Makondo ya nyuma ya uzazi sasa kuzalisha gesi ya kupikia

Dodoma. Changamoto ya harufu mbaya iliyokuwa kero kwa wakazi wa maeneo jirani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, imepata suluhisho baada ya hospitali hiyo kuanza kutumia kondo la nyuma kuzalisha gesi ya kupikia inayotumiwa kwenye wodi ya wazazi.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Kitengo cha usimamizi wa ubora wa huduma hospitalini hapo, Dk Edmund Mgeni alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya waliandaa wazo hilo na kuanza kulifanyia kazi kwa hatua za awali mwaka jana.

Dk Mgeni alisema mpango huo umesaidia wanawake wanaokwenda kujifungua kupata maji ya moto na kuondoa changamoto ya harufu kali iliyokuwa inatoka kwenye shimo la kutupia uchafu huo, ambao ulikuwa ukiathiri sana shughuli za kiutendaji na usalama wa afya.

“Tumeona katika uzalishaji wa gesi kama huo kuna wengine wanatumia vinyesi au mabaki ya mimea, lakini hapa kwetu tunatumia makondo ya nyuma ambayo zamani tulikuwa tunayatupa, leo kwetu imegeuka kuwa ni kitu cha thamani kinatuzalishia gesi,” alisema mtaalamu huyo.

Dk Mgeni alisema mfumo huo kwa sasa unapunguza matumizi ya umeme, kwani maji hayo awali yalikuwa yanachemshwa kwenye majiko yanayotumia nishati hiyo.

Alisema kutokana na idadi kubwa ya wanawake wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua, shimo lililokuwa linahifadhi uchafu huo lilikuwa linajaa mapema na kutakiwa kunyonya taka ambapo gharama yake ilikuwa takriban Sh150,000.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kitendo cha kutupa taka hizo kwenye shimo wakati mwingine ilikuwa ni hatari hata kwa watumishi, kwani majimaji ya makondo hayo baada ya muda huzalisha bakteria na kusababisha uzalishaji wa harufu na kuwa hatari kwa afya za wafanyakazi na wagonjwa watakaokuwa karibu, wakiwamo waliokuwa kwenye wodi ya kifua kikuu.

Muuguzi wa kitengo cha magonjwa ya kifua kikuu ambacho jengo la Ofisi yake lipo karibu na shimo hilo, Emmaculata Kazingo alisema awali kulikuwa na ugumu wa utendaji kazi, lakini walivumilia kwa sababu ya wito na mapenzi yao kwa wagonjwa, ingawa ukweli ni kuwa harufi ilikuwa kali.

Kazingo alisema wagonjwa wanaotibiwa katika idara hiyo mara kadhaa walilalamikia suala la harufu kali, ingawa wengi hawakujua nini sababu na wengine walidhani ni uchafu wodini walikolazwa.

Mkazi wa jijini hapa, Munira Said alisema huduma hiyo itawanufaisha wazazi wanaotoka maeneo ya mbali au kutokuwa na ndugu kupata huduma ya maji moto ambayo ni muhimu baada ya kujifungua.

“Ubunifu wa namna hii ndiyo unaotakiwa, sasa tutapunguza kutembea na madumu ya maji tunapokuja kuona wazazi,” alisema Munira.