Wawili mbaroni tuhuma za mauaji ya mwanafunzi

Muktasari:

  • Mwanafunzi wa darasa la kwanza wilayani Butiama ameuawa, kisha mwili wake kutelekezwa kwenye kichaka jirani na shuleni kwao huku uchunguzi wa awali ukionyesha alinyongwa.

Musoma. Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Magharibi, Wilaya ya Butiama.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase amemtaja mwanafunzi aliyeuawa ni Kambarage Reuben (8), mkazi wa kijiji cha Mwibagi wilayani Butiama.

Kamanda Morcase amesema jana Februari 12, 2024 kuwa tukio hilo lilitokea Februari 8, 2024 jirani na shule alipokuwa akisoma mwanafunzi huyo.

"Siku hiyo binti huyo alichelewa kurudi nyumbani, wazazi wakapata wasiwasi wakaanza kumtafuta hadi shuleni, lakini walipofika shuleni walikuta wanafunzi wametawanyishwa hivyo wakaanza kumtafuta maeneo ya shuleni na kuukuta mwili wake ukiwa umelazwa kwenye kichaka jirani na shule huku ukiwa na sare za shule," amesema.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kifo chake kilitokana na kunyongwa na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea, huku akikataa kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa kuwa uchunguzi  bado unaendelea.

Katika tukio lingine, Isuto Matange (36) mkazi wa kijiji cha Majimoto wilayani Serengeti anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumkata na kuvitoa kabisa viganja viwili vya mikono ya mke wake, Kagembe George.

Kamanda Morcase amesema Mantage alimkata mkewe viganja vyake na kumjeruhi sehemu mbalimbali mwilini kwa kutumia panga walipokuwa njiani wakitoka mahakamani mjini Mugumu katika shauri lililokuwa likihusu ndoa yao.

"Tukio lilitokea Januari 8, 2024 saa 2 usiku wakati wakiwa njiani, Mantage aliingia kwenye shamba la mahindi na kutoka na panga kisha kuanza kumshambulia kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili kabla ya kuokolewa na wasamaria wema," amesema.

Kamanda Morcase amesema mwanamke huyo amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi.

Amesema baada ya tukio hilo mtuhumiwa alitoroka na baada ya msako uliofanywa na jeshi hilo alikamatwa katika visiwa vya Goziba, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera akiwa amejificha.

"Tulifanikiwa kumpata Februari 9, 2024 na hivi tunavyozungvumza yupo njiani analetwa huku kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria," amesema

Amesema chanzo cha ugomvi wa wanandoa hao ni baada ya mke wa mtuhumiwa kuondoka nyumbani kutokana na ukatili aliokuwa akifanyiwa kwa muda mrefu na mumewe.

Amesema mwanamke huyo alitorokea kusikojulikana kwa zaidi ya miezi mitatu, kisha mumewe kuamua kufungua kesi mahakamani na baadaye mwanamke alipatikana na kufika mahakamani.

"Baada ya hakimu kusikiliza pande zote alikataa ombi la mtuhumiwa la kurudiana na mke wake, kwani ilibainika mwanamke huyo alikuwa akifanyiwa ukatili kwa muda mrefu, uamuzi ambao mtuhumiwa hakukubaliana nao," amesema.

Amesema miongoni mwa vitendo vya ukatili alivyokuwa akifanyiwa mwamnke huyo ni pamoja na vipigo vya mara kwa mara, huku mume akishindwa kutimiza wajibu wake wa kulisha familia na jukumu hilo kumuachia mkewe na pale alipokuwa akikosa chakula kwa ajili ya familia alikuwa akipigwa bila kujali hakuacha fedha ya matumizi.