Zanzibar yaanza, yampa mwekezaji bandari ya Malindi

Muktasari:

  • Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeikabidhi Kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) ya nchini Ufaransa, kuendesha na kusimamia bandari ya Malindi kutoka Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), kwa lengo la kuongeza mapato na ufanisi.

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeikabidhi Kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) ya nchini Ufaransa, kuendesha na kusimamia bandari ya Malindi kutoka Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), kwa lengo la kuongeza mapato na ufanisi.

Pia, kampuni hiyo inatarajiwa kuongeza ujuzi kwa watendaji wa bandari na kasi ya ushushaji na upandishaji wa makontena, kupunguza msongamano mkubwa wa meli katika bandari hiyo ambayo ndio mlango wa uchumi kisiwani hapa.

Kwa mujibu wa mkataba wa mpito wa miaka mitano, wakati ikisubiriwa ikamilike bandari ya Mangapwani, Serikali itapata asilimia 30 na mwekezaji akiondoka na asilimia 70.

Kukabidhiwa kwa bandari hiyo ya kushusha na kupokea makasha ya mizigo kwa kampuni hiyo, kunakuja katikati ya mjadala kuhusu sakata la makubaliano ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai katika ushirikiano wa kuwekeza katika bandari kupitia kampuni ya Dubai Port World (DPW).

Kabla na baada ya Bunge la Tanzania kuridhia azimio la ushirikiano huo, kumekuwa na mjadala kwa nini ushirikiano huo hauhusu bandari za Zanzibar.

Kwa nyakati tofauti, Serikali ilikuwa ikitoa ufafanuzi kwamba kuna mazungumzo yanaendelea juu ya uwekezaji utakaokuja kufanyika bandari za Zanzibar.

Mjadala huo ulifika hadi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya baada ya mawakili wanne kufungua kesi kupinga mkataba huo wa ushirikiano na mwisho wa usikilizwaji wake, Mahakama ilitipilia mbali madai ya washtaki.

Bandari ya Malindi

Awali mkataba wa SMZ kuipa kampuni hiyo jukumu la kuendesha bandari hiyo, ulisainiwa Mei 18 mwaka huu na Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Zanzibar (ZPC).

Akizungumza wakati wa kukabidhiana bandari hiyo jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa ZPC, Joseph Abdalla Meza alisema wameanzia mbali hadi kufikia hatua hiyo.

“Hii inafuatia uamuzi wa Serikali kuona shughuli za bandari zimekuwa na changamoto nyingi, kwa hiyo tukasema ili kuimarisha mpango wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali, bora bandari hii ipewe kampuni hii yenye uzoefu mkubwa,” alisema Meza.

Mwenyekiti huyo wa bodi alisema lengo hasa ni kuongeza ufanisi, huku akiwa na imani kuwa hatua hiyo italeta mabadiliko makubwa.

”Nikisema bandari ina maana ni sehemu tu ya kushushia mizigo pekee, lakini sehemu nyingine zilizobaki kama eneo la abiria na bandari nyingine zitaendelea kuwa chini ya ZPC,” alisema.

Alisema gharama za uletaji mizigo kisiwani hapo zinazidi zaidi ya mara tatu ya bandari shindani ikiwemo ya Dar es Salaam na ya Mombasa Kenya, hali inayosababisha biashara kuongezeka bei na hatimaye kupandisha gharama za maisha.

Alisema ukiondoa uendeshaji, mamlaka na vyombo vingine vya usalama vinavyofanya kazi katika bandari hiyo, vitaedelea kufanya kazi kama kawaida.

ZPC wafunguka

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa ZPC, Nahmat Mahfoudh kwa mwaka, mamlaka inakusanya kati ya Sh42 bilioni hadi Sh44 bilioni na kwamba wafanyakazi wote wataendelea na kazi zao chini ya usimamzi wa kampuni hiyo.

