Waziri Ummy apiga ‘stop’ utaratibu mpya NHIF

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesitisha utaratibu mpya kwa wagonjwa wanaotumia bima za afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulioanza kutumika Jumatatu Agosti 1, 2022.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesitisha utaratibu mpya kwa wagonjwa wanaotumia bima za afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulioanza kutumika Jumatatu Agosti 1, 2022.

Utaratibu huo mpya unamtaka mgonjwa anayetumia kadi za NHIF akitibiwa kwenye hospitali moja kwa kutumia kadi hiyo kutotumia kadi hiyo katika hospitali nyingine mpaka apewe rufaa au mpaka siku 30 ziishe.

Waziri Ummy amesema “NHIF wayohoja ya kutaka kudhibiti gharama zisizo za lazima za matibabu lakini nilichowaelekeza leo, Nimeitaka NHIF kusimamisha utaratibu waliouanza leo mara moja”

Hata hivyo, amewaagiza NHIF kukaa na wadau wao kujadili changamoto zilizopo na kuja na utaratibu mzuri wa kuhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyofanya na baadhi ya hospitali.

“Ninawataka NHIF wakae na wadau wao, watoa huduma wa Serikali na binafsi, wajadiliane kuwa tumeona changamoto na tukubaliane tunakwenda kutatua changamoto hii vipi, kwa hiyo hilo swala nimeshalisimamisha” amesema

Agizo hilo la Waziri Ummy limekuja kukiwa na mjadala kwenye mitandao ya kijamii ikikosoa utaratibu huo mpya.

Akitoa agizo hilo, Waziri huyo ameelekeza watumiaji wa bima hiyo waendelee kupata huduma huku changamoto zikifanyiwa ufumbuzi.

Katika maelekezo yake Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi wanaotumia kadi hizo kutotumia hospitali nyingi kwa wakati moja.