Kisukari, presha zatajwa kuchangia watoto kufia tumboni
Muktasari:
- Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na afya ya uzazi, ametaja sababu mbalimbali za watoto kufia tumboni kabla ya kuzaliwa.
Dodoma. Kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wanawake kuharibu mimba kwa watoto kufia tumboni kabla ya kufikisha umri wa kuzaliwa, yaani miezi tisa.
Baadhi ya kinamama hukumbwa na tatizo hili mfululizo, kwani unakuta mimba ya kwanza, ya pili, ya tatu ya nne na kuendelea anakumbana na tatizo hilo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na afya ya uzazi kutoka Hospitali ya kanda ya kati ya Benjamin Mkapa ilioyopo Jijini Dodoma, Dk Israel Soko amelizungumzia tatizo hilo kwa kina alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi Digital leo Machi 15, 2024.
Dk Soko amesema tatizo la watoto kufia tumboni linasababishwa na mambo mbalimbali, yakiwemo magonjwa ya kisukari na presha za mimba, upungufu wa damu na magonjwa ya zinaa yakiwemo kaswende.
Amesema changamoto hiyo ni kubwa kiasi kwa sababu inawapata wanawake wenye magonjwa ya presha ya kupanda wakati wa ujauzito au hata kabla ya ujauzito na wenye ugonjwa wa kisukari kabla au inayotokana na ujauzito.
Sababu nyingine ametaja kuwa ni kutokana na kondo kujiachia lenyewe kabla mtoto hajazaliwa, kutokana na presha, japo hakuna sababu za moja kwa moja zinazoelezwa kwa nini huwa linawahi kujiachia.
Amesema wengine wanashindwa kujua kisababishi kwa sababu mama anakuwa hana presha ya kupanda wala ya kushuka, hana ugonjwa wa kisukari, lakini unakuta mtoto amefia tumboni na wakitafuta sababu wanakosa.
Sababu nyingine ya magonjwa ambayo huwa yanachangia mtoto kufia tumboni ni mwili wenyewe kutengeneza vita kati ya kinga yake ya mwili na kiumbe kilichoingia (mimba) inaitwa antibody and antigene reaction.
Amesema sababu nyingine ni makundi ya damu kati ya mama na baba ambayo husababisha watoto wanapozaliwa hupata changamoto ya manjano au kuishiwa damu.
Amesema hiyo inasababishwa na mama kuwa kwenye kundi lolote la damu lenye hasi (negative) na baba kuwa kwenye kundi la chanya (positive), wanapata changamoto ya watoto kufia tumboni inaitwa (hydrospitalis) ambapo mtoto mwenyewe anatengeneza kinga kwa hiyo anapata idima, anaishiwa damu akiwa tumboni na mwisho wa siku anafia tumboni.
Amesema kitaalamu mama hatakiwi kuwa na kundi lolote la damu lenye negative na baba akiwa kwenye kundi lenye positive kwa sababu hapo ndipo inapotokea changamoto, hivyo inatakiwa wote wawili wawe kundi la damu hasi au chanya.
“Kama watagundua mapema na kwenda hospitali, kuna dawa ambayo mama atachomwa ndani ya masaa 72 baada ya kujifungua kwa sababu mtoto wa kwanza huwa hana madhara isipokuwa kwa mtoto wa pili na kuendelea,” amesema.
Ili kuzuia watoto wasifie tumboni, anawashauri wazazi kuwa wawazi kwa daktari hasa kwa mama kama aliwahi kuharibu mimba kwa baba ambaye alikuwa ni positive, awe muwazi hata kama hatasema kwa mume wake, lakini awe muwazi kwa daktari.
Dk Soko amesema kwa changamoto hiyo kuna dawa mama atachomwa akishafikisha wiki ya 28 hadi ya 32 ambapo atachomwa sindano ya kwanza na sindano ya pili atakuja kuchomwa ndani ya saa 72 baada ya kujifungua.
“Lakini akiendelea kuficha ina maana kuwa matatizo yatakuwa yanaendelea kujitokeza bila kujua changamoto iko wapi?” amesema.
Sababu nyingine ni mapacha wawili ambao hubadilishana damu, yaani unakuta pacha mmoja anamlisha damu pacha mwingine inaitwa Twin Transfusion kwa hiyo mtoto mmoja anampa damu mtoto mwingine hasa pale wanapochangia vitovu au kondo.
Hii inatokea pale damu inapotoka kwa mtoto mmoja na kwenda kwa mtoto mwingine ambapo mmoja ndiyo huwa anadhoofika na hata kufia tumboni na wakati mwingine akiendelea na afya njema.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni matatizo ya vitovu ambapo mtoto anapokuwa mdogo kadiri anavyocheza na kujizungusha kile kitovu kinatengeneza fundo kwa hiyo kadiri anavyoendelea kukua lile fundo linaendelea kujibana na kujivuta mpaka anapokuwa mkubwa lile fundo linakuwa limejifunga kabisa akiwa yupo tumboni, kwa hiyo mtoto atakufa kwa kukosa damu na hewa.
