Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yaja na mpango kukabiliana na Ebola, mikoa 11 yatajwa

Muktasari:

  • Mpango huo wa miezi sita umeundwa kuimarisha uwezo wa nchi katika kuzuia, kugundua mapema na kukabiliana kwa ufanisi na tishio la mlipuko wa virusi vya Bundibugyo.

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imetangaza mpango wa taifa wa dharura wa miezi sita wa kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo (BVD) huku ikitaja mikoa 11 iliyo katika hatari ya kuingiliwa na ugonjwa huo.

Hatua hiyo inakuja kufuatia ripoti za milipuko ya ugonjwa huo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda, hali ambayo imeongeza tishio la maambukizi kuvuka mipaka, na hivyo Shirika la Afya Duniani (WHO) kuitaja Tanzania kuwa iko kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo.

Hata hivyo, jana Julai 27, 2026 Wizara ya Afya nchini Tanzania ilisema Tanzania haina mgonjwa yeyote wala mtu anayeshukiwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.

Kwa mujibu wa mpango huo wa kitaifa wa dharura uliosainiwa na Katibu Mkuu, Dk Grace Maghembe, mikoa 11 imewekwa katika kundi la hatari zaidi kutokana na mwingiliano mkubwa wa kibiashara na usafiri mipakani.

“Mikoa hiyo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Mbeya, Mwanza, Rukwa na Songwe,” umeeleza mpango huo.

Vigezo vilivyotumika kuainisha mikoa hiyo ni pamoja na muunganiko wa usafiri wa anga, barabara, reli na maji kupitia Ziwa Tanganyika na  Ziwa Victoria, pamoja na harakati za wakimbizi na wafanyabiashara katika nchi za Uganda na DRC.

Kupitia mpango huo, Serikali imekadiria kutumia jumla ya Sh13.48 bilioni (Dola za Marekani milioni 4.8) katika kipindi cha miezi sita katika utekelezaji.

Fedha hizo zitatumika katika mifumo ya ufuatiliaji (Surveillance) na maabara, usimamizi wa wagonjwa na udhibiti wa maambukizi (IPC).

Pia zitatumika latika mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii (RCCE) na uimarishaji wa uchunguzi katika vituo vya kuingilia mipakani.

“Mpango huu unalenga kulinda afya ya umma, kuimarisha usalama wa afya, na kulinda utegemezi wa kiuchumi ikiwemo utalii na biashara,”imeelezwa.

Utekelezwaji wa mpango huo utazingatia sera, sheria, mikakati na mipango ya nchi inayoongoza usimamizi wa dharura za afya ya umma na majanga.

Katika utekelezaji wa mpango huo, Wizara ya Afya itaratibu na kushirikiana na sekta nyingine pamoja na wadau mbalimbali kwa kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Matukio ya Dharura  katika ngazi zote.


Msisitizo wa hatua

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akiwa mkoani Kilimanjaro Julai 27, 2026 amesema Serikali imeimarisha ulinzi wa afya katika maeneo ya mipakani ili kuzuia ugonjwa wa Ebola kuingia nchini.

"Kumekuwa na kazi kubwa ikiendelea kufanyika katika maeneo ya mipakani, hasa yale yaliyopo karibu na nchi zenye maambukizi. Hadi sasa hakuna mgonjwa wa Ebola nchini wala mtu anayeshukiwa kuwa na ugonjwa huo na tutaendelea kuimarisha ulinzi afya," alisema.


Hali ya Ebola

Shirika la Habari la AP la nchini Marekani, linaeleza idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya Ebola katika mlipuko unaoendelea DRC imefikia 3,262, huku watu 1,437 wakifariki dunia.

Kwa mujibu wa AP, ikinukuu taarifa ya Wizara ya Afya ya DRC iliyotolewa usiku wa kuamkia leo, idadi hiyo inakaribia mlipuko wa Ebola wa mwaka 2018 hadi 2020, ambao ndio mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.

Taarifa hiyo inaonyesha mlipuko wa sasa umejikita zaidi katika Jimbo la Ituri, mashariki mwa DRC, huku maafisa wa afya wakisema ndio mlipuko wa Ebola unaosambaa kwa kasi zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.

AP imesema mlipuko wa Ebola wa 2018 hadi 2020 nchini DRC na Uganda ulidumu kwa takribani miaka miwili, ukisababisha zaidi ya wagonjwa 3,400 na vifo zaidi ya 2,200, kwa mujibu wa takwimu za Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani (CDC).

Ni mlipuko wa Afrika Magharibi wa mwaka 2014 hadi 2016 uliokuwa mbaya zaidi katika historia, ukirekodi zaidi ya wagonjwa 28,000 na vifo zaidi 11,000.