Woga, uelewa mdogo chanzo wafanyakazi majumbani kukosa haki zao
Woga na uelewa mdogo zimetajwa kuwa miongoni mwa wafanyakazi wa nyumbani kumetajwa kuwa moja ya sababu zinazofanya baadhi yao kushindwa kutambua na kudai haki zao kama wafanyakazi wengine.
Kauli hiyo ilitolewa imetolewa leo Novemba 17,2025 jijini Arusha na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Hifadhi, Hoteli, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu), Saidi Wamba, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano kwa viongozi wa elimu rika wa wafanyakazi wa nyumbani kutoka mikoa sita.
Wamba amesema kuwa licha ya Serikali kutambua rasmi kazi ya wafanyakazi wa majumbani, bado uelewa wao kuhusu haki za msingi, sheria za kazi na hadhi yao kama waajiriwa upo chini. Hali hiyo, amesema, ndiyo imesababisha Shirika la Kazi Duniani (ILO), Serikali na Chodawu kuwakutanisha washiriki 25 kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya sheria za kazi, viwango vya ajira, nafasi ya vyama vya wafanyakazi, ukatili wa kijinsia, mikataba, ujasiriamali, afya na usalama kazini.
meibainisha kuwa elimu hiyo inalenga kuwapa nguvu ya kujitambua na kutambua thamani ya kazi wanazofanya, pamoja na kuwasaidia kuwa mabalozi wa kuwafikishia wengine waliopo katika maeneo yao ya kazi.
"Serikali imetangaza kima cha chini cha mshahara, na hata wafanyakazi wa nyumbani wamejumuishwa. Lakini wengi wao hawajui wanatakiwa kulipwa kiasi gani. Ni muhimu kutambua kuwa hakuna atakayekuletea haki bila wewe kuisimamia. Elimu mnayopata hapa inapaswa kuleta mabadiliko chanya katika maisha yenu," amesema.
Ameongeza kuwa chama hicho kitaendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wafanyakazi wa nyumbani wanapata uelewa sahihi na kuweza kushiriki kikamilifu katika fursa zinazohusu kazi zao, kwani nafasi yao kwa jamii ni muhimu lakini haijatambuliwa vya kutosha.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Kukuza Utambuzi na Kuboresha Mazingira ya Kazi kwa Wafanyakazi wa Nyumbani kutoka ILO, Chiku Semfuko amesema mafunzo hayo yanafanyika kwa ushirikiano na Chuo cha Wafanyakazi Tanzania (TLC) Mbeya ili kuwapatia washiriki elimu ya kitaalamu na vyeti vitakavyowaongezea weledi katika majukumu yao.
“Elimu mnayopata itawasaidia kufanya kazi zenu kwa ufanisi na pia kuwa mabalozi wa kuwafikia wengine ambao sisi hatuwezi kuwafikia moja kwa moja,” amesema.
Mkuu wa Chuo cha Wafanyakazi Tanzania, Hezron Kaaya amesema masuala ya utetezi wa wafanyakazi ni muhimu kwa sababu bado wapo ambao hawajitambui, hawajui haki zao na hawajui namna ya kuzitetea. Amesema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuwaandaa washiriki kuwa sehemu ya harakati imara za kutetea haki za wafanyakazi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Naye Ofisa Elimu Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ambaye pia ni Mratibu wa Dawati la Wafanyakazi wa Nyumbani, Halima Suleiman amesema wizara inaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi katika sekta binafsi ikiwemo kwa wafanyakazi wa majumbani.
Amesema sekta hiyo bado haijatambuliwa vya kutosha na jamii, huku wafanyakazi wenyewe wengi wakishindwa kujitambua kuwa ni waajiriwa kama wengine. Alieleza kuwa kupitia mradi unaoendeshwa kwa ushirikiano na ILO, wameona umuhimu wa kuanzisha dawati maalumu kwa ajili ya masuala ya wafanyakazi wa nyumbani ili kuwaongezea uelewa wa haki zao za msingi.
“Elimu hii itasaidia wafanyakazi wa nyumbani kutambua kuwa kazi wanazofanya ni sawa na kazi nyingine, na wanastahili kuheshimiwa na kulipwa kwa mujibu wa sheria,” amesema.