Waziri Ummy: Pombe feki chanzo ongezeko magonjwa yasiyoambukiza

Waziri Ummy akizungumza alipokuwa akifungua  mkutano wa kwanza wa kujadili  magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika PEN-Plus ulioandaliwa na Shirika la Afya Duniani WHO jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Uzalishwaji wa pombe zisizo na ubora umetajwa kuwa mwiba kwa Serikali kutibia magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo athari zinazotokea katika ini, moyo na figo.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wakati unywaji wa pombe uliokithiri ukiongezeka nchini, uzalishaji wa pombe zisizo na ubora nao unaongezeka na kuwaweka Watanzania katika hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema licha ya kulichukua na kuanza kulifanyia kazi suala hilo, takwimu zinaonyesha unywaji pombe uliokithiri unazidi kuongezeka nchini kwa wastani wa lita 10.4 kwa mtu mmoja kwa mwaka, kutoka wastani wa lita 9.1 mwaka 2016.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 23, 2024 alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza uliokuwa ukizungumzia magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika PEN-Plus ulioandaliwa na Shirika la Afya Duniani WHO.

Waziri Ummy amesema wakati unywaji ukiongezeka, pombe feki zisizo na ubora nazo zinaongezeka,

“Juzi kiwanda cha pombe wameniletea malalamiko kwamba sisi tunazalisha pombe yenye ubora tena wameniomba kwamba watanipa ushahidi wa kiasi gani cha ambazo hazina ubora kinazalishwa na kinaingizwa  sokoni, hivyo kuwaweka Watanzania katika hatari ya magonjwa haya yasiyoambukiza.

“Ni eneo ambalo nalichukua tutaenda kulifanyia kazi na wenzetu wa TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na sheria yetu haiko vizuri sana kwamba nani anatakiwa kudhibiti masuala ya pombe,” amesema.

Amesema, “Tanzania tuna ongezeko la kiwango kikubwa cha unywaji wa pombe, wakati tumepunguza watu wanaokunywa pombe. Kitakwimu tulikuwa na watu wanaokunywa pombe kwa wastani asilimia 26 tumepunguza mpaka asilimia 20.”

“Lakini kiwango cha pombe kimeongezeka kutoka wastani wa lita 9.1 mwaka 2016 mpaka wastani wa lita 10.4 kwa mwaka, kwa hiyo kiwango cha watu kimepungua lakini wanakunywa sana,” amesema.

Amewataka Watanzania kuzingatia mafundisho ya wataalamu wa afya, kwani unywaji pombe kupita kiasi ni hatari kwa afya.

Amesema tabia za unywaji uliokithiri, kutokulala, tabia bwete na ulaji usiofaa ni miongoni mwa vichocheo vya magonjwa ya kisukari, ambayo kwa sasa asilimia tisa ya watu wazima nchini wanaugua. Pia amesema asilimia 15 ya Watanzania wanaugua shinikizo la juu la damu magonjwa yanayochangia asilimia 70 ya magonjwa ya moyo, figo na mengine yasiyo ya kuambukiza.

“Wenye magonjwa sugu ya figo asilimia 80 yao wana tatizo la kisukari au shinikizo la juu la damu.”

Akifungua mkutano huo mkubwa wa kwanza wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika, Waziri Ummy amesema Tanzania kama nchi nyingine za Afrika ina ongezeko kubwa la watu wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza,  kama shinikizo la damu, selimundu na majeruhi wanaotokana na ajali.

“Tutaendelea kuwekeza katika mikakati ya kinga na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kwenye kinga tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na magonjwa haya,” amesema.

Pamoja na hayo amesema utoaji wa huduma za magonjwa yasiyoambukiza upo mpaka katika ngazi za vituo vya afya, “Vituo sasa vina kliniki za magonjwa yasiyoambukiza, tumetoa mafunzo kwa wataalamu sasa hivi ukienda utapimwa  yote.”

Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyo ya kuambukiza Afrika wa WHO, DK Benido Impouma amebainisha kuwa mkutano huo umewakutanisha zaidi ya wadau 300 kutoka mataifa ya Afrika, Ulaya na watabadilisha maarifa namna ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti akishiriki mkutano huo kwa njia ya video amesema ulaji usio sahihi, ukuaji wa majiji na uchafuzi wa hali ya hewa yamekuwa  kichocheo cha magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema maradhi ya moyo, kisukari ni magonjwa yanayoathiri watoto na watu wazee kwa kiwango kikubwa kwa nchi zinazoendelea, hivyo nchi za Afrika  lazima ziwe na juhudi za pamoja kukabiliana na magonjwa hayo.

Naye Programu Ofisa wa Taasisi ya Leona, Harry Helmsley Charitable Trust  ya nchini Marekani,  James Reid amesema magonjwa ya yasiyoambukiza yameathiri watu wengi hivyo matumizi ya teknolojia ndio yatawasaidifia kuishi kwa muda mrefu.