Faida za kujifungulia kwenye maji

Unaweza kusema ni teknolojia mpya, lakini inaelezwa mjamzito kujifungua mtoto wake ndani ya maji ni sayansi iliyofanywa na mabibi wa zamani na ikileta matokeo chanya kwa mama anayejifungua.

Wakati teknolojia sasa ikija na mfumo wa kidimbwi (beseni maalumu) chini ya wataalamu wakunga, kinamama wa zamani hususani Tanzania walijifungua pembezoni mwa mito au mabwawa wakipata ahueni ya kupunguza maumivu (uchungu) kwa kuwa maji hayo hulainisha misuli na kusaidia mama kujifungua kwa wepesi na kuondoa hatari ya kuchanika.

Wakati kinamama hao walijifungua nyakati za mchana, maji yakiwa na joto, kwa kutumia teknolojia mpya ‘water birth’ ambayo imekubalika duniani kwa sasa, imekuja nchini chini ya wataalamu wakunga ambayo inampa mama nafasi ya kuchagua kujifungua mtoto wake katika kidimbwi.

Kwa gharama ya Sh1.5 milioni, hospitali ya CCBRT inatoa huduma hiyo na inatolewa na wataalamu waliopata mafunzo ya kutoa huduma hiyo kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Marekani.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, mmoja wa wataalamu hao, Mkunga Mtaalamu, Agnes Nduguru anasema ‘water birth’ ni njia ya asilia kabisa ambayo inamsaidia mjamzito kupunguza maumivu na kumuweka sawa kisaikolojia akiwa katika hali ya uchungu huku akisisitiza kuwa njia hiyo haizuii maendeleo ya uchungu kwa mjamzito.

Agnes anasema maumivu ya uchungu hupungua kutokana na maji yanayowekwa kuwa katika hali ya uvuguvugu ambao husaidia misuli iliyokaza kulegea.

Anasema hiyo ndiyo sababu mjamzito anayejifungua katika kidimbwi (beseni maalumu) huwekewa maji ya uvuguvugu hadi kufikia usawa wa kitovu chake, ili sehemu za mgongo na kiuno ziweze kumsaidia kupunguza maumivu wakati akiwa katika hali ya uchungu.

“Kuna baadhi ya watu katika jamii huamini kuwa mjamzito anapooga au kujimwagia maji akiwa katika hali ya uchungu huweza kuathiri maendeleo ya uchungu, ‘water birth’ haizuii maendeleo ya uchungu ya mjamzito,” anasema mkunga Agnes.

‘Water birth’ ina faida mbalimbali kwa mama mjamzito ikiwemo kumuepusha kuchanika wakati akijifungua, kumpunguzia maumivu akiwa katika hali ya uchungu pamoja na kumsaidia kutumia muda mfupi kujifungua.


Ni salama kwa mtoto

Kwa wale wanaotamani kutumia njia hiyo, lakini wana hofu juu ya usalama wa mtoto wao endapo ataingia katika maji yaliyopo katika beseni maalumu wakati wa kujifungua, mkunga Agnes anasema huduma hiyo ni salama kwa mtoto na mama kama itafanywa na wataalamu waliopitia mafunzo maalumu ya kutoa huduma hiyo.

Anafafanua, “mtoto anapokuwa katika mji wa mimba anaishi katika maji kwa muda wote wa miezi tisa, hivyo jambo la kutokea kwenye maji si geni na yale maji yanayokuwa katika kidimbwi (beseni maalumu) siku ya mama kujifungua yanakuwa na joto sawasawa na la mama wakati mtoto alipokuwa tumboni na ndio maana maji hayo huwekwa kifaa maalumu cha kupimia joto muda wote ambao mama anasubiri kujifungua.”

Anasema kutokana na uvuguvugu uliopo katika maji hayo, humfanya mtoto asihisi utofauti wowote kwa takribani sekunde 40.

“Kabla ya kufikia muda huo (sekunde 40) mtoto anakuwa tayari ameshapokelewa na wataalamu kwa ajili ya hatua nyingine kufanyika baada ya mtoto kuzaliwa,” anasema.


Si huduma ya dharura

Daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya kinamama kutoka hospitali ya CCBRT, Dk Issa Rashid anasema huduma ya mama mjamzito kujifungulia katika kidimbwi haitolewi kwa dharura, kwani huitaji maandalizi mbalimbali ikiwemo mhusika kufanyiwa vipimo, ili kufahamu kama ana vigezo vinavyoruhusu kujifungulia katika kidimbwi.

Dk Issa alitaja baadhi ya sababu zinazosababisha mama kutoweza kujifungua katika beseni hilo maalumu ikiwemo kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, joto lake kuzidi nyuzijoto 38, presha ya mimba na sababu zote zinazoweza kusababisha mjamzito kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Ni vema pia mama anayetaka kujifungua kupitia ‘water birth’ kufika hospitali mapema, ili kupewa mafunzo ya namna gani huduma hiyo inatolewa, kuandaliwa kisaikolojia yeye pamoja na mtu wake wa karibu aliyemchagua kuambatana naye siku atakayojifungua,” anasema.

Anasema mama anayechagua njia hiyo wakati wa kujifungua hupewa nafasi ya kuchagua mtu wake mmoja wa karibu na anayemuamini kuwa naye katika siku anayojifungua.

Anasema mtu huyo anaweza kuwa mume wake, mama, dada, shangazi ambaye naye huandaliwa kisaikoloja.

“Uwepo wa huyu mtu ambaye amechaguliwa husaidia kumuweka mama sawa kisaikolojia,”

Pia anasisitiza huduma hiyo haitakiwi kutolewa na watu wasiopitia mafunzo maalumu kuhusu namna ya kumsaidia mjamzito kujifungua kwa njia ya kwa njia hiyo.

Dk Issa anasema tangu huduma hiyo kuanza kutolewa katika hospitali ya CCBRT mwishoni mwa Novemba mwaka jana, wameshawahudumia wajawazito watatu ambao wote wamejifungua salama na hadi sasa wao na watoto wao wako salama.

Anasema uhitaji wa huduma hiyo ni mkubwa kutokana na wanawake wengi sasa kuanza kupata elimu juu ya huduma hiyo.


Aliyepata huduma asimulia

Irene (si jina halisi) ni moja kati ya wanawake waliowahi kujifungua kwa njia ya ‘water birth’ katika uzazi wake wa kwanza katika hospitali ya CCBRT na anakiri ilimsaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maumivu wakati akiwa katika hali ya uchungu bila kuathiri maendeleo ya uchungu wake.

Anasema hata uchungu ulipochanganya na njia kufunguka vizuri, alijifungua ndani ya muda mchache na wote (yeye na mtoto) walibaki salama.

“Sijui pengine kwa sababu ulikuwa ni uzazi wangu wa kwanza, lakini kipindi nilipoelekezwa mazoezi ya kufanya ili kusaidia njia kufunguka vizuri nilishindwa kuyafanya nikiwa nje ya maji hadi pale nilipowekwa katika kidimbwi (beseni maalumu).

“Nilifanya vizuri na hata kuniwezesha kujifungua ndani ya muda mfupi na kufanikiwa kupata mtoto wa kike,” anasema.

Anatoa wito kwa wanawake wanaotamani kutumia njia hiyo wasiwe na hofu kwa kuwa njia hiyo ni salama na kuwasisitiza kutokukubali kupewa huduma hiyo na watu wasio na utaalamu katika eneo hilo.