Watumishi wawili kortini kwa tuhuma za ‘ubadhirifu’

Muktasari:
- Gustav na Oberd ambao ni watumishi wa umma, wameshtakiwa kwa makosa mawili likiwemo la ubadhirifu na ufujaji fedha, wizi Sh19.97 milioni ambazo ni mali ya Kijiji cha Mapanda kilichopo wilayani Mufindi.
Mufindi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, imewafikisha mahakamani watu wawili kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh19 milioni, mali ya Kijiji cha Mapanda kilichopo wilayani hapa.
Washtakiwa hao ni Ofisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira, Jeswald Gustav pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mapanda, Oberd Francis Madembo ambapo wameshtakiwa kwa makosa mawili.
Kesi hiyo namba ECO 15/2023 imesomwa Desemba 1, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Mufindi, Edward Uphor na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Restituta Kessy akisaidiana na Husna Kyoba na Lisa Gwakisa Kasongwa.
Aidha ilielezwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka huyo kuwa Gustav na Oberd wanashtakiwa kwa makosa mawili, likiwemo la ubadhirifu na ufujaji na la wizi wa Sh19.97 milioni, mali ya Kijiji cha Mapanda kilichopo wilayani ya Mufindi, walipokuwa watumishi wa umma.
Mwendesha mashtaka Restituta amesema makosa hayo ni kinyume na kifungu cha 28 (1) cha PCCA na kifungu cha 258 (1) na (2) na 270 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.
Washtakiwa hao walipoulizwa walikana makosa hayo, hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 13, 2023 itakapotajwa tena.