Haya ndiyo majibu ya TFRA kuhusu mahitaji ya mbolea nchini
Muktasari:
- Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Lazaro Kitandu anasema mahitaji ya mbolea yameongezeka kwa asilimia 20 kwa msimu wa 2017/18 baada ya utekelezaji wa mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System).
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara zenye matumizi madogo ya mbolea ikitumia wastani wa kilo 19 za virutubisho kwa hekta moja sawa na asilimia 38 ya azimio la Maputo lililoweka lengo la kuongeza matumizi ya mbolea kufikia angalau kilo 50 za virutubisho kwa hekta moja.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Lazaro Kitandu anasema mahitaji ya mbolea yameongezeka kwa asilimia 20 kwa msimu wa 2017/18 baada ya utekelezaji wa mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System).
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Kitandu alisema ongezeko la mahitaji ya mbolea ndiyo limesababisha kuonekana kuna upungufu.
Swali: Kwa nini kumekuwa na malalamiko ya upungufu wa mbolea tangu mfumo wa ununuzi wa pamoja ulipoanza?
Jibu: Mfumo huu wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) unatofautiana na ule wa ruzuku kwani ule ulikuwa ukipeleka mbolea hata sehemu ambazo haikuhitajika kwa fedha ya ruzuku ya Serikali.
Leo hii mfumo huu umeweza kupunguza bei ya mbolea kati ya asilimia 11 hadi40 na kila mkulima amenufaika na mfumo huu tofauti na wakati wa ruzuku, wakulima chini ya asilimia 10 waliweza kunufaika na changamoto nyingi zilijitokeza.
Sasa baada ya mbolea kushuka bei, mwitikio wa watu kununua mbolea umekuwa mkubwa.
Swali: unazo takwimu zinazoonyesha ongezeko la mahitaji?
Jibu: Mwaka jana tuliagiza Urea tani 122,000 lakini tulitumia 88,600 tu, tukabakiwa na tani 33,400. Kwa hiyo ilitumika karibu tani 90,000 tu mbolea hiyo.
Asilimia 60 ya mbolea hiyo iilitumika Nyanda za juu Kusini. Kwa wastani, kila mkoa ulitumia tani 8,000 za urea. Hakuna mkoa uliowahi kutumia zaidi ya tani 8,000 za urea kwa msimu mmoja.
Kwa msimu huu wa sasa (2017/18), hadi Februari hii, tumeshatumia tani 115,000 za urea. Kutoka 90,000, kuna ongezeko la karibu la asilimia 12 na hapo bado msimu haujaisha. Kwa hiyo tunategemea hadi msimu utakapomalizika, tutakuwa tumetumia takriban tani 150,000 za urea peke yake.
Kwa hiyo utaona kuna hamasa ya wakulima wengi kutumia mbolea na sisi tunaona hili ni jambo jema ambalo tumekuwa tukihiji litendeke ili uzalishaji na tija iongezeke kusudi tuimarisha usalama wa chakula nchini.
Swali: Unasema mikoa inayozalisha chakula kwa wingi inatumia wastani wa tani 8,000 kwa msimu kila mkoa. Mbona baadhi ya maofisa ugani wanataja takwimu kubwa zaidi?
Jibu: Kuna tatizo la takwimu ndiyo maana manispaa na hamshauri zinapata changamoto za kutoa takwimu sahihi za matumizi ya mbolea. Mathalani utakuta mtaalamu anasema mkoa unatumia tani 49,000 za urea, wakati kwa uhalisia matumizi hayo hayajafikiwa.
Matumizi makubwa ya mbolea yako Nyanda za juu Kusini wanaotumia asilimia 60 ya mbolea hii ya urea ambayo ni sawa na takribani tani 54,000 kwa msimu.
Kwa hiyo tulipofanya ufuatiliaji kwa mikoa iliyoomba kiasi kikubwa cha mbolea tulipokwenda kukagua, tukakuta wamepiga hesabu kulingana na mahitaji ya udongo badala ya mahitaji ya wakulima.
Kwa mfano, mtaalamu anaangalia udongo huu unahitaji tani kadhaa, mkoa wangu una ekari kadhaa. Kwa hiyo anazidisha hesabu ya mahitaji ya udongo kwa idadi ya hekta zinazotegemewa kulimwa katika mkoa husika. Kwa uhalisia mkulima anaweza kuwa na matarajio ya kutumia mifuko 10 lakini akanunua mifuko minne kulingana na uwezo wake kifedha.
Kwa mfano tulipoomba mahitaji ya urea kwa kila mkoa, tulipata mahitaji ya jumla ya tani 1.2 milioni kwa urea pekee, hakiwezekani kwa mwaka mmoja au miwili ijayo. Hata mahitaji ya mbolea zote za kupandia na kukuzia kwa msimu uliopita tulitumia tani 215,000 tu.
Swali: Kwa nini msiagize mbolea nyingi na kuwahamasisha zaidi wakulima watumie?
Jibu: Nimekupa takwimu za msimu uliopita kwamba tulitumia tani 90,000 za urea, mwaka huu tunaweza kufikia tani 150,000 kwa kiwango cha juu. Sasa ukiletewa tani 1.2 milioni nani atazinunua?
Ni kweli watu wana hamasa ya kutumia mbolea, lakini takwimu bado ni tatizo. Takwimu tulizonazo ni zile za mauzo ya mbolea za mawakala.
