Waziri wa zamani wa kilimo aibana Serikali ununuzi wa kahawa, Bashe amjibu

Wednesday April 28 2021
kahawapic
By Habel Chidawali

Dodoma. Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga ameibana Serikali akitaka kujua ni lini itaruhusu kampuni binafsi kununua kahawa moja kwa moja kutoka kwa wakulima bila kupitia vyama vya ushirika.

Hasunga ambaye ni waziri wa zamani wa kilimo ameeleza hayo bungeni mjini Dodoma leo Jumatano Aprili 28, 2021, pia alitaka majibu ya mkakati wa Serikali kufufua zao la kahawa nchini akisema ni zao la kimkakati.

Katika majibu yake Naibu Waziri wa Kilimo,  Hussein Bashe amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea kutekeleza mkakati wa miaka 10 wa maendeleo ya zao la Kahawa wenye lengo la kuongeza tija na ubora wa kahawa nchini.

Bashe utekelezaji wa mkakati huo umewezesha kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 43,872 za kahawa safi msimu wa 2017/18 hadi tani 67,583 kwa msimu wa 2020/21.

Amesema wastani wa bei kwa wakulima wa kahawa kavu ya Arabika imeongezeka kutoka Sh3,500 mwaka 2019/20 hadi Sh4,000 mwaka 2020/21 na bei ya kahawa ya maganda ya

Robusta imeongezeka kutoka Sh1,100 mwaka 2019/20 hadi

Advertisement

Sh1,200 mwaka 2020/21.

"Mfumo wa ununuzi wa Kahawa kupitia vyama vya ushirika umelenga kuongeza ushindani katika soko la awali kulingana na ubora wa kahawa na pia kuwawezesha wakulima kuwa na nguvu ya pamoja ya kushauriana ili kupata bei nzuri na kunufaika na kilimo hivyo kuondokana na walanguzi wanaowalaghai baadhi ya wakulima," amesema Bashe.

Amesema kampuni binafsi na wenye viwanda vya kahawa wanaruhusiwa kununua kahawa kutoka kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika vya msingi na vyama vikuu.


Advertisement