KUTOKA LONDON: Ulaji nyama wapigwa kikumbo uzunguni

Alikuwa akihubiri. Wahubiri wamejazana mitaani London, wanawake kwa wanaume. Wakristo zaidi.

Wapo wanaotumia vipaza sauti vikubwa, wenye muziki wa simu na wanaohutubia ndani ya vyombo vya usafiri.

Hata wakikatazwa na vyombo vya usalama, hurejea wakijetetea juu ya hulka ya demokrasia nchi zilizoendelea.

Uhuru wa kusema na kujieleza hadharani, ingawa sheria haivunjwi kwa mathalan kutukana kadamnasi.

Alikuwa akituangalia tuliosimama pale, tukisubiri gari moshi la ardhini.

Magari moshi huja kila baada ya dakika mbili au tatu. Hayasimami. Hayasitishi huduma. Labda uwepo mgomo wa wafanyakazi.

Mwisho wa juma huwepo usiku kucha, yakipunguza muda wa kusimama kuwa baada ya dakika tano.

Yupo bwana mmoja anayezunguka moja ya vituo maarufu jijini na spika lake kubwa. Hudunda miziki ya miaka ya 1970. Kila akiulizwa au kuzuiwa hudai nyimbo za siku hizi za vijana hazina “midundo ya kuvutia.”

Hupayuka. “Wako legelege sana. Suruali zimening’inia makalioni. Hawa si wanaume hawa!”

Uhuru wa kujieleza na kusema utakalo huo.

Sasa mhubiri aliendelea na hotuba yake kubwa. Hakutumia kipaza sauti, ila alisikika.

“Mimi sidhani siku hizi wanadamu ni wakweli. Wala sidhani hawa wanaodai wanafuata sayansi ya kimaendeleo wanamwelewa Muumba Mungu! Kaumba viumbe vyote na mimea pia. Uhai ni mali yake. Kutuambia tusile nyama, tule tu majani ni wito wa kipuuzi usiokubali kauli ya Mwenyezi Mungu. Hebu tazameni lile tangazo pale tena!”

Kweli upande uliokabiliana na kituo ulijaa bango pana lenye picha ya Waziri Mkuu, Rishi Sunak aliyechaguliwa miezi miwili na nusu iliyopita baada ya lelemama kadhaa za uongozi.

Tangu ateuliwe kumekuwa na utulivu fulani. Bango hili lenye picha yake linauliza swali. Je, mheshimiwa atakubali kuwa “vegan”, yaani mlo wa mimea mitupu kwa mwezi kwa paundi milioni moja? Ni swali lenye kejeli maana Waziri Mkuu Sunak ni mmoja wa matajiri wakubwa nchini.

Bango linaongeza takwimu zinazokashifu ulaji nyama. Kila siku tatu na nusu huwa tunateketeza maisha ya idadi ya wanyama inayolingana na ya wanadamu waliouawa miaka sita wakati wa vita vikuu vya dunia.

Ikiwa na maana mauaji ya wanyama wanaoliwa - yamezidi ya wanadamu. Hapo hapo katika tangazo mna tovuti ya hawa wapigania haki za wanyama. Bango linamalizia na picha ya ndama na nguruwe. Tovuti inaitwa Gen.Org (kifupi cha Generation Vegan) ...kundi la wapinzani wa kula nyama. Kati ya mabadiliko wanayoleta ni milo ya nyama kama “bacon” (nguruwe wa kukaanga) au vitafunio vyovyote vya nyama ila vimetengenezwa kwa mboga.

Wanasisitiza wanadamu tunaweza kuishi kwa kula mimea mitupu bila kuua wanyama.

Mhubiri ananyooshea bango kidole. Anamaka:

“Hivi wanadamu tumewahi kujiuliza unapokata tunda kama ndizi, kitunguu, mhindi au hata mua, je havisikii maumivu? Nani kawadanganya mimea haihisi maumivu? Eti mtasema haina mdomo. Haina sauti. Lakini utafiti wa kisayansi umeshathibitisha mimea hukerwa na ina hisia kama zetu maana ni viumbe hai. Mmesikia utafiti uliofanywa kwa kuweka mimea chumba chenye muziki fulani. Ikiwa ule muziki unachusha mimea hufa. Mmea una hisia. Kudai tusiue wanyama, na tule kila kitu cha mimea ni unafiki na kukiuka masharti ya Muumba dunia.”

Wasafiri tunamtazama jamaa.

Tunamsikiliza.

Tunasonga mbele na treni tukitafakari.