Madaktari wataja sababu kitanzi kupotelea mwilini

Kitanzi ni moja ya njia za uzazi wa mpango, ambacho mwanamke huwekewa kupitia ukeni ili kuzuia mimba.

Hata hivyo, kitanzi hicho kimekuwa shubiri kwa Penina John, baada ya kudai kilipotelea mwilini na kulazimika kutanuliwa mirija ya uzazi ili kitolewe.

"Nilianza kupata ganzi kwenye paja la kulia kushuka hadi mguu, nilihisi ni hali ya kawaida, lakini kila nilipokaribia kuingia kwenye siku zangu, hali ile ilizidi kunitesa," alisema.

Alisema aliendelea kupata ganzi hadi alipoamua kwenda hospitali na baada ya uchunguzi wa madaktari bingwa wa uzazi, aliambiwa kitanzi hakipo mahala pake, hivyo anatakiwa atanuliwe mirija ya uzazi ili kitafutwe.

"Niliambiwa nisubiri hadi nitakapoingia kwenye siku zangu ndipo matibabu yafanyike, wakati huo kuna kiuzi cha kitanzi ambacho awali nilikuwa nakisikia, lakini nikawa sikisikii tena.

"Madaktari waliniambia inabidi nitanuliwe mirija ya uzazi, kitanzi kitafutwe kiko wapi, ilichukua kama saa mbili hadi kumaliza matibabu yale.

"Mwanzo nilijua ni changamoto ndogo, lakini kutokuwepo kwa kile kiuzi ndipo kulinitisha zaidi, waliniambia kama kingekuwa kinaonekana ingekuwa rahisi kitanzi kutolewa, hivyo kusababisha isijulikane kitanzi kiko sehemu gani," alisema Penina ambaye alianza kutumia uzazi huo wa mpango baada ya kujifungua mtoto wake wa pili mwenye miaka sita sasa.

Siwema Joachim, aliyekuwa akitumia kijiti, anasema alilazimika kukitoa kutokana na kupata damu ya hedhi mara kwa mara bila mpangilio.

"Ilinitesa hadi nikalazimika kukitoa baada ya mwaka mmoja, hivi sasa situmii njia yoyote ya uzazi wa mpango zaidi ya kutumia kalenda tu," anasema Siwema.

Hao ni baadhi ya wanawake wanaopitia changamoto kadhaa katika matumizi ya uzazi wa mpango, licha ya kuelezwa wanaotumia uzazi wa mpango ni wachache wanaopata madhara madogo madogo, lakini faida ni kubwa.

Miongoni mwa maudhi hayo ni matiti kujaa, kusikia kichefuchefu, homoni nyingine hubadilisha mzunguko wa hedhi na huenda akaona ukeni kunakuwa kukavu na wakati mwingine hamu ya tendo la ndoa kupotea.


Chanzo chatajwa 

Daktari bingwa wa uzazi wa Hospitali ya Mkoa Morogoro, Daniel Nkungu anasema kitanzi kupotelea kwenye mfuko wa uzazi inategemea kiliwekwaje.

"Kama mwekaji alikisukumiza kikaingia kwenye nyama inawezekana kupotea, hilo linakuwa tatizo la mwekaji, alisukumiza bila utaalamu na kutoboa kizazi.

"Badala ya kukaa ndani ya mfuko wa uzazi kinakaa nje, hilo huwa mara nyingi ni tatizo la mwekeji, hana utaalamu wa kutosha," anasema.

Anasema kinapoingia mahali pabaya kitasababisha maumivu kwa aliyewekewa, ingawa sehemu iliyotobolewa itaweka kidonda ambacho kikipona kitaacha kovu.

“Athari zake mara nyingi ni maambukizi kwenye kizazi, mwenye tatizo hili anatakiwa kuonana na madaktari bingwa waliosomea eneo hilo wamfanyie uchunguzi, japo hilo haliwezi kuwa tatizo moja kwa kila mtu, kitanzi kikiwekwa vizuri hakina matatizo yoyote," anasema Dk Nkungu.

Daktari mwingine wa masuala ya uzazi, Abdul Mkeyenge anasema kitanzi kwa baadhi ya watu walioweka anaweza asionekane kutokana na sababu mbalimbali.

“Kuna muda nyama zinaota, katika kutoa kisionekane haraka, au kile kiuzi kisionekane, hiyo huwa inatokea kwa baadhi ya watu," anasema daktari huyo bingwa wa masuala ya uzazi wa hospitali ya Salaamani, Temeke jijini Dar es Salaam.

Anasema kitanzi kwa anayewekewa kinaingizwa ukeni na kwenda kukaa karibu na shingo ya kizazi na mfuko wa uzazi

"Hata hivyo njia za uzazi wa mpango zote zina madhara, mimi ukiniuliza sikushauri utumie, lakini njia rafiki ni kutumia kondomu au kufanya tendo la ndoa siku zisizo za hatari,” anasema.

Akizungumzia taarifa iliyotanda kwamba mama anayetumia kitanzi, kama hakijawekwa vizuri anaweza kupata ujauzito na mtoto kuzaliwa akiwa amekishikilia, Dk Mkeyenge anasema hakuna kitu kama hicho.

Anasema mwanamke kabla hajaamua kutumia njia za uzazi wa mpango, ikiwamo kitanzi anapaswa kupata ushauri wa watu wa uzazi wa mpango vema.

Kuhusu wanaume kukisikia kitanzi kwa wenza wao wakati wa kujamiiana, Dk Mkeyenge anasema hiyo ni kweli inatokea kwa kuwa kitanzi kina kiuzi ambacho hutokeza.

Hata hivyo, anasema kuhusu wanawake walioweka kitanzi na wenza wao wana maumbile makubwa, sio kweli kama wanapojamiiana wanasababisha kukisogeza kitanzi ndani zaidi kwa wake zao.

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) wa mwaka 2022 unaonyesha asilimia 45 ya wanawake wenye uwezo wa kufanya tendo la ndoa wanaotumia njia za uzazi wa mpango, asilimia 36 wanatumia njia za kisasa na asilimia 8 wanatumiaji njia za asili.

Hata hivyo, njia ya vipandikizi ndiyo inayotajwa kutumika zaidi miongoni mwa wanawake kwa asilimia 14, ikifuatiwa na njia ya sindano kwa asilimia tisa.