Wiki sita za moto kwa wanafunzi wa darasa la tatu

Muktasari:

  • Watalazimika kusoma maudhui ya mtalaa wa Kiingereza wa darasa la kwanza na la pili kwa muda wa wiki sita. Hatua hiyo yaibua mjadala kwa wadau wa elimu.

Serikali hivi karibuni ilitoa waraka wa elimu namba 05 ambao pamoja na mambo mengine unazungumzia ufundishwaji wa masomo ya mtalaa mpya kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari.

Hata hivyo, jambo lililogusa hisia za baadhibya watu kwente mtalaa huo uliotolewa na kutiwa saini na Kamishna wa elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa, ni maelekezo ya wanafunzi wa darasa la tatu kufundishwa maudhui ya somo la Kiingereza yaliyomo kwenye mtalaa mpya kwa kipindi cha wiki sita.

“Waraka upo wazi, zamani KiIngereza walikuwa wanaanza kufundishwa darasa la tatu, sasa kitaanza kufundishwa darasa la kwanza. Hawa wapo la tatu, itabidi wafundishwe Kiingereza cha la kwanza la la pili, ndio waendelee na masomo, mambo yako hivyo,”anasema Dk Mtahabwa alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa maagizo hayo ya waraka ambao umekuwa ukisambaa mitandaoni.

Wakati swali kuu likiwa ni kwa namna gani wanafunzi hao wanaweza kusoma maudhui ya madarasa mawili kwa kipindi hicho kifupi, wadau wa elimu waliozungumza na Mwananchi, wametoa hoja tofauti za kimtazamo.

Mustapha Puya ambaye ni mwalimu kwa taaluma, anakitazama kitendo hicho kama vurugu kwenye elimu.

‘’Hata maandalizi ni vurugu, walimu wamekwenda kufundishwa kwa siku mbili, tulisema mwaka 2012 mtaala huo haujaandaliwi vizuri, wakauvuta mpaka 2014 makubwa yaliyolalamikiwa hayajapatiwa ufumbuzi ikiwemo Tanzania kuwa na mikondo miwili inayomaliza shule kwa wakati mmoja, tuna mazingira ya kuwachukua wanafunzi hao, anaeleza na kuongeza:

‘’Hata kwenye miundombinu hakuna iliyojengwa kuchukua wanafunzi watakaomaliza ambao kutakuwa na mikondo miwili, walimu hawafahamu kinachoendelea masuala ya biashara na maadili nani kawafundisha lakini yanaanza, kwa hiyo hiyo mitaala haijakidhi matakwa ya wadau,

Anasema linaloshangaza ni kama kuna walimu walioandaliwa kufundisha masomo mapya, akisisitiza kama walimu watapatiwa mafunzo ya mtalaa mpya kwa siku mbili hakuna haja ya walimu kujifunza vyuoni kwa miaka mitatu.

Suala la ufundishaji kwa wiki sita limemgusa pia, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John cha jijini Dodoma, Dk Shadidu Ndossa anayehisi kuwapo kwa ugumu katika ufanisi wake.

“Darasa la tatu wana miaka mitatu ya kuwepo shuleni hivyo kuwepo mpango mkakati wa kuhakikisha wanafidia kidogokidogo yale mafundisho ambayo hawakupata, lazima tukubali mabadiliko yanavyokuja lazima baadhi waumie na wengine wafurahi,” anasema.

Mwalimu mstaafu, Bakari Heri anasema kilichofanyika ni mwendelezo wa Serikali kuleta utani katika mifumo ya elimu, akifafanua kuwa ni mzaha kumfundisha mtoto stadi za Kiingereza kwa wiki sita ilhali zilipaswa kusomeshwa kwa miaka miwili.

‘’Ukisema watawafundisha maudhui ya darasa la kwanza na la pili, hayo ni madarasa tofauti, hiyo ni sawa na miaka miwili. Sasa unawezaje kuminya maarifa ya miaka miwili kwa wiki sita kama sio kufanya utani? anahoji na kuongeza:

‘’Halafu somo lenyewe ni muhimu; ni Kiingereza ambacho tunataka watoto wetu wakijue barabara. Lakini pia hao walimu kwa nchi nzima, wamefundishwa namna ya kufundisha maudhui hayo ndani ya huo muda mfupi? Ninachokiona hapa ni kuwabebesha mzigo watoto ambao hawatoumudu.’’

