Wauguzi wanolewa huduma kwa waliowekewa njia mbadala ya upumuaji

Baadhi ya wauguzi kutoka Idara ya upasuaji wa Sikio, Pua na Koo (ENT) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kuwekewa njia mbadala ya upumuaji (Tracheostomy). Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

  • Mgonjwa asipopatiwa huduma stahiki anaweza kupata madhara

Mwanza. Wauguzi 38 kutoka Idara ya upasuaji wa sikio, pua na koo (ENT) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini hapa,  wamejengewa uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kuwekewa njia mbadala ya upumuaji.

Mafunzo hayo yalifanyika jana Februari 24, 2024 hospitalini hapo na kusimamiwa na Kaimu Mkuu wa idara hiyo, Dk Rogers Machimu.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza madhara kwa wagonjwa waliowekewa njia mbadala ya upumuaji yanayoweza kujitokeza, kwa sababu zinazoweza kuzuilika.

Bila kuweka wazi idadi ya waliowekewa njia hiyo Bugando, Dk Machimu ametaja makundi ya wanaoweza kuhitaji upasuaji huo unaoongeza ufanisi katika upumuaji kuwa ni wagonjwa wenye saratani ya koo, walioziba njia ya juu ya upumuaji, waathirika wa ajali na waliolazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

Amesema njia ya hewa ni rahisi kuathirika, hivyo inahitaji huduma ya mtu ambaye ana utaalamu unaojitosheleza.

“Mgonjwa asipopatiwa huduma stahiki anaweza kupata madhara. Kupitia elimu hii kwa wauguzi tunaamini wagonjwa watakuwa salama,” amesema.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Bugando, Dk Bahati Wajanga akifunga mafunzo hayo ya siku mbili kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Fabian Masaga, amewataka wauguzi kutumia ujuzi walioupata kulinda usalama wa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji huo.

“Tunatarajia baada ya hapa sasa wagonjwa watakuwa salama. Katumieni ujuzi huu kuwahudumia wasipate maambukizi kwenye njia ya hewa ili kuifanya Bugando kituo cha utalii wa matibabu,” amesema Dk Wajanga.

Muuguzi, Jema Kamugisha akizungumza kwa niaba ya wauguzi walionufaika wa mafunzo hayo, ameahidi kutumia elimu waliyopatiwa kuboresha huduma na ustawi wa wagonjwa katika idara ya ENT hospitalini hapo.