Wizara ya Madini yaja na mpango kuwezesha wachimbaji wadogo
Waziri wa Madini Anthon Mavunde(katikati) akizungumza na Wanawake wachimbaji wa madini wakati wa kongamano la miaka 25 ya Chama cha Wanawake Wachimbaji (Tawoma) lililofanyika mjini Geita.
Muktasari:
- Serikali kupitia Wizara ya Madini imeandaa Programu ya kuwezesha Uchimbaji Madini kwa tija (MBT) lengo likiwa kuwajengea uwezo wachimbaji kuchimba kwa kutumia teknolojia za kisasa na kunufaika na kazi hiyo.
Geita. Wizara ya Madini iko katika mchakato wa kuanzisha programu ya Uchimbaji kwa maisha bora ya baadae “Mining for a Brighter Tomorrow” (MBT) lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo waweze kuchimba kwa tija zaidi.
Akizungumza katika Kongamano la miaka 25 ya Chama cha Wanawake Wachimbaji Tanzania (Tawoma), Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema mradi huo utatoa maeneo ya kuchimba pamoja na kuwawezesha kimtaji na mitambo ili waweze kuongeza Uzalishaji.
Amesema katika kutekeleza Dira ya 2030 Wizara imejipanga kufanya utafiti wa jiofizikia kwa kutumia ndege katika maeneo ambayo hayajafanyiwa tafiti ili kuchochea ukuaji wa Sekta ya madini na kuongeza mchango katika pato la Taifa.
“Kwa sasa utafiti umefanywa ni asilimia 16 tuu ya eneo lote tutatumia ndege kupiga picha ili kufikia asilimia 100 ya maeneo ifikapo 2030 tuweze kuchochea zaidi uwekezaji,” amesema Mavunde
Akizungumzia uwezeshwaji wa wanawake wachimbaji, Waziri Mavunde amesema Shirika la Madini Tanzania (Stamico) limefanya tafiti kwenye mikoa minne na kubaini changamoto zinazowakabili ambapo kupitia tafiti hizo watawezeshwa vifaa vya uchimbaji na kuchimba kisasa.
“Stamico imefanya stadi kwenye mikoa minne kuona changamoto wanazokabiliana nazo na kupitia stadi hizo watawawezesha vifaa vya uchimbaji na serikali itaendelea kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo ili kupata ufanisi na kuchimba kwa tija,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Venance Mwase amesema moja ya wajibu wa shirika hilo ni kuwalea wachimbaji wadogo na ili kujua changamoto zinazowakabili wamefanya tafiti kwenye mikoa minne ya Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara na kubaini changamoto tano zinazowakwamisha wachimbaji wadogo kuchimba kwa tija.
Ametaja changamoto hizo kuwa Matumizi ya teknolojia duni ambazo hazina tija na nihatarishi kwa maisha na afya zao, ukosefu wa taarifa sahihi za kijiolojia hali inayopeleka wachimbe kwa kubahatisha na kupoteza mitaji na wakati mwingine kuchimba kwa kutumia ramli za kiganga.
Changamoto nyingine ni wachimbaji wadogo kutokoposheka pamoja na ukosefu wa masoko ambapo amesema katika kutatua changamoto hiyo tayari Serikali imeanzisha vituo vya mfano vya uchenjuaji kwa kutumia teknolojia rahisi ili waweze kujifunza kwa vitendo.
Amesema Stamico imeendelea kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo nchi nzima na kwamba wanafanya mazungumzo za taasisi za fedha ili waweze kuwaamini wachimbaji na kuwakopesha.
Kuhusu taarifa za kijiolojia tayari serikali imenunua mitambo 15 ya kuchoronga kwa ajili ya wachimbaji wadogo inayotarajiwa kuzinduliwa Oktoba 21 mwaka huu jijini Dodoma.