Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upungufu watalaamu wa dawa ngazi ya msingi watajwa kufikia asilimia 81

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) Fadhili Hezekiah akizungumza Jana na vyombo vya habari, kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafamasia duniani.

Muktasari:

  • Tanzania ikiadhimisha Siku ya Famasia duniani, inakabiliwa na upungufu wa wataalamu wa kada hiyo kwa asilimia 57 katika vituo vyote vya afya na asilimia 81 katika ngazi ya msingi.

Dar es Salaam. Tanzania inakabiliwa na upungufu wa wataalamu wa kada ya famasia na wateknolojia dawa kwa asilimia 81 katika ngazi ya msingi, hali inayotajwa na wataalamu kuchangia wagonjwa kutopata huduma stahiki za dawa.

Vituo vya ngazi ya msingi vinavyojumuisha hospitali za Wilaya, halmashauri, vituo vya afya na zahanati, ndivyo vinavyohudumia asilimia 80 ya Watanzania.

Takwimu hizo zinaonyesha uwepo wa wataalamu hao katika ngazi za msingi ni asilimia 19 pekee, hali inayotajwa na wataalamu kuwa inaweza kuleta athari, huku serikali ikieleza mikakati iliyopo.

Hata hivyo takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuna wateknolojia dawa zaidi ya 23,000 na wafamasia zaidi ya 3000, hivyo kundi hili pamoja na wateknolojia dawa wasaidizi jumla ni 35,000 na kwamba kuna maduka ya dawa 25,000 nchi nzima.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 25, 2024 na wafamasia wakati wa mafunzo kwa vyombo vya habari ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hayo.

Wataalamu wa dawa wametaja madhara yanayoweza kujitokeza endapo kutakuwa na utolewaji wa huduma za dawa na kada ambazo siyo za famasi, ni pamoja na uwezekano wa kutokutoa taarifa sahihi kwa mgonjwa kuhusiana na dawa husika.

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah amesema mafunzo wanayopewa wataalamu wa dawa huhusisha uwepo wa taarifa sa msingi, ambazo mfamasia anatakiwa kuongea na mgonjwa.

“Taarifa za dawa si za ujumla zinazohusiana na uhifadhi, utumiaji, ukiacha ile dozi taarifa ya dawa siyo dozi kwamba anatumia mara ngapi kwa kutwa, kuna taarifa zingine nyingi ambazo mtu wa kada nyingine hatakuwa anazifahamu.

“Mwishowe itabaki dawa zinatolewa kama kugawiwa, lakini yale maelezo sahihi hayatolewi na hiyo inasababisha watu kutokupata matokeo yaliyotarajiwa kwa matibabu husika,” amesema Hezekiah.

Pia amesema watu wanaweza kupata madhara yatokanayo na kutopata taarifa sahihi na kutumia dawa isivyo sahihi.

Pia ametaja mgongano wa maslahi katika kumueleza mgonjwa kama kuna changamoto, “Asiye na taaluma ya dawa anaweza kushauri badala ya hili fanya hivi, kitu ambacho si sahihi kwa mfano dawa ya amepewa ya kumeza mtaalamu mwingine anafahamu habari ya kuchoma sindano.”

Alipoulizwa iwapo hilo linachangia usugu wa dawa, Hezekiah amesema usugu ni jambo mtambuka na kwamba upungufu wa watumishi unaweza kuchagiza hilo.

“Inapotokea mtumishi anazidiwa na wagonjwa, maelezo yake anapotoa dawa hayawezi kuwa ya kujitosheleza, matokeo yake mtumiaji ataenda kuitumia pasipokuwa na taarifa sahihi na hilo linaweza kusababisha dawa ikatumika vibaya kwa maana ya kutokumaliza dozi na mwisho wa siku ikamletea shida.

“Hasa anapoanza kupata ahueni na kama hakuambiwa uendelee mpaka dawa itakapokwisha, njia nzuri ya kutumia kuepuka vitu kadhaa ili dawa isipungue nguvu, atajikuta dawa inayokua kwenye mwili kutibu ni kidogo na wadudu wanaanza kuizoea na kusababisha usugu hili ni jambo muhimu.”

Amesisitiza kuwa pamoja na hayo usugu pia husababishwa na mambo mengi ikiwemo dawa zinazopita shambani kwenye mimea, katika mifugo na mifumo ya maji.


Serikali yafafanua

Kukiwa na changamoto hiyo, serikali imekiri upungufu huo na kwamba juhudi zinazoendelea kwa sasa ni kuwaajiri, ambapo kwenye kila nafasi zinazotolewa za ajira kila mwaka kuna wataalamu wa dawa wanaajiriwa kwa wastani usiopungua 100 mpaka 200 kuanzia  wafamasia, wateknolojia dawa na wateknolojia wasaidizi.

Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema lengo ni kuona kila siku serikali inapunguza pengo  lililopo ingawaje bado kuna juhudi za ziada zinahitajika kwa sababu ongezeko la vituo vya afya nchini ni kubwa.

Amesema serikali inawekeza sana katika sekta ya afya na kwa mwaka kuna wastani wa vituo si chini ya 500 vinaongezeka.

“Hata ukiongeza wataalamu 500 unaona pengo lipo, kwahiyo ni eneo ambalo serikali inalifanyia kazi kwa kutoa nafasi za ajira kwa kadri inavyowezekana,” amesema.

“Kuna upungufu wa wataalamu wa kada ya dawa kwa asilimia 57 katika vituo vyote, ngazi ya msingi tulifanya utafiti na tathmini mwaka jana Novemba, tukabaini zaidi ya asilimia 81 wanaotoa huduma za dawa si wataalamu wa dawa kwa ngazi ya msingi.

“Hapa kuna hoja twende kuona utaratibu wa kuimarisha ngazi ya msingi ili tuweze kupata huduma bora kwa kuwa kwa sasa kuna hilo pengo, hii ni tathmini ambayo tuliifanya mwaka jana na tunaendelea kuifanya pia mwaka huu.”

Msasi ametaja njia nyingine wanayoitumia ni kuendesha zoezi la mafunzo kwa kila robo mwaka kupitia timu maalum kutoka katika ofisi yake, wataalamu wa dawa kutoka mkoani na halmashauri na kwenda moja kwa moja kwenye vituo.

“Tunakaa na mtaalamu kwenye kituo awe daktari, tabibu, muuguzi tunamshauri namna ya kugawa dawa, kutoa taarifa, kusimamia bidhaa za dawa ili angalau kusiwe na hilo pengo kubwa na huduma  ziendelee kutolewa licha ya kuwepo na hiyo changamoto, lakini lengo la serikali ni kuendelea kuajiri wataalamu wa dawa,” amesema.

Matumizi yasiyorasmi ya antibaotiki yamedaiwa husababisha usugu wa vimelea kuongezeka nchini ambapo mwaka 1993 matumizi ya dawa za antibaotiki yalikuwa asilimia 39, mwaka 2002 asilimia 42, 2014 asilimia 67.7 na mwaka 2017 hadi 2022 wastani wa asilimia 65.

Matokeo ya tafiti iliyofanyika mwaka 2017 yalionyesha asilimia 92 ya wagonjwa hupata matibabu yao katika maduka ya dawa na kati yao asilimia 92.3 hununua antibiotiki holela bila kutumia cheti cha dawa kilicho idhinishwa na daktari.

Kuhusu siku ya famasia

Mfamasia ni mtaalamu wa afya aliyebobea kwenye masuala ya dawa na ndiye anayajua mambo mengi kuhusu usalama, utendaji ufanisi na ubora wa dawa.

Mfamasia ana jukumu la kuhakikisha mgonjwa anapata dawa zilizo na ubora, kuhakikisha utoaji wa dawa za binadamu unafuata sheria na kanuni zilizopo kuhakiki kama dawa anazopata mgonjwa zinamfaa na kuelekeza jinsi dawa zinavyopaswa kunywewa/kutumika na pia kumsaidia au kujibu maswali ya mgonjwa juu ya dawa.

Msasi anasema wafamasia wanawajibu wa kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa ili kupunguza athari za usugu.

Anasema hapo awali lengo la kuanzishwa kwa maduka ya dawa muhimu ilikua ni kufikia maeneo ambayo yana uhitaji wa dawa hasa ya pembezoni lakini sasa imekua tofauti na kuwa wameandaa kitabu chenye mpango kazi wa kupambana na usugu wa vimelea vya dawa utakaoenda hadi mwaka 2028.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Dawa na VifaaTiba - TMDA Kanda ya Afrika Mashariki, Adonis Bitegeko amesema wamekuwa wakifanya ukaguzi na ufuatiliaji wa dawa huku akitoa rai na ushauri kwa wanataaluma wa dawa.

Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania, Boniface Magige amesema wafamasia wanashiriki kikamilifu katika mfumo wa afya kwa kutoa huduma ikiwemo kuelimisha wagonjwa kuhusu matumizi sahihi ya dawa, kuzuia madhara ya dawa na kushirikiana na wataalamu wengine wa afya kuhakikisha usalama na ufanisi wa matibabu.