Serikali yaandaa mtaala wa mafunzo ya magonjwa yasiyoambukiza

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mpendae, Toufiq Salim Turky (CCM) ambaye amehoji kuna mkakati gani wa kutoa elimu kuhusu Ugonjwa wa Saratani nchini Jumatatu April 24,2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Serikali imeandaa mtaala wa mafunzo wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani kwa watoa huduma wa ngazi za msingi ili kuwajengea uwezo wa kutoa elimu kwa jamii.

Dodoma. Serikali imeandaa mtaala wa mafunzo wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani kwa watoa huduma wa ngazi za msingi ili kuwajengea uwezo wa kutoa elimu kwa jamii.

 Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ameliambia bunge leo Jumatatu April 24,2023 kuwa, miongoni mwa mikakati mingine ni kuandaa vipindi mbalimbali na machapisho ya utoaji wa elimu ya afya dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo saratani.

Dk Mollel alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mpendae, Toufiq Salim Turky (CCM) ambaye amehoji kuna mkakati gani wa kutoa elimu kuhusu Ugonjwa wa Saratani nchini.

Naibu Waziri amesema serikali imekuwa ikitumia njia mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na ugonjwa wa saratani kupitia vipindi vya redio na televisheni, machapisho na magazeti, mitandao ya jamii kama Facebook, Instagram na Televisheni za sehemu za kusubiria wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya.

“Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kutoa elimu ya ugonjwa wa saratani kama ifuatavyo, Kuandaa kampeni mbalimbali za uelimishaji wa jamii na uchunguzi wa awali wa saratani nchini ikiwemo huduma Mkoba,” amesema Dk Mollel.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, kumekuwa na utaratibu wa kuendelea kutoa elimu katika maeneo mengi hasa yenye mkusanyiko ili kuwezesha mapambanao ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Tanzania inatumia Sh99.09 bilioni kutibu magonjwa yasiyoambukiza kwa mwaka, ikiwa gharama hiyo imeongezeka kutoka Sh35.65 bilioni mwaka 2016/2017.