Amesema kama mtoto hatafia tumboni atakufa wakati wa kujifungua kwa sababu kadiri mtoto anaposhuka wakati wa kuzaliwa ndivyo kitovu kinavyozidi kujifunga fundo kama la kamba au kitovu kinamzunguka mtoto na kama hatafanya vipimo vya ultrasound na kugundua kama kitovu kimezunguka kadiri uchungu unavyozidi ndivyo kitovu kinavyozidi kumnyonga mtoto, kwa hiyo mpaka unafika muda wa kujifungua unakuta tayari mtoto ameshakufa.
“Hivi vitu huwa vinatokea na wala si uchawi huwa vinatokea, kadiri mtoto alivyokuwa anacheza mle ndani kwa sababu kuna muda anajizungusha mwenyewe unakuta anatengeneza hilo fundo….na huwa linaanzia tangu mtoto akiwa mdogo,” amesema Dk Soko.
Matibabu yake
Dk Soko amesema tiba ya tatizo hilo ni kuwahamasisha kinamama wajawazito kuanza kliniki mapema mara anapojihisi ni mjamzito kwa ajili ya kufanya vipimo mapema hasa vipimo vya damu kuona wingi wa sukari na kama iko juu ataanzishiwa dawa.
Pia amesema watapima ugonjwa wa kaswende na kama mama anayo basi atatibiwa, watapima pia presha na kujua ikoje na kama iko juu ataanzishiwa dawa kwa ajili ya kuifanya ikae kwenye kiwango cha kawaida.
Amesema pia kuna virutubisho ambavyo mama atapewa na pia kundi la damu litajulikana mapema ambavyo vyote ni faida ya kuanza kliniki mapema.
“Bila kufanya hivyo ndipo matatizo yanapotokea unapata kifafa cha mimba au mtoto kufia tumboni, hata sukari ni hivyo hivyo utapima awali, utapima tena ukiwa na wiki 16, wiki 20 na ikionekana imepanda utaonekana kuwa umepata ugonjwa wa sukari kutokana na ujauzito, hivyo utaanzishiwa dawa mapema na taratibu za kukuzalisha mapema pia zitaandaliwa,” amesema Dk Soko.
Amesema ikiwa mama atakutwa na matatizo ya sukari na presha wakati wa ujauzito hata utaratibu wa kliniki utabadilika, kwani hatakwenda tena kwa nesi, bali kwa daktari kwa sababu ya uangalizi wa karibu.
Amesema hizo ndiyo faida za kuanza kliniki mapema na pia zinaweza kuzuia vifo vya watoto wakiwa tumboni kwa kupata elimu ya afya ambako unafundishwa viashiria vya hatari wakati wa ujauzito.
Amesema mama akipata elimu ya afya inakuwa ni vizuri kwa sababu akiona siku ya kwanza mtoto amepunguza kucheza, anawahi hospitali ambapo atapimwa na kujua changamoto ya mtoto tumboni na ikibidi kuzalishwa mapema, ili upate mtoto mwenye afya njema.
Amesema tatizo la mwanamke kuishiwa damu wakati wa ujauzito kunasababishwa na mimba kuongeza matumizi ya damu mwilini na ndiyo maana huwa wanapewa dawa za kuongeza damu wanapoanza kliniki.
Amesema changamoto iliyopo baadhi ya wajawazito huwa hawazitumii kwa sababu huwa zina maudhi na changamoto ndogo ndogo, anaporudi tena kliniki damu huwa imeshuka zaidi, jambo ambalo ni hatari.
“Unaweza kukuta damu ya mjamzito imeshuka hadi nne au tano kutoka saba, wakati wastani wa damu ni kuanzia 11.5 na kuendelea,” anasema.
Daktari huyo amesema mtoto anahitaji damu kwa wingi katika ukuaji wake, hivyo kadiri anavyokuwa mama anahitaji awe na damu nyingi kwa ajili ya kupeleka virutubisho na hewa kwa mtoto, hivyo mfuko wa mtoto unatakiwa uwe na damu nyingi.
Amesema damu inaweza kuongezeka kwa kutumia dawa za kuongeza damu alizoandikiwa kila mwezi na kwa upande wa vyakula lishe ambavyo vinaweza kuongeza damu ni kama vyakula jamii ya mikunde, maini ambayo yana protini na madini chuma ambavyo yana faida katika kuongeza damu na madini chuma.
Ametaja vyakula vingine kuwa ni dagaa, samaki, matunda na mboga za majani ambazo zina vitamini zinazosaidia katika kuzalisha chembe nyekundu za damu.