“Kuna kuongeza uwezo na tija katika kuendesha bandari na kuweka mikakati kuifanya iwe inakwenda kwenye mifumo mizuri jambo ambalo litatusaidia kufika tunapotaka kufika,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema hatua hiyo pia italeta mababadiliko ya utendaji wa kimazoea na utamaduni wa kufanya kazi.

Wakati wa kusaini makubalino ya uendeshaji wa bandari hiyo Mei 18, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum alisema licha ya Serikali kufanya jitihada kuboresha mazingira ya bandari hiyo kununua vifaa vya Sh17 bilioni na kuweka mifumo, bado changamoto zilibaki palepale.

“Kama meli ilikuwa ikitumia siku saba sasa itatumia siku mbili. Gharama zile ambazo zilikuwa zinatumika kuleta meli hapa Zanzibar zilikuwa kubwa na zinabebwa na watumiaji,” alisema.

Dk Khalid alisema meli wakati mwingine zinakaa siku 42 na kila siku zinalipa takribani dola 30,000 hadi dola za Marekani 50,000.

“Hii ni gharama kubwa kwa hiyo hili limefanyika kwa nia safi kabisa maana bandari ndio geti kubwa la biashara katika visiwa,’’ alisema.

Alisema kwa sasa kuleta meli gharama zake ni kati ya Dola za Marekani 15,000 hadi Dola za Marekani 50,000, huku kuleta makontena ikigharimu Dola za Marekani 4,000.

Kauli ya mwekezaji

Naye Mtendaji Mkuu wa Zanzibar Multpupurse Terminal (ZMT) inayotokana na kampuni ya AGL, Nicolas Escalin, alisema watafanya kazi kama timu na wanaamini wataleta mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa bandari huku wakijivunia kufanya kazi kisiwani humo.

“Tupo hapa kuleta mabadiliko ya uendeshaji wa bandari iwe na tija. Tuna uzoefu wa kutosha katika masuala haya kwa hiyo tutawekeza mbinu mpya kuonyesha njia bora katika matumzi ya vifaa kufikia malengo ya Serikali kukuza uchumi wake,” alisema.

Wakati bandari ya Malindi inajengwa mwaka 1920 ilikuwa na uwezo wa kuegesha meli moja kubwa, lakini kwa sasa kuna meli nyingi zinaingia na hivyo biashara kupanuka.

Licha ya kuifanyia upanuzi inaweza kuegesha meli kubwa moja na ndogo moja yenye urefu wa mita 90.

Walichosema wadau

Mtaalamu wa masuala ya uchukuzi, Talib Omar alisema iwapo nia ya Serikali, ni kuleta mabadiliko hakuna budi kuungwa mkono jambo hilo, kwani sehemu yoyote yenye msongamano, haiwezi kuleta ufanisi huku akitahadharisha uwekezaji huo kuzingatia maslahi ya Taifa.

“Gharama zote za ushushaji na upandishaji wa mizigo, zinakwenda kwa mwananchi ambaye ndio mlaji wa mwisho, kwa hiyo hakuna shaka mpaka kufikia hatua hiyo, Serikali imeona umuhimu wake. Kikubwa ni kuzingatia maslahi ya Taifa,” alisema Omar.

Mwenyekiti wa Chama cha Ada-Tadea Taifa, Juma Khatib, alisema jambo hilo lilikuwa limechelewa kufanyika, kwani kulikuwa na ucheleweshaji na msongamano mkubwa wa makasha kwa sababu ya udogo wa bandari na kukosekana kwa mbinu mbadala.

Khatib ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya kuondoa msongamano katika bandari hiyo, alisema hatua hiyo pia itaondoa urasimu katika uendeshaji wa bandari hiyo.

“Kuondoa foleni katika bandari hii imeshindikana muda mrefu. Mimi najua kwa sbabu niliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya kuondoa msongamano huo lakini ilishindikana,” alisema.