Vyakula pendwa, hatari kwa afya

Dar es Salaam. Unapenda kula saladi/kachumbari, nyama choma, mayai ‘macho ya ng’ombe’, maziwa yasiyochemshwa na vinginevyo? Unapaswa kuchukua tahadhari unapokula vyakula hivi ili kuepukana na changamoto za kiafya.

Wataalamu wa afya wanasema vyakula vinaweza kutokuwa salama kwa mlaji kutokana na mambo mbalimbali, ikiwemo maandalizi na upikaji ikiwa hakijaiva vizuri.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takriban watu milioni 600, ikiwa ni wastani wa mtu mmoja katika kila watu 10 huugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama, huku watu 420,000 kati yao hufariki dunia.

Pia inaelezwa watoto walio na umri chini ya mwaka mmoja pamoja na wazee ni miongoni mwa makundi ya watu wanayoongoza kuwa katika hatari ya kuathirika zaidi na tatizo hilo.

Akizungumza na Mwananchi, Meneja Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto wa Shirika la Word Vision, Dk Daudi Gambo anasema kila chakula kuna aina yake ya mapishi na matayarisho ambayo yameruhusiwa kitaalamu.

 Dk Gambo, ambaye pia ni mtaalamu wa lishe, anatolea mfano mboga za majani hazitakiwi kupikwa sana ili kubaki na virutubisho kwa kuwa vitamini zilizomo zina tabia ya kutoweka zinapokuwa katika hali ya kiwango kikubwa cha joto.

“Ingekuwa si kwa sababu ya kuhofia magonjwa, mboga za majani zisingekuwa zinapikwa kabisa, lakini inashauriwa kuzipika kwa wastani ili kuua bakteria na kuzifanya kuwa salama kuliwa,” anasema.

Kwa upande wa vyakula vya protini, anasema inashauriwa viliwe vikiwa vimeiva vizuri na katika kiwango kinachotakiwa, ili kurahisisha mmeng’enyo kama ilivyo katika vyakula vyenye asili ya wanga na mafuta.

“Ulaji wa chakula cha protini kisichoiva ipasavyo kinasababisha mmeng’enyo wake kuwa mgumu…vyakula vya protini vinavyotokana na wanyama visivyoivya ipasavyo au kuandaliwa vizuri vinasababisha mtu kupata maradhi ya tumbo,” anasema.

Kuhusu maziwa, Gambo anaeleza yanatakiwa kuchemshwa vizuri ili kuondoa bakteria wanaoweza kusababisha magonjwa mbalimbali, ikiwemo kuumwa tumbo pamoja na Kifua Kikuu.

Kwa wale wanaopendelea kula saladi, anasema ni vema kuhakikisha zimeandaliwa katika hali ya usafi ili kuepuka kujiweka katika hatari ya kuumwa tumbo, kuhara, kutapika, kupata ugonjwa wa Taifodi, minyoo pamoja na Amoeba.

Kwa mujibu wa tovuti ya Better Health, ulaji wa chakula kisichoiva vizuri unaweza kusababisha sumu au maambukizi kwenye chakula. Hiyo ni hali ya kuchafuka kwa chakula kunakotokana na uwepo wa vimelea mbalimbali kama bakteria, virusi au sumu.

Kwa upande wake, daktari wa magonjwa ya binadamu, Shita Samwel anaunga mkono kauli ya Dk Gambo, huku akieleza ni vema watu kuzingatia uandaaji na upishi wa vyakula kitaalamu ili kupata virutubisho vinavyopatikana katika vyakula husika na kujiepusha na maradhi.

“Hakikisha unapika chakula hadi kiive vizuri kwa kuzingatia kiwango cha joto kinachopendekezwa na wataalamu,” anasema.

Kwa mujibu wa tovuti ya State Food Safety, upikaji mzuri wa chakula unaweza kuua vimelea wote hatarishi na kueleza kuwa chakula kilichopikwa kwenye nyuzi joto 70 ni salama.

Tovuti ya Medium inaeleza kwa wastani vyakula aina ya mbogamboga vinatakiwa kupikwa katika nyuzijoto 65, huku vya kuchemsha hasa vile vitokanavyo na wanyama vinashauriwa kupikwa kwa zaidi ya nyuzijoto 100.


Wanaopunguza miili

Kuna baadhi ya watu wamejiwekea utaratibu wa kupenda kula saladi, hasa wale waliopo katika mchakato wa kupunguza miili, hivyo nao wanatakiwa kuchukua tahadhari wakati wa uandaaji wa chakula hicho.

Mbali na wataalamu wa afya kushauri chakula hicho kiandaliwe vizuri, kinatakiwa kupitishwa katika moto mdogo, hasa mboga za majani ili kuua vijidudu vilivyomo.

Dk Gambo anasema hali hiyo inatokana na mboga hizo kuandaliwa katika mazingira tofauti, hasa maji yanayotumika kumwagilia pamoja na mbolea zinazotumika.


Dhana ya mayai mabichi na sauti

Wapo ambao hula mayai mabichi kwa lengo la kulainisha sauti zao na kuendelea kuwa bora, ikiwamo waimbaji.

Dhana hiyo haina ukweli, wataalamu wanashauri watu kunywa maji ya kutosha ambayo si ya baridi ama barafu ili kuwa na sauti bora.

Ulaji wa mayai mabichi wa mara kwa mara una athari, kwani kuna hatari ya kuambukizwa salmonellosis au homa ya ndege.

Mbali na ulaji mayai mabichi, pia kuna watu wanaopenda kula yasiyoiva, mfano ‘macho ya ng’ombe’ si ya kugeuza ambayo huiva upande mmoja, chipsi mayai ambayo haikauki vizuri, hali ambayo ni hatari kwa afya.

Tabia hii inaweza kuchangia kupata maambukizi ya bakteria wanaosababisha ugonjwa wa kuhara, homa, kutapika na kuumwa tumbo.