Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WHO yatoa kauli mlipuko wa hantavirus

Muktasari:

  • Hantavirus ni ugonjwa nadra lakini hatari unaosababishwa na virusi vinavyosambazwa zaidi kupitia mkojo, mate au kinyesi cha panya waliobeba maambukizi.

Dar es Salaam. Wakati hofu ikitanda kimataifa baada ya mlipuko wa ugonjwa hatari wa hantavirus kuripotiwa kwenye meli ya kitalii iliyokuwa na abiria na wahudumu 147, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema hatari ya mlipuko huo kusambaa duniani bado iko chini.

Mlipuko huo uliogundulika Mei 2, 2026, watu watatu wamethibitishwa kufariki dunia na wengine kadhaa wakiwa katika hali mbaya.

Mlipuko huu umetokea ikiwa imepita takribani miaka sita tangu dunia ipitie kipindi kigumu cha mlipuko wa virusi vya corona, vilivyosababisha ugonjwa wa Uviko19 uliosababisha wagonjwa na vifo vingi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na WHO jana Jumatatu, Mei 4, 2026 pamoja na ukali wa ugonjwa huo, WHO imesema hatari ya mlipuko huo kusambaa duniani bado iko chini.

Hata hivyo, imesisitiza umuhimu wa tahadhari, hasa kwa wasafiri na wahudumu wa sekta ya utalii wanaotembelea maeneo yenye uwezekano wa uwepo wa panya.

WHO imesema jumla ya watu saba wamehusishwa na mlipuko huo wawili wamethibitishwa maabara kuwa na maambukizi ya hantavirus na watano wanashukiwa. Miongoni mwao, mmoja yuko mahututi katika chumba cha uangalizi maalum (ICU), huku wengine watatu wakiripoti dalili za awali.

Meli hiyo, yenye bendera ya Uholanzi, ilianza safari yake Aprili 1, 2026 kutoka Ushuaia na kupita maeneo mbalimbali ya kiikolojia ikiwemo Antaktika, kabla ya kusimama katika visiwa kadhaa vya Bahari ya Atlantiki. Kufikia sasa, meli hiyo imesimama karibu na pwani ya Cabo Verde huku uchunguzi ukiendelea.

Kisa cha kwanza kilihusisha mwanaume aliyepata homa na dalili za tumbo Aprili 6 akiwa ndani ya meli hiyo, kabla ya hali yake kuwa mbaya na kufariki Aprili 11.

Kisa cha pili, mwanamke aliyekuwa karibu na mgonjwa huyo, alionyesha dalili akiwa Saint Helena na baadaye kufariki Aprili 26 akiwa Johannesburg. Vipimo vilithibitisha kuwa alikuwa ameambukizwa hantavirus.

Kisa kingine kilichothibitishwa kinahusisha mwanaume aliyelazwa ICU nchini South Africa baada ya hali yake kuzorota, huku vipimo vya maabara vikithibitisha maambukizi hayo Mei 2. Kifo cha tatu kiliripotiwa Mei 2 kwa mgonjwa aliyekuwa na dalili za nimonia.

Hantavirus ni ugonjwa nadra lakini hatari unaosababishwa na virusi vinavyosambazwa zaidi kupitia mkojo, mate au kinyesi cha panya waliobeba maambukizi. Dalili zake huanza na homa, maumivu ya mwili na matatizo ya tumbo kabla ya kuendelea haraka kuwa ugonjwa mkali wa mapafu unaoweza kusababisha kifo.

Ingawa maambukizi ya mtu kwa mtu ni nadra, WHO imesema kuna ushahidi mdogo wa maambukizi ya aina hiyo, hasa kwa virusi aina ya Andes vinavyopatikana Amerika Kusini.

Hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa na nchi zinazohusika, ikiwemo Uingereza, Hispania, Uholanzi, Afrika Kusini na Cabo Verde. Hatua hizo ni pamoja na kutenga wagonjwa, kufuatilia waliokutana nao, na kufanya vipimo vya kina vya maabara.

Abiria waliopo ndani ya meli hiyo wameelekezwa kubaki vyumbani mwao kadri iwezekanavyo, kuzingatia usafi wa mikono na kuripoti dalili zozote mapema. Aidha, uchunguzi unaendelea kubaini chanzo halisi cha maambukizi hayo, ikiwemo uwezekano wa kuhusika kwa mazingira yenye panya au mwingiliano na wanyamapori wakati wa safari.

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa hakuna chanjo wala tiba maalum ya hantavirus kwa sasa, lakini matibabu ya mapema na uangalizi wa karibu hospitalini yanaweza kuongeza nafasi ya kupona.