Zitto awataka wabunge kuwatoa hofu Watanzania sakata la bandari

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

What you need to know:

Chama cha ACT Wazalendo kimelitaka Bunge kujadili suala la mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai na kuwaondoa hofu wananchi kuhusu yale yanayojadiliwa kwenye mitandao ya kijamii.


Musoma. Chama cha ACT Wazalendo kimelitaka Bunge kujadili suala la mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai na kuwaondoa hofu wananchi kuhusu yale yanayojadiliwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe amesema hayo leo Alhamisi Juni 8, 2023 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu kauli ya ACT- Wazalendo baada ya suala hilo kuzua mjadala.

Zitto amewataka wawakilishi hao wa wananchi kujadili kwa uwazi jambo hilo na kwenye marekebisho parekebishwe, akisema chama hicho baada ya kutafakari na kusoma kwa kina baadhi ya nyaraka zinazohusua suala hilo kimeamua kuja na mambo hayo na kuwataka wabunge kuyazingatia.

Amewataka wabunge hao kujadili maeneo yanayowatia hofu wananchi ikiwemo suala la muda wa mkataba pamoja na vipindi vya kufanya marejeo, kuuzwa kwa bandari na maeneo ya makubaliano sambamba na kuvunjwa kwa mkataba pale pande mbili zikishindana.

 “Suala la umiliki wa kampuni ya uendeshaji kama itakuwa na hisa sawa kwa sawa kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai. Pia, suala la ulinzi wa bandari kama vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania pekee ndiyo vitatoa ulinzi,” amesema.

Kiongozi huyo aliyewahi kuwa mbunge wa majimbo ya Kigoma Mjini na Kaskazini kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2005, amesema suala eneo lipi la bandari ya Dar es Salaam litaendeshwa na kampuni binafsi na bandari zipi zitakuwa sehemu ya uwekezaji.

Zitto ambaye yupo katika ziara ya mikoa 11 ya kuimarisha chama hicho, amesema suala la upekee wa kampuni binafsi itakayoendesha bandari kwamba nchi pia iwe na ‘exclusivity’ dhidi ya kampuni kuwa na mikataba na bandari shindani na Tanzania.

"Tunawasihi Watanzania wote, ni muhimu tujadili masuala haya kwa misingi ya ukweli bila kuweka hisia za kibaguzi zitakazotugawa kama Taifa.

“Viongozi wa kisiasa tuwe makini na kauli tunazotoa kwani zinaweza kuongeza taharuki kwenye masuala ambayo kwa hakika yanahitaji ‘ukweli’ kuliko hisia,” amesema Zitto.