Hii hapa dawa wenye unene uliopitiliza

Dar es Salaam. Unafahamu kuwa kujinyima kula au matumizi ya dawa za kupunguza unene, havina matokeo chanya kwa mtu aliyefikisha uwiano wa urefu na uzito (BMI) 35 mpaka 40?

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, BMI inayotakiwa ni 18 mpaka 29.5. Hata hivyo, tafiti zilizowahi kufanyika zinaonyesha njia salama ya kupunguza uzito na isiyo na madhara makubwa kiafya, ni kufanyiwa upasuaji wa kupunguza tumbo la chakula.

Daktari bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Aga Khan, Blessing Nkenda, alisema matibabu ya kupunguza uzito yapo ya aina nyingi, lakini wenye uzito huo ni ngumu kupungua kwa njia za kawaida.

“Huyu mtu hata afanye matibabu ya kupunguza kula chakula peke yake, madawa mbalimbali ya kupunguza uzito, hayawezi kusaidia kwani mahitaji ya mwili wake hawezi kukaa na njaa na akila anakula chakula kingi, utafiti unaonyesha upasuaji pekee ndio unafaa,” alisema Dk Nkenda.

Hospitali ya Aga Khan imekuwa kati ya hospitali za kwanza nchini kufanya upasuaji wa kupunguza uzito (Bariatric Surgery) kwa wagonjwa wanne.

Upasuaji huo umefanyika kupitia ushirikiano na daktari bingwa wa upasuaji wa tatizo la unene kutoka nchini Pakistan mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika fani hiyo, Dk Syed Tanseer Asgher ambaye amefanya upasuaji kwa watu 3,000 kwa mafanikio.

Mkuu wa kitengo cha upasuaji Aga Khan, Dk Athar Ali alisema wameanza kwa wagonjwa wanne na wataendesha kambi nyingine ya upasuaji katika miezi ijayo.


Upasuaji unavyofanyika

“Upasuaji wa kupunguza unene unajumuisha upasuaji wa aina mbalimbali, kama vile upasuaji wa kugawanya tumbo (gastric bypass), unaohusisha kufanya mabadiliko katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula ili kumfanya mtu apungue uzito.

“Ni upasuaji maalumu ambao unafanywa kupitia mbinu ya laparaskopiki, yaani upasuaji wa tundu dogo, unaoweka mkazo katika kusaidia watu walio na unene kupita kiasi kupungua uzito kwa kiwango kikubwa, huku wakiboresha maisha na afya yao kwa ujumla,” alisema Dk Athar.

Alisema unene kupita kiasi ni ugonjwa sugu unaoelezewa kama tatizo la kuwa na mafuta kupita kiasi mwilini.

Katika ngazi ya mtu binafsi, unene kupita kiasi unasababishwa na kula sana vyakula vilivyosindikwa na kutoushughulisha mwili.

Dk Athar aliongeza: “Chanzo kikuu cha kunenepa kupita kiasi mara nyingi ni hali duni kijamii na kiuchumi na ukosefu wa usawa, kwani mambo haya hujidhihirisha kama kukosa maarifa kuhusu tabia zinazozingatia afya na kipato duni kiasi cha kushindwa kuzingatia afya.”

Alisema huduma hiyo ya ubia yenye gharama ya Sh19 milioni kwa wodi za kawaida, Sh20 milioni kwa wodi za kati, ya Sh22 milioni kwa wodi za daraja la kwanza, inalenga kusaidia wagonjwa wanene kupita kiasi kupungua uzito kwa kiwango kikubwa na kuboresha afya kwa ujumla na ubora wa maisha yao katika nchi wanazoishi.

Akizungumzia umuhimu wa huduma hiyo, daktari wa magonjwa ya ndani Hospitali ya Aga Khan, Dk Mandela Makalala alisema:

“Upasuaji wa kupunguza unene umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya huduma za afya kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Kisukari (IDF) mwaka 2019 ambapo wagonjwa 897,000 wa kisukari wameripotiwa nchini ambayo ni asilimia 3.6 ya idadi ya watu wazima.

Alisema kulingana na ripoti ya kimataifa ya lishe (GNR), asilimia 15.2 ya wanawake watu wazima na asilimia 5 ya wanaume watu wazima wana tatizo la unene kupita kiasi nchini Tanzania.

Dk Makalala aliongeza: “Tafiti za hivi karibuni zimeonyesha upasuaji wa kupunguza unene kimsingi unaweza kuwa tiba iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu kwa watu wenye kisukari aina ya 2 na kwa wale wanaosumbuliwa na unene kupita kiasi, ambao hawana kisukari, inaweza kupunguza hatari ya kupata kisukari”.