Mwalimu Heri anahoji kama darasa la saba watafundishwa kwa wiki sita maudhui ya darasa la kwanza na la pili, hali itakuaje kwa wanafunzi wa darasa la pili ambao waraka hujaeleza kama na wao watalazimika kujifunza mtalaa wa darasa la kwanza.

‘’ Hawajasema darasa la pili watafidia vipi maudhui ya darasa la kwanza. Tuna mipango mingi na mizuri lakini tatizo ni kutojipanga na kutaka kulazimisha kila kitu kifanyike kwa wakati mmoja. Kama Taifa linataka mtalaa mpya kwa nini usingeanza tu na wanafunzi wanaoingia darasa la kwanza au wanaoingia kidato cha kwanza, halafu madarasa yaliyobaki yakamalizia miaka yao kwa mitalaa ya zamani?’’ anahoji.

Kwa upande wake, mtunzi wa vitabu Richard Mabala, haoni tatizo kwa wanafunzi wa darasa la tatu kusoma maudhui ya mtalaa wa darasa la kwanza na la pili, akisema kitendo hicho kitawasaidia wanafunzi hao kujifunza vitu tofauti na vile ambavyo walifundishwa.

“Darasa la kwanza wanachojifunza ni kusoma, kuandika na hesabu kwa hiyo mitaala mipya sio tofauti sana ya ile ya zamani, wasiwasi nilionao ni kuhusu maandalizi, tumekuwa na mitaala ya umahiri tangu 2005 lakini sijui ni walimu wangapi wamefundishwa kutengneza masomo kiumahiri baada ya kiujuzi,”anasema.

Mtazamo wake unaungwa na mhadhiri wa saikolojia Chuo Kikuu cha Dodoma Christian Bwaya anayesema kitakachofanyikani walimu ni kupitia upya mahiri za kusoma, kuhesabu, kuwasiliana na nyinginezo kwa kutumia mbinu mpya za ufundishaji na upimaji kama zinavyoanishwa kwenye mtalaa ulioboreshwa.

“Kwa hiyo mwalimu wa darasa la tatu anapoandaa andiko lake kwa muhula wa kwanza, anaweza kutenga majuma matano ya mwanzo kupitia kupitia mahiri moja kwa kila wiki,”anasema.

Akitoa mfano, Bwaya anasema wiki ya kwanza, mwalimu hupitia umahiri wa kusoma, wiki ya pili umahiri wa kuandika, wiki ya tatu, umahiri wa kuhesabu kwa kutumia mihutasari ya darasa la kwanza na pili kwa mtaala ulioboreshwa.

“Hili linawezekana kwa sababu kwa kiasi kikubwa mtoto tayari alishajifunza mahiri hizo kwa kutumia mbinu tofauti za ufundishaji na vigezo tofauti kidogo vya upimaji kwa mtaala wa zamani,”anasema.


Walimu wameandaliwa?

Kiongozi mmoja wa walimu mkoani Mara wilayani Musoma ambaye hakutaka jina lake liandikwe, anasema kwa walimu wa sekondari bado hawajaanza kupatiwa mafunzo lakini baadhi ya walimu wa shule za msingi walipatiwa mafunzo hayo.

“Kwa walimu wa Musoma ratiba ya mafunzo inaanza Desemba 30,2023 ambapo waratibu elimu kata ndio wanaanza kupewa mafunzo ili wao ndio wakawaelimishe walimu wa shule ya msingi,”anasema.

Naye mwalimu wa Shule ya msingi Qiblatein ya Dar es Salaam Abdurashid Laiza anasema tayari amepatiwa mafunzo yanayohusu mitalaa mipya.

“Mafunzo tuliyapata yametolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), tulikuwa walimu wakuu 40 kutoka shule mbalimbali zisizo za Serikali katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa siku moja,”anasema


Kauli ya TET

Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dk Aneth Komba anasema katika kipindi hicho cha wiki sita si masomo yote ya mtalaa mpya yatafundishwa, bali ni somo moja la lugha ya Kiingereza.

Kuhusu maandalizi ya ufundishwaji wa mtalaa huo, anasema TET imeshatoa vitabu vya kiada na miongozo kwa walimu.

“Tumejiandaa na kuandaa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuandaa moduli za mafunzo na kutoa mafunzo kwa walimu wote wa Serikali na binafsi,”anasema