Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uwekezaji wa Sh34 bilioni kuboresha mafunzo ya wahudumu afya EA

Mmoja wa watoa huduma za afya kutoka Shirika la Utafiti na Tiba Barani Afrika (Amref Health Africa) akitoa huduma mkoba ya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza, NCDs katika moja ya kambi za matibabu zilizofanyika nchini Uganda.

Muktasari:

  • Zaidi ya wataalamu 28,500 wa afya wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja, huku wanafunzi zaidi ya 72,800 wakifikishiwa mafunzo yaliyoboreshwa.

Dar es Salaam. Wakati magonjwa yasiyoambukiza yakiendelea kuongezeka kwa kasi, taasisi mbili za masuala ya afya, Amref Health Africa na Novo Nordisk Foundation, zimezindua mpango wa kupanua na kuboresha mafunzo ya wataalamu wa afya Afrika Mashariki, kupitia uwekezaji wa dola za Marekani milioni 13.2 (takriban Sh34 bilioni).

Chini ya mpango huo wa pamoja, jumla ya taasisi 55 za mafunzo ya afya katika nchi za Kenya, Uganda, Tanzania na Ethiopia zitaimarishwa ili kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kuzuia na kutibu magonjwa yasiyoambukiza.

Uzinduzi wake umefanyika leo Jumanne, Aprili 28, 2026, kando ya mkutano wa afya wa kikanda unaoendelea jijini Nairobi, Kenya.

Mpango huo wa miaka mitatu unalenga kukabiliana na ongezeko la magonjwa ya moyo, kisukari na magonjwa mengine ya mfumo wa mwili yanayojulikana, ambayo kwa sasa yanachangia takriban asilimia 40 ya vifo vyote katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa muda mrefu, juhudi nyingi za afya duniani zimejikita katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza. Hata hivyo, mwelekeo umebadilika kwa kasi, huku magonjwa sugu yasiyoambukiza yakiongezeka na kuweka shinikizo jipya kwa mifumo ya afya ambayo kwa kiasi kikubwa haijaandaliwa ipasavyo kuyakabili.

Changamoto kubwa iliyobainishwa ni pengo la mafunzo kwa wataalamu wa afya, ambapo vyuo vingi vinatumia mitaala iliyopitwa na wakati, vina miundombinu hafifu ya kidijitali na vinakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kisasa vya mafunzo ya vitendo.

Kupitia mpango huo, taasisi hizo 55 zitapewa uwezo wa kuboresha mafunzo ili kuandaa wataalamu wanaoweza kukabiliana moja kwa moja na mzigo wa magonjwa hayo.

Inatarajiwa kuwa zaidi ya wataalamu 28,500 watanufaika moja kwa moja, huku wanafunzi zaidi ya 72,800 wakipata mafunzo yaliyoboreshwa kupitia mfumo huo mpya.

Aidha, vituo 12 vya ubora  vitaanzishwa na kufanya kazi kama vituo vikuu vitakavyosaidia taasisi nyingine 43 kupitia mfumo wa hub-and-spoke. Mfumo huu unalenga kusambaza maarifa, utaalamu na rasilimali kwa upana zaidi, hususan katika maeneo ya vijijini yenye upungufu mkubwa wa wataalamu wa afya.

Mpango huo pia utaweka mkazo katika matumizi ya teknolojia za kisasa katika elimu ya afya. Hii ni pamoja na mafunzo ya kidijitali yanayoboreshwa kwa kutumia akili unde (AI), matumizi ya maabara za kuiga (simulation labs), pamoja na mfumo wa masomo mseto unaochanganya ujifunzaji wa ana kwa ana, simu na mtandao.

Hatua hizi zinakusudia kufanya elimu ya afya iwe rahisi kupatikana na yenye ufanisi zaidi, hasa katika maeneo yenye rasilimali chache.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa uwekezaji huo, Ofisa Mkuu wa Sayansi wa Novo Nordisk Foundation, Profesa Flemming Konradsen, amesema hatua hiyo ni ya kimkakati kwa mustakabali wa sekta ya afya.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika taasisi zinazozalisha wataalamu wa afya ni msingi muhimu wa kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, huku ukijenga uwezo wa kufundisha, kufanya utafiti na kutoa huduma bora kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Amref Health Africa, Dk Githinji Gitahi amesema Afrika inahitaji suluhisho zinazoongozwa na Waafrika wenyewe ili kukidhi mahitaji halisi ya mifumo ya afya ya bara hilo.

Ameeleza kuwa kuimarisha elimu ya afya si jambo la ziada, bali ni msingi wa kujenga mifumo imara ya huduma za afya, yenye uwezo wa kuwafikia hata walio pembezoni.

Mbali na hilo, amesema mpango huo utaweka msisitizo mkubwa katika usawa kwa kuhakikisha kuwa mafunzo yanafika hadi maeneo ya vijijini ambako uhaba wa wataalamu wa afya ni mkubwa.

Pia utatoa fursa kwa wanafunzi wa uzamivu (PhD) kutoka kila nchi shiriki, kukuza uongozi wa kitaaluma na tafiti ndani ya taasisi husika, pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya afya, amesema.

Kwa mujibu wa waandaaji, maboresho yote yatakayofanywa yataingizwa ndani ya mifumo ya kitaifa ili kuhakikisha yanaendelea kuwa endelevu hata baada ya ufadhili kuisha.

Hatua hii inatarajiwa kuziwezesha nchi za Afrika Mashariki si tu kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, bali pia kujenga mifumo madhubuti itakayoweza kujibu changamoto nyingine za afya zitakazojitokeza siku zijazo.