TUONGEE KIUME: Sisi tuko hivi, wanawake wanataka tuwe vile

Ukweli ni kwamba, hutakiwi kujichosha kuwa mwanamume anayemtaka mwanamke hatofanikiwa. Na sio wewe tu, tangu dunia hii ianze hakuna mwanaume aliyefanikiwa kwenye hilo.

Wakati mwanamume anataka mwanamke ambaye labda anampenda na kumuheshimu tu, wanawake wenyewe wanataka mwanaume mwenye mwili wa mazoezi, ambaye akichomekea anapendeza.

Mwanamume anayejua kupika ili wikiendi yeye akiwa anaangalia tamthilia, mwanamume aingie jikoni ampikie, amuandalie mezani na kumlisha huku akipooza chakula kwa kikupuliza kwa mdomo.

Pia, mwanamume huyo huyo mwenye mwili wa mazoezi na anayejua kupika awe ‘handsome’ ili wakitoka wakipiga picha aweze kupost kwenye mitandao, siye mwenye sura kama nyuma ya sufuria hatuwezi kupendeza hata picha zikihaririwa kwa kompyuta.

Kisha huyo huyo ‘handsome’ anatakiwa awe na kazi nzuri. Awe kwenye ofisi moja kali ‘full’ kiyoyozi hapo mjini, Posta.

Na isiwe kazi nzuri tu, pia awe na pesa zinatosha kununua gari nzuri, kuishi kwenye nyumba nzuri. Pia, pesa za kutosha kutoka kila wikiendi.

Bado unatakiwa uwe hupendi mpira, huvuti sigara, hunywi pombe , huna marafiki au kama unao basi wachache na sio wale wa kufuatana nao mara twende baa, sijui twende Taifa kwenye mechi ya Simba Yanga, hutakiwi.

Pia, uwe unapenda muziki, unajua kucheza sana na kuimba angalau kwa mbali.

Pia, usiwe na mtoto au kama unaye usiwe unawasiliana na mama yake. Wanawake ndiyo wanataka mwanamume wa aina hii.

Ukisoma vigezo vyote hivi utagundua kuwa kwa neno moja wanawake wanataka mwanamume mzuri, kama ambavyo sisi pia tunapenda mwanamke mzuri.

Lakini tofauti yetu na wao ni kwamba wenyewe wanachagua kwa kuangalia vitu vidogo vidogo sana ambavyo nikisema havina maana sijui kama hawataona nawatukana.

Wengine wanaweza kujitetea kwamba vigezo hivyo sio vya mwanamke, ni vya msichana. Ni kweli sio uongo, lakini kabla ya kuwa mwanamke, wanawake wote huwa wasichana. Na katika kipindi hicho ndipo wanawake wanafanya uchunguzi kwa wanaume kana kwamba wanataka kuajiri askari.

Matokeo yake wanashindwa kupata mwanaume ‘handsome’ mwenye hela, gari nzuri, nyumba nzuri, anayejua kupika, asiyekunywa pombe, kuvuta sigara, asiyekuwa na mtoto na mwenye marafiki wachache au asiyekuwa na marafiki kabisa.

Huwezi kupata mwenye sifa hizi zote kwa pamoja kwa hiyo wakishaanza kuona usichana wao unafifia na sasa wanaelekea kwenye kuwa wanawake ndipo wanaamua kuokota yeyote anayepita mbele.

Wakishafikia hatua ya kuokota hapo ndiyo sisi wenye vitambi, tusiokuwa na kazi ya kueleweka, walevi, wavuta sigara, wenye watoto na tusiokuwa na hela tunapewa nafasi.

Sio mbaya kupenda vitu vizuri, lakini kufikiri unaweza kupata mwanamume ambaye ni mkamilifu ni kujidanganya. Sisi ni binadamu sio malaika, tumeumbwa kwa msingi wa kuchanganya mabaya na mazuri.