Prime
Fahamu dalili tano kwa mtoto mwenye ugonjwa wa moyo
Arusha. Kati ya watoto milioni mbili wanaokadiriwa kuzaliwa kila mwaka nchini, 13,000 hadi 14,000 kati yao huzaliwa na matatizo mbalimbali ya moyo.
Imeelezwa kuwa kati yao, 4,000 wanahitaji upasuaji kwa gharama ya kuanzia Sh4 milioni hadi Sh15 milioni kwa mtoto mmoja.
Miongoni mwa dalili za haraka zilizoainishwa na wataalamu kutambua mtoto mwenye tatizo la moyo ni pamoja na kupumua kwa shida, mapigo ya moyo kwenda kasi, kukohoa mara kwa mara na kifua kisichoisha, nimonia na kuchelewa hatua za ukuaji.
Daktari bingwa wa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru iliyoko mkoani Arusha, Deborah Mchaile anasema watoto wengi wanaozaliwa na matatizo ya moyo mbali na kurithi, idadi kubwa inatokana na kukumbwa na changamoto katika ukuaji wao akiwa tumboni mwa mama yake.
“Baadhi ya chanzo ni ukosefu wa lishe stahili, matumizi ya baadhi ya dawa tiba na matumizi ya vipodozi vyenye kemikali ambayo yanaweza kuathiri ustawi wa ukuaji wa moyo au umbo la moyo au hata ufanyaji kazi wake,” anasema.
Anasema kuna aina tano za magonjwa ya moyo kwa watoto, ikiwemo tundu kwenye kuta za moyo ambalo huleta hatari ya damu kuchanganyika, kufunga au kubana kwa mishipa ya damu ambayo hupunguza mtiririko wa damu sambamba na moyo wenye maumbo yasiyo ya kawaida.
Matatizo mengine ya moyo ni ugonjwa wa valvu za moyo ambao huathiri kufunguka na kufunga kwa moyo na huweza kusababisha damu kuwa na mtiririko hafifu sambamba na mishipa ya damu kuchanganyika ambayo huusababishia ushindwe kufanya kazi inavyotakiwa.
Dalili
Dk Deborah anataja dalili za mtoto mwenye magonjwa ya moyo kuwa ni mapigo ya moyo kuwa juu kuliko kawaida (kwenda kasi), kupumua kwa shida au kukohoa mara kwa mara kikohozi kisichoisha.
“Dalili nyingine ambazo ni kubwa zaidi ni kuchelewa katika hatua za ukuaji, mzazi au mlezi anapaswa kuchukua hatua za haraka anapoona mtoto wake anamlisha vizuri kwa lishe inayotakiwa lakini anadumaa, yaani ukuaji wake unakuwa hafifu, lakini zaidi akiona mtoto anabadilika rangi, hasa maeneo ya kucha na midomo inabidi achukue hatua haraka,” anasema daktari huyo.
Sababu na hatua za kuchukua
Ofisa Lishe Mkoa wa Arusha, Milembe Doto anasema miongoni mwa sababu ni ukosefu wa virutubisho muhimu anavyopaswa kula mama kipindi chote cha ujauzito wake ili kumfikia mwanaye kwa ajili ya ukuaji mzuri.
Anataja moja ya sababu ni upungufu wa foliki asidi ambayo hupatikana kwa mama ambaye anakula mboga za majani, matunda, maharage na nafaka zilizorutubishwa.
Pia upungufu wa mafuta ya Omega -3 ambayo husaidia ukuaji wa afya ya moyo na ubongo wa mtoto na hupatikana kwa mama kula samaki, dagaa na mbegu za chia. “Sababu nyingine ni upungufu wa virutubisho vya zinki na madini chuma sambamba na vitamin D, C na E ambayo hupatikana kwa mama kula nyama nyekundu, kuku, dengu, uyoga, pia mbegu za tikiti na maboga, lakini pia matunda yenye asidi kama machungwa na limao, lakini pia ale karanga, mayai na maziwa,” anasema Doto.
Anasema ili kuepuka mtoto kuzaliwa na matatizo hayo, vipo baadhi ya vitu ambavyo mjamzito hapaswi kuvitumia kwa usalama wa mtoto wake aliye tumboni.
Vyakula hivyo ni pamoja na lishe yenye mafuta mengi, unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara, lakini pia unywaji wa vinywaji vyenye kafeini nyingi kama kahawa, chai, vinywaji baridi vya soda na nishati sambamba na ulaji wa chumvi kupita kiasi,” anasema Doto.
Simulizi za wazazi
Akizungumza katika kambi ya madaktari bingwa wa moyo iliyofanyika kwa siku tatu katika Hospitali ya Arusha Lutherani (ALMC), Happy Julius (34) mkazi wa Olturoto wilayani Arumeru anasema mtoto wake aliugua homa za mara kwa mara pamoja na ugonjwa wa nimonia tangu akiwa na miaka mitano.
“Alianza kuugua nimonia na homa za mara kwa mara, tumekuwa tukimpeleka hospitali na kupatiwa dawa za homa na wakati mwingine zinachanganywa na za maumivu ambazo ni panadol au paracetalmol lakini dawa zikiisha anaumwa tena,” anasema Happy. Anasema wamehudhuria hospitali mara kwa mara kabla ya mtoto kubainika ana matatizo ya moyo Aprili mwaka huu, katika Hospitali ya ALMC.
“Nilipomleta hapa nilimwambia daktari ni maradhi ya muda mrefu na baada ya mahojiano alinishauri nimpime moyo, ndipo alibainika ana shida kwenye valvu za moyo,” anasema Happy na kuongeza;
“Nilishtuka sana kusikia nikamuone daktari wa moyo, lakini niliishiwa nguvu zaidi kusikia kweli mwanangu ana shida ya moyo na matibabu yake ni upasuaji.”
Hata hivyo, kwa huzuni Happy anasema aliamua kuwa muwazi kwa Mkuu wa msafara wa kambi hiyo, Dk Peter Kisenge na kufanikiwa kupata msaada wa matibabu bure ya upasuaji.
Naye Saumu Salimu (28), mkazi wa Kambi ya Fisi jijini Arusha anasema mtoto wake aliugua nimonia na kifua huku akikohoa mara kwa mara. Anasema alipoona hakuna mafanikio, alienda hospitali na kupatiwa rufaa ya kwenda JKCI mwaka 2018, akagundulika kuwa na tundu kwenye moyo. Ili kupatiwa matibabu, anasema ilihitajika awe na Sh4.5 milioni.
Elimu ya lishe kwa wajawazito
Rehema Mbise, ambaye kwa sasa ni mjamzito wa miezi saba na mkazi wa Sombetini jijini Arusha, anasema elimu ya lishe imekuwa duni wanapohudhuria kliniki na ameiomba Serikali kutoa msisitizo kwa wahudumu wa afya ili kuokoa maisha ya watoto wao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge anasema JKCI inatoa huduma mbalimbali, ikiwemo ya upasuaji na asilimia 70 ya gharama za matibabu kwa watoto huchangiwa na Serikali, na wazazi wakichangia asilimia 30.
“Pamoja na hilo, zaidi ya asilimia 80 ya watoto wanaogundulika kuhitaji huduma ya upasuaji bado hawamudu,” anasema.
Akizungumza jijini Arusha kwenye maadhimisho la Lishe kitaifa Oktoba 30, 2024, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema Serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa kutibu magonjwa yasiyoambukiza yanayotokana na ulaji usiofaa.