Waziri Nyansaho aipa UWT Sh125 milioni kwa mradi wa ufugaji samaki
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho akizungumza kwenye mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa UWT mkoa wa Mara. Picha na Beldina Nyakeke
Mbali na msaada huo, Dk Nyansaho ameahidi kuanza mchakato wa kutafuta fedha za ujenzi wa nyumba za watumishi wa UWT katika wilaya zote za mkoa wa Mara pamoja na makao makuu ya jumuiya hiyo mkoani humo.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho, ametoa zaidi ya Sh125 milioni kwa ajili ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria, hatua inayolenga kuimarisha uchumi wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Mara.
Mbali na msaada huo, Dk Nyansaho ameahidi kuanza mchakato wa kutafuta fedha za ujenzi wa nyumba za watumishi wa UWT katika wilaya zote za mkoa wa Mara pamoja na makao makuu ya jumuiya hiyo mkoani humo.
Akizungumza leo Alhamisi, Juni 18, 2026, mjini Musoma wakati wa kilele cha mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa UWT Mkoa wa Mara, Dk Nyansaho amesema fedha hizo zitatumika kuanzisha mradi wa vizimba vitano vya kufugia samaki katika Ziwa Victoria, mradi unaotarajiwa kuwa chanzo cha uhakika cha mapato kwa jumuiya hiyo.
Amesema wanawake wana mchango mkubwa katika kuimarisha amani, usalama, mshikamano na maendeleo ya taifa, lakini mafanikio ya majukumu hayo yanategemea uwepo wa msingi imara wa kiuchumi.
“Wanawake mna mchango mkubwa katika kusimamia mambo ya msingi katika nchi yetu, ikiwemo amani, mshikamano na umoja wa kitaifa. Hata hivyo, msingi wa yote hayo ni uchumi, hivyo ni muhimu UWT Mkoa wa Mara kuwa na uchumi imara,” amesema.
Dk Nyansaho amesema mazingira bora ya kazi, ikiwemo upatikanaji wa makazi mazuri kwa watumishi wa jumuiya hiyo, yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuchangia maendeleo endelevu ya UWT.
Pia, amewataka wanawake kuendelea kutekeleza wajibu wao katika malezi ya familia kwa kuzingatia maadili, upendo na hofu ya Mungu ili kujenga jamii na taifa lenye misingi imara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema Serikali ya mkoa huo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa lengo la kuinua ustawi wa wananchi na uchumi wa mkoa kwa ujumla.
Amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaendelea kupungua mkoani humo, huku juhudi zikielekezwa zaidi katika kufungua fursa za kiuchumi kwa wanawake.
Katibu wa UWT Mkoa wa Mara, Sophia Maregesi, amesema mafunzo hayo ya siku tatu yalilenga kuwajengea uwezo viongozi wa jumuiya hiyo kutoka mkoani na wilaya zote ili kuboresha utendaji wao.
Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mara, Nancy Msafiri, amesema washiriki walipata maarifa yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, huku wakianza maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 kwa lengo la kuimarisha ushindi wa chama hicho.