Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye ulemavu wafunuliwa fursa ununuzi wa umma

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania, Omary Itambu amesema elimu hiyo itawawezesha walemavu kujiajiri na kuajiri wengine.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania, Omary Itambu amesema utolewaji wa elimu na mafunzo ya ununuzi wa umma kwenye kundi la wenye ulemavu utawawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa zabuni za Serikali.

Amesema hayo kwenye hafla ya ugawaji wa vifaa saidizi vya mafunzo kwa Jumuiya ya Watu Wasioona, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) leo Mei 23, 2025 jijini Dar es Salaam, huku ikihudhuriwa na viongozi wa Serikali.

Itambu amesema mafunzo waliyopewa ni elimu kumbukizi inayowapa njia ya ununuzi wa umma kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).

“Tenda tutakazoomba serikalini zinahusisha usafi, sare na chakula. Sheria inataka taasisi zote za Serikali zinapofanya ununuzi lazima zitenge asilimia 30 kwa makundi maalumu,” amesema.

Redio hizo walizopewa na vitabu vya nukta nundu vina maelezo ya kupata tenda za Serikali, jinsi ya kujiunga na NeST pamoja na fursa zake.

Amesema vikundi vya walemavu vinapaswa kusajiliwa ili vipate sifa ya kukidhi vigezo vinavyohitajika ili kupata zabuni.

“Tunataka mafunzo haya yaenee nchi nzima ili waliopo na mikoa mingine wanufaike na mafunzo haya,” amesema Itambu.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba amesema lengo ni kuhakikisha makundi yote yanapata kazi, huku akisisitiza kuendeleza mafunzo hayo nchi nzima.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa mfumo wa NeST, zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh15 bilioni zimetolewa kwa watu wenye ulemavu, vijana na hata wazee.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, mgeni rasmi, Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Toba Nguvila amesema walemavu wanapaswa kushirikishwa katika mchakato mzima wa ununuzi wa umma sambamba na kupata zabuni za Serikali.

Aidha, amepongeza mafunzo waliyoyapata pamoja na vifaa hivyo saidizi katika kuwawezesha wao kupata tenda hizo.

Ikumbukwe walemavu hao wanaweza kuanzisha kikundi, wakapata zabuni, kisha wakaajiri watu wengine kutekeleza.

Dk Nguvila amesema hatua hiyo itawawezesha kukua kiuchumi, kwa kuwa mikakati ya Serikali kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma inatoa mwongozo wa makundi maalumu kunufaika na michakato ya zabuni za Serikali.

Amesema PPRA haina budi kuongeza juhudi ili makundi ya watu wenye ulemavu wasajiliwe NeST na wanufaike na fursa zilizopo.

Amesema redio hizo zenye uwezo wa kutumia memori kadi, watazitumia kisha elimu watakayopata watasaidia na wengine.

Amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kupendelewa ili wapate fursa za kazi zinazotangazwa, huku akisema hawataki walemavu wawe ombaomba.

“Ndiyo maana wana kampuni zao, na sisi tunawapa vifaa hivi ili wapate kazi kuijenga nchi yetu,” amesema.

Amesema wakipata kazi, wazifanye kwa uadilifu ili miradi watakayopewa walemavu ifanyike kwa ubora zaidi ukilinganisha na mingine.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema kitendo cha kutoa elimu na kuwapa vifaa walemavu kitawawezesha wao kuendelea kushiriki na kuzipata fursa zilizopo.

“Ilala zipo Sh17 bilioni, tutazigawa kama mkopo, tutawatendea haki, watazikopa zote na watahitaji zaidi ya hizo,” amesema.