivyo kuleta sintofahamu kwa wananchi.

“Kutokana na hali hiyo Waziri wa Tamisemi amemuagiza Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tamisemi kumsimamisha kazi mwalimu Omary Abdalahemedi Kwesiga pia ameagiza Scholastica Kanje ambaye ni ofisa muuguzi msaidizi apelekwe kwenye baraza la uuguzi na ukunga kwa hatua zaidi,” alieleza taarifa hiyo.

Mara baada ya agizo hilo, Msajili wa baraza la uuguzi na ukunga Tanzania, Agnes Mtawa ametangaza kumsimamisha kazi kwa miezi mitatu muuguzi wa Hospitali ya Mount Meru Arusha, Scholastica Kanje.

Msajili amesema Scholastica alifanya mzaha katika jambo hilo la kitaifa kwa kuigiza kumchoma sindano mteja na kusambaa mitandaoni suala linaloweza kuleta upotoshaji mkubwa na kuzua taharuki kwa wananchi.

“Kitendo hiki ni kinyume cha sheria ya uuguzi na ukunga ya mwaka 2010 (25)(3)(k) na maadili ya ukunga na uuguzi inayomtaka kila muuguzi afanye kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa na viwango.

“Kutokana na kitendo hicho nimemuagiza muuguzi mkuu wa mkoa ambaye ni msimamizi wa taaluma katika mkoa kumsimamisha kazi kwa kipindi cha miezi mitatu na kisha kutoa taarifa ya zoezi zima la lililosababisha muuguzi huyu kufanya mzaha huo ambayo itawasilishwa kwenye kikao cha baraza kwa maamuzi,” amesema Mtawa.