WHO yatoa neno jitihada za Tanzania kufikia ajenda ya afya kwa wote

Muktasari:

  • WHO yasema ni lazima kuendelea kuwekeza katika huduma za afya ya msingi na afya za jamii ili kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma.

Dar es Salaam. Dk Charles Sagoe-Moses, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania, katika kuadhimisha siku ya afya duniani leo Aprili 7, 2024 amesema Tanzania inaendelea kujitahidi kufikia ajenda ya afya kwa wote, ikizingatia haki za kila mtu na kuhakikisha zimejumuishwa katika sera na mikakati.

 “Ili kufikia maono ya afya kwa wote na kukuza haki za kila mtu kupata huduma za afya, lazima tuongeze juhudi zetu katika kushughulikia mambo yanayoathiri afya, ikiwa ni pamoja na umasikini, kutokuwepo kwa usawa, na miundombinu duni,” amesema.

Katika taarifa yake ya kuadhimisha siku hii, amesema kwa msaada kutoka kwa washirika, WHO Tanzania imekuwa na itaendelea kuisaidia Tanzania katika mazungumzo ya kimkakati na sera.

Hatua hiyo amesema inalenga kudumisha mfumo wa afya unaoweza kutoa huduma inayopatikana, nafuu, bora, kamili, na iliyohusishwa kwa kila mtu kulingana na ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.

Amesema Tanzania imefanikiwa kupunguza  vifo vya uzazi, juhudi za kufikia kila mtoto kwa chanjo, na kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi, Kifua Kikuu, homa ya ini, Malaria, na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Dk Sagoe-Moses amesema ni lazima kuendelea kuwekeza katika huduma za afya ya msingi na za jamii ili kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma.

Kila Aprili 7, WHO hushirikiana na mataifa wanachama, jumuiya ya kimataifa, mashirika ya ndani na nje ya nchi kusherehekea Siku ya Afya Duniani ili kutoa fursa ya kimataifa ya kuelekeza umakini kwenye masuala muhimu ya afya ya umma na ajenda ya bima ya afya kwa wote.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Afya yangu, haki yangu’, ikilenga haki ya kila mtu, kila mahali, kupata huduma bora za afya, elimu, na taarifa; na maji safi ya kunywa, hewa safi, lishe bora, makazi bora, mazingira mazuri ya kazi, na uhuru kutokana na ubaguzi.