Waziri Mkuu Majaliwa kung’arisha siku ya amani kimataifa
Muktasari:
- Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema kesho Septemba 21 Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya amani duniani ambayo Kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro.
Moshi. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya amani duniani ambapo Kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro Septemba 21.
Kwa mara ya kwanza, siku ya amani Kimataifa iliadhimishwa Septemba 21 mwaka 1982 baada ya Baraza la umoja wa Mataifa kutangaza siku hiyo kuwa ndio siku maalum ya kukumbushana juu ya kuimarisha maadili ya amani.
Akitoa taarifa kwenye vyombo vya habari leo Jumanne, Septemba 20 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema maadhimisho hayo Kitaifa yanafanyika mkoani humo katika ukumbi wa Kuringe uliopo Manispaa ya Moshi ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Amani yetu, Maendeleo yetu.’
Amesema katika maadhimisho hayo kutakuwa na matembezi ya amani pamoja na mijadala ya kuelimisha na kukuza umoja na mshikamano katika Taifa.
"Septemba 21 shughuli zitafanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 8 mchana katika ukumbi wa Kuringe hapa Moshi na mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambapo shughuli mbalimbali yakiwemo matembezi ya amani yatafanyika kwa maandamano," amesema.
Babu aliwataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuja kumsikiliza Waziri mkuu na kusikiliza mada mbalimbali zitakayozungumzwa siku hiyo ikiwemo mijadala ya kuelimisha na kudumisha amani.
Naye Ofisa habari kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa, Stella Vuzo amesema kutokana na umuhimu wa siku hiyo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutterez anatarajia kugonga kengele maalumu ya amani mjini New York kukumbusha Amani.
Amesema maadhimisho hayo yatahudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Zlatan Milisic, viongozi wa dini, asasi za vijana pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali.