Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Si pweza pekee, bali samaki wa aina zote huamsha hamu ya kujamiiana - Utafiti

Umewahi kusikia au kuaminishwa kuwa samaki aina ya pweza wanahamasisha kujamiiana?

Sasa siyo pweza pekee bali samaki wa aina zote wana nafasi kubwa ya kusaidia kuamsha hisia za kujamiiana na kutia mimba mara tatu zaidi, utafiti mpya ulitoka umebainisha hilo.

Utafiti huo uliochapishwa wiki hii kwenye Jarida la Metro, umeonyesha ulaji wa samaki angalau mara tatu kwa wiki husisimua hamu ya kujamiiana na kuyapa manii nguvu mara tatu ya kutungisha mimba.

Watafiti hao kutoka Marekani, wamebaini kuwa samaki ana protini nyingi inayosisimua hamu ya kukutana kimwili kama mwanamke na mwanaume wote watawatumia kwa kiwango sawa.

Utafiti huo unaonyesha mbali na kusisimua hamu ya kujamiiana, pia huzipa uhai mbegu za kiume na kuyafanya mayai ya mwanamke kuwa imara na yenye afya.

Pia, umebaini kuwa ili wenza hao wapate faida hizo za samaki wale angalau mara tatu kwa wiki.

Wanasayansi kutoka katika Chuo cha Afya ya Umma Havard cha Marekani, waliwafanyia utafiti wanandoa na wapenzi 501 waliokuwa wakijaribu bila mafanikio kupeana ujauzito na walikuwa wamepoteza hamu ya kujamiiana na walibaini baada ya kula samaki kwa wingi kila kitu kilirudi kama zamani.

Utafiti huo pia umebaini asilimia 39 ya wenza hao walikuwa na hamu zaidi ya kufanya mapenzi siku walizokula samaki wote kwa kiwango sawa.

Walisema waliokula posheni mbili kwa wiki walikuwa na hamu ya kukutana kimwili mara nane kwa mwezi ukilinganisha na waliokula chini ya hapo ambao hupata hamu ya kukutana kimwili mara sita.

Kiongozi wa utafiti huo, Dk Audrey Gaskins alisema asilimia 92 ya waliokula samaki walipata mimba ndani ya mwaka mmoja, ukilinganisha na asilimia 79 ambao hawakula samaki.

“Nawashauri wenza kushirikiana kula samaki zaidi kwenye mlo wao wa kila siku ili kupata faida hizo, ni vema pia robo tatu ya mlo ukawa ni samaki,” anasema Dk Gaskins.

Kwa Tanzania

Utafiti huo unaungwa mkono na Mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mariam Nyamwaira anayesema samaki wa aina zote wana omega 3 inayosisimua damu inayofanyakazi hadi kwenye viungo vya uzazi.

Nyamwaira anasema samaki ana madini ya Nitric Oxide (NO) ambayo ipo kwenye mfumo wa gesi isiyo na rangi na inafanya kazi ya kuzisaidia chembe za mwili kuwasiliana na mifumo ya fahamu mwilini.

Anasema Nitric oxide inafanya kazi nyingi mwilini, hasa kwenye suala la nguvu za kiume. Mtaalamu huyo anasema nitric oxide inafanya kazi ya kusisimua mirija yote ya damu mwilini na hasa ile iliyopo kwenye mfumo wa uzazi na hivyo kuruhusu damu isafiri kwa kasi na ujazo unaotakiwa kwenye mirija iliyopo kwenye mfumo uzazi.

“Ili uume uweze kusimama kikamilifu, inatakiwa damu isafiri kwa kasi na ujazo unaotakiwa na mchakato huu unafanikiwa kwa sababu nitric oxide inawasiliana na mfumo wa damu ili kuisisimua ile mishipa ya damu iweze kuipitisha kwa kasi wakati ambao tayari moyo umeshasukuma damu kuileta kwenye mishipa na mwanaume yupo tayari kisaikolojia, ”anasema.

Anasema kirutubisho kiitwacho ‘nitrates’, husaidia mwili kuzalisha nitric oxide kwa wingi na kina kinapatikana kwa wingi kwenye samaki na mboga za majani.

Mtaalamu huyo anasema kwenye samaki kunapatikana pia madini ya zinc ambayo kazi yake kubwa ni kuzalisha kichocheo kinachoitwa ‘testosterone.’ Ili mwanaume aweze kupata hisia ya kutaka kujamiiana, kichocheo hicho kinatakiwa kiwe kwenye kiwango kikubwa.

Anasema madini ya zinc ndiyo yanayofanya kazi kubwa ya kuhakikisha kichocheo cha testosterone kinazalishwa kwa wingi mwilini.

Hivyo kwa tafsiri nyingine, ni kadiri madini ya zinc yanavyozalisha homoni ya testosterone kwa wingi, na mwanaume naye anakuwa katika nafasi nzuri ya kupokea hisia na hujiweka tayari kushiriki tendo.

Licha ya madini ya zinc kupatikana kwenye samaki, Nyamwaira anasema yanapatikana pia kwenye mbegu za maboga, za matikiti, vitunguu saumu na ngano.

“Kwa ujumla samaki ana kila aina ya madini, protini, fati zinazochangia kwa kiasi kikubwa suala zima la kushiriki tendo la ndoa kikamilifu,” anasema mtaalamu huyo wa lishe.

Kaimu Mkurugenzi wa Chakula na Lishe, Dk Vincent Assey anasema hajawahi kufanya utafiti kuhusiana na samaki kusaidia katika tendo la kujamiiana.

“Ninachojua samaki wana protini zinazosisimua mishipa ya fahamu hivyo inawezekana zikawa na nafasi kubwa katika hilo, kwa sababu tendo hilo huhitaji uimara wa mwili na mishipa ya fahamu, ” anasema Dk Assey.

Anasema samaki pia ana wingi wa protini na fati ambayo husaidia mwili katika mambo mengi. Anafafanua, protini husaidia kutengeneza chembe chembe za mwili.

“Mafuta husaidia kuupa mwili nguvu na unaweza usipate vitu vingi vinavyohitajika katika mwili vikiwamo vya mafuta, lakini ukila samaki unakuwa umekula vyakula vinavyotia nguvu kutokana na mafuta yake.

“Samaki anapatikana kwenye maji ambako kuna madini mbalimbali yanayotengeneza mishipa ya fahamu inafanya kazi kwa wepesi, inasaidia pia kupeleka taarifa haraka kwenye ubongo,” anasema dakatari huyo.

Anasema wanaokula samaki kwa wingi huwa na kinga ya maradhi ya goita, shambulio la moyo na kupooza.

Anasema kuna omega 3 inayopatikana kwa wingi kwenye samaki ambayo inasaidia ukuaji wa mwili na akili, hivyo kufanya chakula hicho kuwa na faida nyingi kwa mwili wa binadamu.

Naye mchuuzi wa pweza katika Soko la Samaki la Kimataifa Feri, Harun Sufian anasema wanaume ndiyo wateja wake wakubwa wa bidhaa hiyo.

Anasema hupata wateja wa kike lakini siyo kwa idadi kubwa kama wanaume. “Huwa nawasikia wengi wao wakisema inawasaidia kukidhi haja za wake zao na za kwao pia.

“Mimi pia nalitambua hilo, ukila pweza kila mara bwana huwezi kuadhirika nyumbani, heshima inakuwepo ya kutosha, ” anasema Sufian huku akicheka.