Zimamoto yachunguza chanzo moto kuteketeza ghorofa Mwanza
Muktasari:
Ghorofa hilo linalotumika kwa makazi na maduka ya biashara limewaka moto leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 saa 6:00 mchana huku mali za wafanyabiashara zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye vyumba vitatu zikiteketea.
Mwanza. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Mwanza limesema linafanya uchunguzi kubaini chanzo cha moto uliozuka na kuteketeza jengo la ghorofa moja Mtaa wa Rwagasore katikati ya Jiji la Mwanza.
Ghorofa hilo linalotumika kwa makazi na maduka ya biashara limewaka moto leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 saa 6:00 mchana huku mali za wafanyabiashara zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye vyumba vitatu zikiteketea kwa moto huo.
Akizungumza mara baada ya kufanikiwa kuuzima moto huo, Kaimu Kamanda wa jeshi hilo, Kamila Labani amesema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika huku akiahidi kufanya uchunguzi maalumu ili kukijua.
"Moto umeanzia vyumba vya juu na sisi hatujaruhusu kuweza kuamia katika vyumba vingine vya chini kazi kubwa ilikuwa ni kuzuia moto huo usitoke kwenye chumba ulipoanzia kwenda kwenye nyumba nyingine za jirani na kazi hiyo imefanywa kwa nguvu ya askari wetu mahili kwa kushirikiana na wananchi na vikosi vingine,
“kimsingi vyumba vilivyoungua ni vitatu na vitu vilivyokuwa vinaungua ni vya plastiki ambavyo pia ni sehemu ya gesi na huwa vinawaka kwa uharaka sana, hadi hivi sasa ni vigumu sana kukutamkia chanzo kwa sababu lazima tukusanye maelezo na taarifa mbalimbali kutoka kwa wamiliki na wanaotumia jengo hilo na baadaye timu maalumu ya uchunguzi itakuja kuchunguza na kutoa taarifa ya chanzo cha tukio hilo,"amesema Laban
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema hamna mtu alijeruhiwa wala kupoteza maisha kutokana na moto huo.
“Sehemu ya juu ya nyumba hiyo ambayo ilikuwa ikitumika kuhifadhia vifaa vya wafanyabiashara wenye maduka katika eneo hilo ndo vimeungua na mali zake lakini kwa upande wa maduka mengine ambayo yalikuwa yamezunguka hili jengo kwa upande wa chini vitu vyake vimeweza kuokolewa chini ya usimamizi wa jeshi la polisi lakini mali zote ambazo zilikuwa upande wa juu kimsingi zote zimeteketea,”amesema Mutafungwa
Nakuongeza,“Jeshi la Polisi litaendelea kukaa na vikosi vingine kujua chanzo cha moto huo...mpaka sasa hakuna mtu ambaye amepoteza maisha wala kuumia zaidi ya kuteketeza mali zilizokuwa vyumba vya juu,”
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ametoa wito wa uchunguzi wa wa haraka kubaini çhanzo cha moto huo huku, akishukuru vyombo vya usalama na wananchi kufika na kuuzima moto huo.
Nasir Silaji, shuhuda wa moto huo na mfanyabiashara katika eneo hilo amesema awali alianza kuona moshi kwenye jengo hilo na hata alipojaribu kuwaambia watu wengine walipuuzia hadi kufikia kuteketeza mali.
"Ulianza moshi kidogo kutoka nikawaambia watu mbona naona moshi pale juu wengi wao walidharau wakasema labda wanaoishi huko wanapika na mimi ndio nilikuwa wa kwanza kuona moshi baada ya dakika tano nikaona watu wanaanza kuokoa mali na baadae kidogo ndo nikaona vikosi vya ukoaji vikifika kwa ajili ya kuzima moto,"amesema Silaji
Manka Dankiman, Mfanyabiashara mwajiriwa wa eneo hilo amesema hajafahamu chanzo cha moto huo katika jengo hilo zaidi ya kusikia na kuona moto ukiwa unawaka katika jengo hilo.
Geofrey Elikana, Mfanyabiasha katika eneo hilo amesifu jitihada zilizofanywa na vikosi vya uokoaji kutoka jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) huku akitaka miundombinu kuboreshwa zaidi.
"Mimi duka langu lipo jirani na hili gorofa lililokuwa likiungua nashukuru kwa kuuzima moto huo katika jengo hilo kwa sababu ungeendelea na mimi ninge athirika lakini hata kwa jirani yetu ambaye alikuwa na duka katika nyumba hiyo na mwenyewe amefanikiwa kuokoa vyombo vyote kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na uokoaji kiukweli wamefanya kazi kubwa sana na pongezi ziende kwao,"amesema Elikana