Uzoefu wa Dk Tanseer

Dk Tanseer alitoa mwanga zaidi juu ya hili kupitia uzoefu wake wa awali na anaongeza kwa kusema:

"Moja ya sababu za kupata nafuu ya ugonjwa wa kisukari aina ya 2 ni kwa sababu ulaji wa chakula unazuiwa mara baada ya upasuaji kufanyika, hasa vyakula vya wanga vilivyokobolewa, ambavyo kwa kawaida havimeng’enywi vizuri baada ya kufanyiwa aina fulani ya upasuaji wa kupunguza uzito.

“Hii inasaidia kupunguza viwango vya sukari kwenye damu, ambayo ina athari ya moja kwa moja kwa ugonjwa wa kisukari. Pili, mgonjwa anapopoteza uzito mkubwa baada ya upasuaji, inaboresha ukinzani wa insulini.’’


Hatua za upasuaji

Akielezea hatua za upasuaji, Dk Nkenda alisema kabla ya upasuaji, mgonjwa anafika na kuangaliwa uzito wake kama umefikisha BMI 35 mpaka 40 au la.

Pia wanaangalia kama ana magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, kwani upasuaji huo hufanyika kwa njia ya matundu.

“Tunamfanyia upasuaji kujihakikishia kama huduma yetu itamfaa na kwa kuwa tunamfanyia upasuaji wa matundu, tunachokifanya ni kupunguza ukubwa wa tumbo la chakula akila kidogo anakuwa ameshiba.

“Atakunywa glasi moja ya maji anakuwa ameshiba, sababu sehemu ambayo umeng’enywaji wa chakula inaanzia, inarefushwa hivyo chakula kikitoka kwenye tumbo kinaingia pale, tunairefusha kama sentimita 50, muda wa umeng’enywaji unakua mfupi, hivyo anaanza kupungua uzito,” alisema.

Akielezea maisha baada ya upasuaji, Dk Nkenda alisema humfuatilia mgonjwa kwa muda mfupi na wakihakikisha hatua zote muhimu wamezivuka, humshauri aanze kula vyakula vya lishe bora.

“Ataanza kula mlo kamili kwa kuzingatia makundi matano ya chakula kwa kiasi na mwezi wa kwanza atapungua kwa kasi na ataendelea hivyo mpaka mwili ufike mahali panapofaa,” alisema.


Sababu za unene

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge, alitaja sababu ya kuwa na uzito mkubwa ni kutopangilia mlo sahihi kwa maana ya kula mlo kamili.

Alisema kwa kawaida kila binadamu anatakiwa kuwa na uwiano sawa kati ya urefu na uzito wa mwili, yaani BMI.

“Kawaida inatakiwa kuwa 18 mpaka 29.5, ikiwa kuanzia 30 kwenda juu ana uzito uliopitiliza, kuna sababu nyingi sana zinazochangia mtu kuwa na uzito uliopitiliza, ikiwa ni pamoja na nyama zembe za mgongoni na kutofuatilia mlo kamili.”

Alisema kitu cha msingi cha kuzingatia ni kuepuka vyakula vyenye mafuta na sukari kwa wingi ambavyo wengi wamekuwa wakivipenda zaidi.

“Mji kama Dar es Salaam unakua kwa kasi na watu hawapati ratiba ya kula vizuri, wanapenda kula vyakula vya mafuta na sukari kwa wingi na wanatumia pombe kupitiliza, vyakula vya kusindika ambavyo ndivyo vilivyozoeleka.

“Ukiangalia vyakula karibu vyote ni vya kusindika, kuna kuku wa kisasa, soseji anakula ili apate ladha mdomoni na havina maana mwilini na vyakula vingi vinawekwa katika mafriji kwa muda mrefu na hivyo vinapoteza ubora,” alisema.

Dk Mkeyenge alitaja changamoto nyingine kuwa ni mafuta hayo kwenda kurundikana kwenye mishipa ya damu, hali inayochochea uzito na kuzalisha tatizo la shinikizo la damu kwa walio wengi, hasa wanawake na wanaume.


Lishe bora

Ofisa lishe mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Fatma Mwasora alisema ili kukabiliana na uzito uliokithiri na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ni muhimu kupunguza vyakula vya mafuta na wanga.

“Ale mbogamboga kwa wingi, asile ugali, wali, mkate kwa wingi, wasiruke milo. Mtu ahakikishe anakula milo mitatu kwa siku na ahakikishe anafanya mazoezi hata kama hapati muda ofisini anaweza kunyanyuka na kutembea kidogo,” alisema.

Akizungumzia ulaji unaofaa, mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila, Theresia Thomas alisema unatakiwa uwe ni mchanganyiko wa mbogamboga na matunda ambavyo huongeza kinga za mwili kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na vyakula vingine.