Prime
Wenye shingo nene wakae chonjo
Muktasari:
- Utafiti mwingi unaonyesha kuwa shingo nene, inaweza kuwa ishara ya hatari ya magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu na matatizo ya moyo.
Mwanza. Katika ulimwengu wa sasa wa tiba, wataalamu wanaendelea kutafuta njia rahisi na za haraka za kutambua hatari za magonjwa sugu kabla hayajawa makubwa.
Moja ya viashiria ambavyo vimepata uzito mkubwa katika kazi za kitafiti za hivi karibuni ni unene wa shingo.
Ingawa kwa wengi inaweza kuonekana kama suala la mwonekano wa mwili tu, utafiti mwingi unaonyesha kuwa shingo nene, inaweza kuwa ishara ya hatari ya magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu na matatizo ya moyo.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na watafiti wa afya ya jamii mwaka 2020 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uliochapishwa katika jarida la International Journal of Diabetes and Endocrinology, shingo nene hupimwa kwa kuangalia mzunguko wa shingo.
Utafiti huo ulibaini kuwa wanaume wenye zaidi ya sentimita 37 walikuwa kwenye hatari kubwa ya matatizo ya kimetaboliki, huku wanawake wenye zaidi ya sentimita 34 pia walionyesha hatari kama hiyo.
Watafiti walihitimisha kuwa kipimo hicho kinaweza kutumika kama njia rahisi ya kuchunguza hatari za kiafya katika jamii zenye rasilimali chache.
Aidha, mapitio makubwa ya kitafiti yaliyofanywa mwaka 2018 na kuchapishwa katika jarida la Diabetology & Metabolic Syndrome, yalichunguza kazi zaidi ya 30 kutoka nchi mbalimbali.
Matokeo yake yalionyesha kuwa watu wenye shingo nene walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata shinikizo la damu, walikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na ongezeko la mafuta mabaya (LDL cholesterol) pamoja na hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Watafiti walieleza kuwa mafuta yanayokusanyika sehemu ya juu ya mwili (ikiwemo shingo) yanaathiri vibaya mfumo wa moyo na mishipa.
Mtaalamu wa tiba kutoka Uingereza, Dk Ian Green alinukuliwa katika ripoti ya afya mwaka 2022 akisema mafuta yanayokusanyika sehemu ya juu ya mwili, hasa shingoni yana uhusiano mkubwa na hatari ya magonjwa ya moyo kuliko mafuta ya sehemu nyingine.
Kauli hii inaungwa mkono na kazi za kitafiti zinazoonyesha kuwa mafuta ya juu ya mwili, huingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa damu na kuongeza hatari ya matatizo ya kimetaboliki.
Utafiti zaidi
Mwaka 2021, utafiti uliofanywa nchini Ghana kwa wanawake wanaofanya biashara masokoni, ulibaini kuwa wanawake wenye shingo nene walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na shinikizo la damu. Pia walikuwa na viwango vya juu vya uzito kupita kiasi.
Watafiti walihitimisha kuwa kipimo cha shingo kinaweza kusaidia katika uchunguzi wa haraka wa afya katika jamii.
Katika utafiti uliofanywa Nigeria mwaka 2021 na kuchapishwa katika jarida la PubMed, watafiti waligundua kuwa wagonjwa wenye shingo nene walikuwa na viwango vya juu vya sukari na mafuta kwenye damu.
Katika tafiti mbalimbali za kimataifa, wataalamu wamegundua kuwa shingo nene ina uhusiano mkubwa na ‘insulin resistance’, hali ambayo mwili hushindwa kutumia vizuri homoni ya insulini.
Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2019 uliohusisha watu wazima kutoka nchi kadhaa, watu wenye shingo nene walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata kisukari cha aina ya pili. Pia walionyesha dalili za mapema za matatizo ya kimetaboliki.
Mwaka 2017, utafiti uliofanywa kuhusu ugonjwa wa usingizi ambapo njia ya hewa huziba au hupungua wakati mtu amelala (Obstructive Sleep Apnea -OSA) ulibaini kuwa shingo nene ni moja ya vihatarishi vikuu vya ugonjwa huo na mafuta yanayozunguka shingo huzuia njia ya hewa wakati wa usingizi.
Wataalamu walionya kuwa hali hii inaweza kusababisha kukosa usingizi wa kutosha, uchovu mkali pamoja na hata hatari ya magonjwa ya moyo.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya jamii, sababu kuu za kupendekeza kipimo cha shingo, ni urahisi wa kupima bila kutumia vifaa maalum, ni cha haraka na nafuu na kinaweza kufanyika hata katika zahanati ndogo.
Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa shingo nene si uthibitisho wa moja kwa moja wa ugonjwa bali ni kiashiria tu kinachopaswa kuambatana na vipimo vingine muhimu ambavyo ni pamoja na kiashiria cha uzito wa mwili (BMI), mzunguko wa kiuno na vipimo vya damu.
Nini cha kufanya ikiwa una shingo nene?
Wataalamu wanashauri kupima afya hospitalini mara kwa mara, kupunguza uzito kupita kiasi, kufanya mazoezi ya mwili, kula lishe bora yenye mafuta kidogo na sukari kidogo na kufuatilia shinikizo la damu na sukari.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kisayansi kutoka Afrika na duniani kote, shingo nene ni kiashiria muhimu kinachoweza kusaidia kubaini hatari za magonjwa kama, kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na matatizo ya usingizi.
Hata hivyo, kama wataalamu wanavyosisitiza shingo nene inapaswa kutazamwa kama ishara ya tahadhari, si hukumu ya ugonjwa.