Wavuvi ‘watema nyongo’ ziwa kufungwa, wagusia uvuvi haramu

Muktasari:

  • Ziwa Tanganyika lina ukubwa wa kilometa za mraba 32,900 huku Tanzania ikimiliki kilometa za mraba 13, 489, sawa na asilimia 41 ya ziwa lote.
  • Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonyesha asilimia 19 ya samaki waliozalishwa nchini mwaka 2021, zilitoka Ziwa  Tanganyika

Mwanza. Licha ya kueleza kushtushwa na tangazo la mpango wa Serikali wa kufunga shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika kwa kipindi cha miezi mitatu wakidai hawajashirikishwa, baadhi ya wavuvi ndani ya ziwa hilo wamependekeza mbinu mbadala wanazoamini zitalinda na kuhifadhi rasilimali ya uvuvi nchini.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Alhamisi Januari 10, 2024 kuhusu tangazo la kufunga shuguli hizo kwa miezi mitatu kuanzia Mei hadi Agosti 15, 2024, wavuvi hao wamesema taarifa za mpango huo wamezipata kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zikimnukuu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati wa ziara yake mkoani Kigoma.

Kupitia tangazo hilo, Waziri Ulega amesema kusitisha shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika kwa muda huo ni utekelezaji wa mikakati na Mkataba wa kikanda wa usimamizi wa uvuvi endelevu ambao pia unatekelezwa katika nchi za Burundi, Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) ambazo pia zinamiliki sehemu ya ziwa hilo.

Ziwa Tanganyika lina ukubwa wa kilometa za mraba 32,900 huku Tanzania ikimiliki kilometa za mraba 13, 489, sawa na asilimia 41 ya ziwa lote huku takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zikionyesha asilimia 19 ya samaki waliozalishwa nchini mwaka 2021, zilitoka ziwa hilo.

Akitoa maoni yake kuhusiana na hilo, Katibu wa Wavuvi Mkoa wa Kigoma, Bakari Almasi ameshauri kabla ya tangazo la uamuzi wa aina hiyo, ni vema Serikali kupitia taasisi zake ziwe zinawashirikisha wadau wanaohusika kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi ili kupata mawazo na uamuzi wa pamoja.

“Kushirikisha wadau kunatoa fursa ya kuchakata na kufikia maamuzi ya pamoja unaozingatia hoja, masilahi na manufaa ya pande zote kwa faida ya umma,’’ amesema Almasi huku akisisitiza kuwa maoni hayo hayalengi kupinga tangazo na mpango wa Serikali

Amesema kabla ya kufunga shughuli za uvuvi, ni vema Serikali ifikirie mbadala wa kipato kwa wavuvi na wote wanaoishi pembezoni mwa ziwa ambao maisha na kipato chao kinategemea sekta ya uvuvi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa wavuvi mkoani Kigoma, Francis John amesema kabla ya kutangaza uamuzi huo, Waziri Ulega alikutana na kufanya mazungumza na wavuvi wa Katonga wilayani Kigoma na kuwaeleza sababu ya Serikali kuchukua hatua hiyo.

Hoja ya wadau wote kushirikishwa kikamilifu pia imetolewa na Songoro Kitapile, mvuvi katika mwalo wa Buhingwe mkoani Kigoma akisema kama wangeshirikishwa mapema kabla ya tangazo la Serikali, wangeshauri ziwa lifungwe kati ya Aprili 15 hadi Julai 15 ambao ndio kipindi cha samaki na dagaa kuzaliana.

‘’Kwa kawaida, samaki na dagaa Ziwa Tanganyika huzaliana kati ya Mei hadi June kila mwaka; hivyo muda wa kufunga ziwa unapaswa kuwa katikati ya mwezi Aprili hadi katikati ya mwezi Julai. Ni bahati mbaya hatupati fursa ya kutoa mawazo na maoni yetu kwa sababu hatushirikishwi,’’ amesema Songoro.

Uvuvi haramu

Joshua Michael, mvuvi mwingine wa Ziwa Tanganyika ameshauri kampeni ya kuzuia shughuli za uvuvi iambatane na mikakati ya kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu ambalo ni tishio kuu kwa mazalia na rasilimali ya uvuvi nchini.

“Uvuvi haramu ni chanzo kikuu cha uharibifu na kupotea kwa mazao ya samaki kwa sababu wanaofanya aina hiyo ya uvuvi wanavua na kuharibu mazalia ya samaki. Lazima tuweke na kutekeleza mikakati madhubuti kukabiliana na tatizo hili katika maziwa yote nchini,’’ amesema na kushauri Joshua.