Zitto Kabwe: Siku 100 za Rais Mwinyi zaleta matumaini mapya Zanzibar

Zitto Kabwe: Siku 100 za Rais Mwinyi zaleta matumaini mapya Zanzibar

Muktasari:

  • Desemba 7, 2020, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alimwapisha Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na hivyo kutekeleza Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2010 kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Zitto aeleza matarajio yake kwa Mwinyi
Zitto aeleza matarajio yake kwa Mwinyi
Zitto aeleza matarajio yake kwa Mwinyi

Hivyo, kama Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo mtazamo wangu katika Makala Hii fupi ni mtazamo wa mwanachama wa chama ambacho ni mshirika mdogo katika Serikali.

Kwanza, Chama cha ACT Wazalendo kinampongeza Dk Mwinyi ambaye ni Rais wa Awamu ya Nane ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri na kubwa ambayo ameifanya katika kipindi cha siku 100 tangu kuapishwa kwake.

Ni vigumu kupima kazi za Rais katika siku 100 kwa sababu mara nyingi katika nchi zetu ambazo hazina muda wa mpito, siku hizo hutumika kuunda Serikali.

Hata hivyo, baadhi ya matendo, maneno na haiba hutoa sura ya mwelekeo wa Serikali mpya.

Baraza la Wawakilishi ndio kwanza linakutana na hakuna hata muswada mmoja wa sheria ambao limepelekewa na Serikali mpya.

Lakini katika siku hizi 100 za mwanzo wa awamu yake, Rais Mwinyi ameonyesha uongozi na utayari wa kushughulikia changamoto kubwa za Zanzibar za mpasuko wa siasa, umoja wa kitaifa, rushwa na ubadhirifu, changamoto katika utoaji wa huduma za kijamii, kukwamua changamoto zinazoikabili sekta binafsi, kukuza uchumi na kutatua tatizo la ajira.

Ninapongeza hatua hizi za awali alizo onyesha za kutatua mpasuko wa kisiasa uliokuwapo Zanzibar katika kauli zake na vitendo.

Ni dhahiri kuwa dhamira hiyo imejionyesha katika utayari wake wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kumteua Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Lakini pia ameteua wawakilishi wawili kutoka chama cha ACT na kuanza kuachiwa kwa watuhumiwa wa kisiasa waliokuwa magerezani na teuzi zake Serikalini ambazo zimeepuka kasumba iliyotawala huko nyuma ya kubagua sehemu ya Wazanzibari.

Uteuzi wa vijana wengi, wa kike na wa kiume ni ishara nzuri sana kuhusu Zanzibar inayokuja. Kwa sababu vijana waliopewa majukumu mazito ndiyo viongozi wajao. Wizara nyeti kama Utalii inayokusanya mapato kwa asilimia 82 ya fedha za kigeni za Zanzibar na asilimia 31 ya Pato la Taifa la Zanzibar, kupatiwa kijana tena wa kike, kwa Zanzibar hii ni hatua kubwa kwa Wanawake wa Zanzibar.

Wizara ya vikosi vya SMZ, Fedha na Uwekezaji kuwa chini ya vijana pia ni jambo jema sana.

Hata nafasi zilizobaki za Wizara zinazotokana SUK kutakuwa na vijana wazuri.

Binafsi kwa hatua hii naona tumetiwa moyo na hatua ambazo Rais Mwinyi amechukua za kukemea na pale ilipobidi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi na watumishi wa umma wasio waadilifu.

Hali hii imerudisha kiasi nidhamu Serikalini. Hali kadhalika hatua ya kutembelea maeneo zinapotolewa huduma za afya, wepesi wake wa kukutana na wadau wa sekta ikiwamo binafsi na utayari wake wa kutatua kero zao.

Hivyo tumefarijika kuona kuwa naye anakerwa na kutokuwapo kwa ufanisi wa kuridhisha katika maeneo ya bandari na ukusanyaji wa mapato.

Hivyo, uamuzi wa haraka wa kuchunguza kuanguka kwa jengo la Maajabu na kuwekwa wazi kwa muhtasari wa Taarifa ya uchunguzi kulikofanywa na Waziri wa Utalii ni ishara ya mwenendo mpya wa uwajibikaji katika kushughulikia mambo ya umma.

Pamoja na hatua hizo za kutia moyo, ninaamini kazi iliyo mbele ya Serikali ya Awamu ya Nane ambayo ACT – Wazalendo ni sehemu yake, bado ni kubwa.

Naamini kuwa hatua hizi za awali na nia njema, zitaweza kuleta matunda yaliyotarajiwa ikiwa zitaendana na mabadiliko ya mifumo na ujenzi wa taasisi imara zitakazoendeshwa kiweledi na kufuata misingi ya uwajibikaji.

Zitto aeleza matarajio yake kwa Mwinyi

Ni matarajio ya wengi kuwa katika muda uliosalia, Rais Mwinyi kwa kushauriana na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif watajielekeza katika mageuzi ya utumishi wa umma na mageuzi ya vyombo vya ulinzi.

Lakini pia kwa mwendo huu alioanza nao, nina uhakika ndani ya miaka mitano, Zanzibar ile tuitakayo yenye utulivu, umoja na ushirikiano, itakuwa.

Imeandikwa na Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo.