Sababu za mwasho huu kwa wanaume

Mwasho katika maeneo ya uzazi kwenye ngozi ya pochi inayobeba kiwanda cha kuzalisha mbegu za kiume yaani kokwa ni moja ya tatizo ambalo kila mwanaume amewahi kulipata katika maisha yake. Mwasho huo unaowasha kupita kiasi hatimaye kumlazimisha mwathirika kujikuna mara kwa mara huwapata zaidi wanaume waliobalehe na kuendelea.

Mwathirika huona na nafuu anapojikuna kiasi cha kupata hisia za raha au buruduani ndiyo maana ni kawaida kujikuta akishindwa kujizuia kujikuna hata mbele za watu.

Kipindi hiki ambacho baadhi ya maeneo hasa ya Pwani na kaskazini kama Mkoa wa Kilimanjaro hali ya hewa ni joto kali, hivyo wanaume hushtaki tatizo hili kwa wataalamu wa afya.

Zipo sababu mbili zinazochangia wanaume kupata muwasho katika maeneo hayo ikiwamo fangasi za ngozi na mkereketo unaotokana na vimichubuko.

Hali hii inachangiwa na usafi duni au kutokwa jasho kupita kiasi kwenye eneo hilo ambalo lipo katikati ya mapaja.

Eneo hilo kimaumbule huwa ni rahisi kupata vimichubuko vidogo vidogo visivyoonekana kwa macho wakati wa majukumu ya siku ikiwamo kutembea.

Wanaume wanene au wenye mapaja makubwa yanayobana eneo la kati wako katika hatari zaidi ya kupata vimichubuko vinavyoleta mkereketo.

Vimichubuko hivyo husababisha mkereketo au shambulizi juu ya ngozi kutokana na kuvamiwa na vimelea hatimaye kuwasha.

Kanaweza kuwa ni kamwasho kadogo lakini baadaye unapojikuna kumbe ndiyo unaongeza vimichubuko zaidi hivyo kuwasha zaidi na hatimaye kujikuna.

Na kama usafi wa eneo hilo utakuwa ni duni ni kawaida kuvamiwa na vimelea wa fangasi ambao huitaji hali ya unyevunyevu na joto joto ili kujistawisha na kushambulia.

Uambukizi wa fangasi wa ngozi mara kwa mara huwapata wanaume katika kipindi hiki cha joto lakini hata katika maeneo ya baridi wanaweza kupata tatizo hili. Tabia ya uvaaji nguo mbilimbili na ngumu ngumu zinazohifadhi joto huchangia eneo hilo kutokwa na jasho jingi, hivyo kuwa katika mazingira mazuri kwa fangasi. Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu