Zumaridi adai Polisi walichukua Sh19.5m, kadi yake ya CCM

Mshtakiwa namba moja katika kesi ya Jinai namba 10/2022 Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi (Kushoto) akimsikiliza mmoja wa mawakili wake, Erick Mutta alipofika katika mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza kusikiliza kesi yake leo. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wake, Hakimu, Monica Ndyekobora ameahirisha kesi hiyo hadi Disemba 22, mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Mwanza. Shahidi wa tisa utetezi katika kesi ya jinai namba 10/2022, Diana Bundala maarufu 'Mfalme Zumaridi' ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza kwamba wakati wa ukamataji askari polisi walichukua Sh19.5 milioni chumbani kwake.

  

Mfalme Zumaridi ambaye ni mshtakiwa namba moja kati ya tisa wanaoshtakiwa katika kesi hiyo ameenda mbali kuwa askari hao walichukua kadi yake ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hati tano za nyumba, kadi mbili za benki (Equity na CRDB), simu mbili aina ya Samsung na Infinix.


Amesema askari hao wakiongozwa na Inspekta Mapunda walichukua kadi ya gari aina ya Harrier na Toyota Wish, hati ya kusafiria, kitambulisho cha Nida, cheti cha kuzaliwa na vyeti vya kuzaliwa vya watoto wake, David Moses na Edward Moses.


Akiongozwa na Wakili wa utetezi, Erick Mutta, Zumaridi anayeshtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo shambulio la kudhuru mwili ameyasema hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Monica Ndyekobora.


"Walivyokuwa wanaingia ndani ya geti nilisikia mlipuko nikahisi kama Tairi limepasuka ile milio ilizidi nikatoka chooni nikaja chumbani ninakolala nikafunua pazia kuchungulia niliona maaskari wengi sana wengine wamevaa nguo za kiraia wakiwapiga watu waliokuwemo ndani ya uzio wa nyumba yangu," amesema


"Kabla hawajafika kwenye nyumba niliyokuwemo walikuwa wanavunja vioo vya nyumba zingine zilizokuwepo ndani ya uzio wa nyumbani kwangu huku wakisema wakinikamata wataniua," amesema


Ameongeza; "Walivyoingia walinipiga sana, askari mmoja aliniambia tuonyeshe pesa zilipo wewe unapesa, nikawa nimenyamaza tu wakaanza kunivuta wakinitoa nje ya chumba changu, wakanitoa hadi nje na kuniambia nilale chali nikiangalie jua,"


Amesema baada ya Afande Mapunda kumuulizaa alipohifadhi fedha simu zake walizodai wanazihitaji kwa ajili ya uchunguzi aliwaarifu ziko kwenye mkoba ndani ya chumba chake ambapo baada ya kuruhusiwa kwenda kuufata alikuta fedha na simu hizo zikiwa zimechukuliwa.


Mhubiri huyo alipoulizwa na Mwendesha mashtaka wa Serikali, Dorcas Akyoo iwapo ana elimu ya Thiolojia, amejibu alitokewa na Mungu ambaye ndiyo alimwambia aanze kuhubiri injili hiyo.


"Kanisa langu lilifungiwa ndiyo maana wakati nakamatwa sikuwa katika ibada ila nilikuwa nyumbani kwangu nikiendelea na shughuli zangu. Lakini ukiniuliza iwapo nimesoma Thiolojia, sijasoma ila nilioteshwa na Mungu," amesema Zumaridi


Awali, Shahidi wa nane katika kesi hiyo, Suzan Simon Ndalawa (29) akitoa ushahidi wake ameieleza mahakama kuwa aliamua kwenda kwa Mfalme Zumaridi baada ya kutelekezwa na mzazi mwenzake.

Amesema baada ya kutalakiana na mmewe huyo, Ally Abbas alimpangishia chumba Mtaa wa Iseni jijini Mwanza kabla hajamfungulia kesi katika mahakama ya mwanzo Mkuyuni iliyoamuru mtoto wake 'SS' akabidhiwe kwa baba jambo ambalo alipingana nalo na kukata rufaa katika mahakama ya Wilaya ya Nyamagana.


"Nilishangaa Februari 25, mwaka huu nikiwa kwa wakili wangu Bahati Kessy jengo la Nyanza walikuja askari watatu akiwemo Afande Paulina na Robert wakinitaka niende nao kituo cha Polisi Kati ambapo walinitaka nimpeleke mtoto nilipokataa wakaniamuru nivue viatu na simu niwape kisha wakaniweka mahabusu," ameeleza


Kati ya waliotoa ushahidi wao leo ni Wakili wa Mme wa Suzan (Ally Abbas) kwenye kesi ya madai ya mtoto 'SS', Linus Mnishi ambaye ameieleza mahakama hiyo kuwa maelezo ya onyo yaliyowasilishwa na jamhuri leo mahakamani hapo siyo ya kwake kwani katika maelezo aliyochukuliwa kituoni aliweka saini kwenye kila ukurasa na dole gumba lakini maelezo yaliyowasilishwa hayana alama hizo.


"Hiyo document (nyaraka) ambayo niliandika maelezo yangu niliweka saini na dole gumba lakini kwa hii ambayo nimeletewa hapa sijaona sahihi wala dole gumba nililoweka, saini iliyowekwa hapa siyo saini niliyoweka kwenye maelezo yangu," ameeleza

Baada ya mashahidi hao kumaliza kutoa ushahidi wao, upande wa utetezi ukaieleza mahakama kuwa hauna shahidi mwingine hivyo kuiomba mahakama hiyo kufunga kesi hiyo.


Baada ya maelezo hayo, Hakimu, Ndyekobora ameahirisha kesi hiyo hadi Disemba 22, mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kutoa hukumu ya kesi hiyo.