Tukiweza kupata takwimu zote za mbolea kutoka kwa mawakala, ukweli utafahamika. Ili kupanga malengo ya mbele, huwa tunaweka ziada ya asilimia 20 hadi 25 kwa msimu unaofuata.
Msimu unaofuata tutaweka malengo makubwa zaidi na hii bei ilivyoshuka inalenga kuongeza kiwango cha matumizi ya mbolea hapa nchini.
Swali: Awali kulikuwa na mzozo kuhusu bei hali iliyomfanya Waziri wa Kilimo atoe agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kujadili upya bei na mawakala, tatizo lilikuwa nini?
Jibu: Awali mbolea za kupandia ikiwemo (DAP), hazikuonyesha changamoto kwa sababu hakukuwa na tatizo la mvua. Mvua iliponyesha iliharibu miundombinu kwa baadhi ya barabara na kuleta changamoto kubwa kwa baadhi ya maeneo. Ndiyo maana Waziri wa Kilimo alitoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kukaa na wafanyabiashara ili kurekebisha mahali ambako bei elekezi haina uhalisia.
Bei elekezi inamsaidia mkulima na pia mfanyabiashara kupunguza tofauti za kimaslahi na zile faida zilizozoeleka huko nyuma, ambazo hazikumsaidia mkulima.
Agizo la Waziri halikulenga pia ongezeko la bei ya mbolea inayosambazwa sasa. Mbolea hizo bei zake hutegemea soko la dunia au la kimataifa. Ni kama ilivyo kwenye mafuta, yakipanda bei na sisi huku kwetu bei inapanda na yakishuka na sisi bei inashuka.
Swali: Sambamba na hilo, hivi karibuni mmepandisha bei ya mbolea, je ni kwa sababu ya malalamiko ya mawakala?
Jibu: Hapana. Hii mbolea inayosambazwa imeingia hivi karibuni na kwenye soko la dunia imepanda bei. Kwenye soko la dunia bei ya urea imepanda kwa takribani dola za Marekani 70. Kama tungeachia soko huria, Dar es Salaam ingeuzwa Sh54,000 badala ya 47,400 ilivyo sasa. Lakini kwa kuwa tumetumia mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja, kwa kuruhusu ushindani kupitia zabuni tumepata mbolea hii kwa dola 267 tofauti na dola 310 - 330 iliyoko kwenye soko la dunia.
Lengo la Serikali ni kuwasaidia wakulima na bei hizi zinazobadilika kutokana na mwenendo wa soko la dunia.
Kuanzia Mei hadi Julai kila mwaka, bei ya mbolea hushuka kwa sababu nchi zinazoitumia kwa wingi zinakuwa zimemaliza msimu wa kilimo hususan nchi za India na Brazil.
India peke yake inatumia kati ya tani 8 milioni hadi 10 na Brazil hivyo hivyo. Sisi mbolea tunayoagiza haizidi tani 400,000. Lakini tunayotumia ndani ya nchi kwa mwaka haizidi tani 250,000.
Kwa vile tunaagiza mbolea ya hapa kwetu na nchi nyingine ambazo hazina bandari, wafanyabiashara hao hao wanafanya biashara na nchi nyingine.
Kwa mfano mwaka jana, tulikuwa na tani 389,135, lakini mbolea aina zote iliyobaki nchini ilikuwa tani 215,000. Kwa sasa zaidi ya asilimia 50 ya mbolea inayotumika hapa nchini ni mbolea ya kukuzia, urea ikiongoza. Mbolea zingine za kukuzia ni pamoja na CAN, SA, NPK nk.
Swali: Hivi karibuni mmeagiza mbolea nyingine ya Urea kupitia Kampuni ya Export Trading Company, tani 20,000. Je, kampuni zilizoshinda zabuni awali zilielemewa?
Jibu: Hapana, suala la kuelemewa halipo ila kati ya watu walioshindana katika zabuni iliyopita ETG ndio alikuwa mshindi na alipewa zabuni ya kuleta mbolea na wengine watanunua na kusambaza kutoka kwake.
Tukishapata mahitaji yote kwa jumla, tunampa aliyeshinda zabuni ili aagize kwa niaba ya wenzake waliokosa zabuni hiyo. Mbolea inapoletwa wao wanachukulia bandarini kwa bei ile ile ya zabuni.
Ni kweli hawa wasambazaji siyo wa kudumu, mwingine anaposhinda anapewa kwa bei ile ile. Tulipotangaza zabuni mwezi huu mwanzoni, hao wengine waliokuwa na bei ya juu tuliwaacha tukawapa ETG.
Swali: Mna mikakati gani ya kuagiza mbolea kwa msimu huu wa masika unaotarajiwa kuanza Machi?
Jibu: Kwa sasa mbolea hii ya kupandia (DAP) tumefanya mazungumzo na Morocco tumekubaliana watuletee nyingi kwa bei ya chini na tayari kuna mkataba wa kutuleta mbolea ya DAP tani 100,000 ambayo italetwa kwa awamu tofauti.
Februari 20 zitaletwa tani 32,000 za DAP ambayo tunadhani itasaidia kwa kanda ambayo msimu wake unaanza hivi karibuni na wale wanaofanya kilimo cha umwagiliaji.